WASANII WA FILAMU KUNUFAIKA NA KAZI ZAO

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni  na Michezo Dkt. Fenella Mukangara akiongea na baadhi ya Viongozi wa mashirikisho ya wasanii wa filamu na Muziki kuhusu urasimishaji wa kazi za wasanii wa Filamu na Mziki jijini Dar es Salaam (jana). (Picha na Benjamin Sawe wa WHVUM)

Na Concilia Niyibitanga- WHVUM

Serikali imeamua kuweka mfumo rasmi utakaowawezesha Wasanii wa Filamu na Muziki nchini   kunufaika na kazi wanazozibuni na kuzitengeneza.

Hayo yamesemwa leo  Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara wakati akiongea na Viongozi wa Mashirikisho  ya Wasanii wa Filamu na Muziki.

Dkt. Mukangara amesema kuwa Serikali imesikia kilio cha Wasanii kwa kuirasimisha Sekta ya Filamu na Muziki ili kuondokana na kilio cha muda mrefu cha Wasanii kutonufaika na jasho lao.

Amesema kuwa Serikali itatumia mfumo wa kuziwekea kazi hizo stampu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo zitakuwa na usalama kwa nia ya kuondokana na uzalisha na udurufishaji ovyo wa kazi hizo na kazi hizo zitawekewa ‘bar code’ kwa wepesi wa ufuatiliaji.

Urasimisaji huu unaotarajia kuanza rasmi Januari, 2013 utawezesha wasanii kukopesheka ili kupata mitaji itakayowawezesha kutengeneza kazi bora na zenye viwango  na zitakazoweza  kuingia katika soko la ushindani. Ameeleza Dkt. Mukangara.

Amesema kuwa kwa sasa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo; Wizara ya Fedha; na Wizara ya Viwanda na Biashara zinaweka katika mfumo wa kielektroniki taratibu zinazowezesha utekelezaji wa mfumo huu kuwa rahisi.

Aidha, Dkt. Mukangara ametoa wito kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake katika kuhakikisha  kero ya Wasanii kuibiwa na kutofaidika na kazi zao inaondoka na kuwataka vijana kujipanga vizuri ili kuitumia fursa hii na hata katika siku za usoni waweze kuwa na  Saccos za vijana katika tasnia ya filamu na muziki na waweze kukopesheka kupitia Mfuko wa Vijana.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi, Bw. Adrian Nyangamalle ameipongeza Serikali kwa hatua ya kuirasimisha Sekta ya Filamu na Muziki na kuiomba Serikali kuangalia uwezekano pia wa kurasimisha Sanaa za Ufundi ambazo zinaonekana kusahaulika  katika  mfumo huo.

Bw. Nyangamalle amesema kuwa katika Wasanii milioni 9 nchini, takribani Wasanii milioni 4 ni Wasanii wa Ufundi, hivyo ni changamoto kwa Serikali hususan Wizara yenye dhamana na Sekta hiyo kuona umuhimu wa kurasimisha kazi za Sanaa za Ufundi.

Popular posts from this blog

MAMBO 6 YA KUZINGATIA KATIKA MAHUSIANO

Mwanajeshi Aliyepiga Picha na Mbunge wa Arusha Mjini-Chadema Godbless Lema Kwenye Mkutano wa Hadhara Akamatwa

MATAJIRI WATANO WANAOONGOZA TANZANIA