HOTUBA YA MHESHIMIWA PEREIRA AME SILIMA (MB), MWENYEKITI WA BARAZA LA TAIFA LA USALAMA BARABARANI (T)
HOTUBA
YA MHESHIMIWA PEREIRA AME SILIMA (MB), MWENYEKITI WA BARAZA LA TAIFA
LA USALAMA BARABARANI (T) KWENYE UFUNGUZI WA MAADHIMISHO YA WIKI YA
NENDA KWAUSALAMA BARABARANI KITAIFA MKOANI IRINGA TAREHE 17 SEPTEMBA,
2012
Mhe. Mgeni Rasmi
Mhe. Eng. Gerson Hosea Lwenge (Mb), Naibu Waziri wa Ujenzi na Makamo Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani
Ndugu Mbarak Abdulwakil, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Ndugu Herbert Mrango, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi
Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (Mb), Mkuu wa Mkoa wa Iringa
Ndugu Said Ally Mwema, Inspekta Jenerali wa Polisi
Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa
Wajumbe wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani (T)
Wageni Waalikwa
Wanahabari
Mabibi na Mabwana
Asalaam Aleikum, Amani ya Mungu iwe juu yenu
Awali
ya yote napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwako Mhe. Mgeni rasmi
kwa kukubali kwako kuungana nasi katika ufunguzi wa wiki ya
maadhimisho ya nenda kwa usalama barabarani ambayo kitaifa
inaadhimishwa hapa mkoani Iringa. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka
huu ni
“PAMBANA NA AJALI ZA BARABARANI KWA VITENDO, ZINGATIA SHERIA”
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Maadhimisho
ya Wiki hii yana lengo la kuelimisha na kukumbushana wajibu wa kila
mtumiaji wa barabara katika kufuata sheria za usalama barabarani. Ni
katika kipindi hiki BARAZA ambacho hufanya maadhimisho haya kwa
kuwakusanya wadau mbalimbali wa usalama barabarani kwa ajili ya
kujikumbusha au kujifunza. Maonesho huwawezesha wananchi (wadau)
kujifunza pamoja na mambo mengine, sheria na kanuni mbalimbali za
usalama barabarani. Katika maadhimisho haya wadau watakaoshiriki ni
Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Wizara ya Ujenzi, Wakala
wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi
Kavu na Majini (SUMATRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Scania
Tanzania Ltd, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji na Mashirika yasiyo ya
kiserikali yanayojihusisha na Usalama Barabarani.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Tangu
nimeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa BARAZA hili nimeweza kujionea matatizo
na changamoto mbalimbali zinazohusiana na masuala ya usalama barabarani
ambazo mimi pamoja na wajumbe wa BARAZA tumekuwa tukikutana mara
kadhaa katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo na changamoto
zinazotukabili. Suala la usalama barabarani linawahusisha wadau
mbalimbali, hivyo kila mdau akitekeleza wajibu wake, ajali za
barabarani zitapungua kama sio kumalizika kabisa.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Pamoja
na jitihada nzuri inayofanywa na Serikali kuboresha Miundombinu ya
barabara bado kuna tatizo kubwa la madereva na wapanda pikipiki kutojali
Sheria na kanuni za usalama barabarani. Kikubwa kinachochangia ajali
hizi ni makosa ya kibinadamu kwa asilimia 78, ubovu wa magari kwa
asilimia 12, miundombinu ya barabara kwa asilimia 4 na mengineyo kama
moto, hali ya hewa nk kwa asilimia 8.
Katika makosa ya kibinadamu, makosa yanayoongoza ni:-
Mwendokasi
Uzembe wa madereva
Uzembe wa wapanda pikipiki
Uzembe wa wapanda baiskeli
Uzembe wa watembea kwa miguu
Madereva kuendesha magari wakiwa wametumia vilevi
Mhe. Mgeni Rasmi,
Kwa
kuwa makosa ya kibinadamu ndiyo yanayoongoza katika kuchangia ajali
nyingi za barabarani, BARAZA la Taifa la Usalama Barabarani
likishirikiana na Polisi kikosi cha Usalama Barabarani pamoja na wadau
wengine wa usalama barabarani limekuwa na mikakati mbalimbali katika
kukabiliana na ajali hizo.
Tumekuwa
tukitoa Elimu ya Usalama Barabarani kwa watumiaji wote wa barabara
kupitia vyombo vya Habari (Redio na Televisheni). Hadi sasa kuna jumla
ya vituo vya Radio 48 nchi nzima vinavyotumika kutoa elimu ya usalama
barabarani.
Kuchapisha vipeperushi vya Elimu ya Usalama Barabarani na kuvigawa maeneo mbalimbali.
Askari
wa Usalama Barabarani kwenda katika shule za Msingi na Sekondari
kuwafundisha wanafunzi na walimu, kutoa elimu kwa watu mbalimbali wakati
wa Maonyesho ya Sabasaba na Nanenane. Aidha, Elimu hutolewa katika
Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani.
Kuhakikisha kwamba kila anayeomba Leseni ya Udereva lazima awe amesoma katika Chuo kinachotambulika na Serikali.
Kuhakikisha
kwamba madereva wote wa Magari ya Abiria wanakuwa wamesomea na kupata
Cheti cha kuendesha magari ya abiria kibiashara (PSV Certificate) toka
Vyuo vya NIT na VETA.
Kusisitiza mabasi yote yanayosafiri Masafa marefu kuwa na Madereva wawili wakati wote wa safari.
Askari wa Usalama Barabarani kufanya Doria katika barabara kuu na barabara za ndani ya Mikoa.
kuwashirikisha
wananchi katika kutoa taarifa mbalimbali za uvunjaji wa sheria za
Usalama Barabarani kupitia Namba za simu za Viongozi wa Polisi zilizopo
kwenye Vipeperushi na ile ya Chumba cha Mawasiliano ya Polisi. Aidha,
katika mabasi yaendayo mikoani kuna namba za Simu zimebandikwa kwa ajili
ya abiria kutoa taarifa ya makosa ya madereva.
Kushirikiana
na wadau wa Usalama Barabarani kama Wizara ya Ujenzi, Wizara ya
Uchukuzi, SUMATRA, TANROADS, TBS, BIMA, TABOA, TATOA, DARCOBOA nk.
katika kukabiliana na ajali za barabarani na madereva wakorofi wasiotii
sheria.
Kuendelea
kuishauri Serikali kuifanyia marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani
ili itoe adhabu kali kwa madereva wasiotaka kufuata sheria. Mhe. Mgeni
rasmi kwa sasa sheria ya usalama barabarani inayohusu tozo
(notification) imerekebishwa kutoka Tshs. 20,000.00 hadi kufikia Tshs.
30,000.00
Kufuatia
kuanza kwa matumizi ya leseni mpya za udereva, utaratibu wa kuweka
points katika leseni za madereva wanaofanya makosa utaanza kutumika, ili
hatimaye madereva wanaokithiri kwa makosa wanyang’anywe leseni kabisa.
Mchakato
wa kuanzisha mfumo wa “Car Tracking” utakaomilikiwa na Serikali upo
mbioni kukamilishwa ili kudhibiti mwendokasi wa mabasi yanayosafiri
masafa marefu.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Ni
lengo letu kutekeleza kikamilifu mikakati tuliyojiwekea ili ifikapo
2020 vifo na majeruhi wa ajali za barabarani viwe vimepungua kwa
asilimia 50 kama Azimio la Umoja wa Mataifa lilivyoelekeza.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Takwimu
zinaonyesha kwamba kati ya Januari – Juni, 2012 jumla ya matukio ya
ajali 11,163 yaliripotiwa ambapo jumla ya wenzetu 1,808 wamepoteza
maisha yao kutokana na ajali hizo. Aidha, jumla ya watu 9,155
walijeruhiwa katika kipindi hicho.Kati ya ajali zote 11,163
zilizoripotiwa, ajali 2,641 ambazo ni sawa na asilimia 24 zimehusisha
pikipiki.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Naomba
kupitia Hotuba hii kwenye maadhimisho haya ya wiki ya nenda kwa
usalama barabarani hapa Mkoani Iringa, niwape pole wafiwa wote
waliopoteza wapendwa wao, na wale wote waliopata ulemavu wa maisha
kutokana na ajali za barabarani. Aidha, nawaombea pia majeruhi wote
kupona haraka ili warudi kwenye kazi zao za kulijenga taifa.
Ndugu Mgeni Rasmi;
Nimalizie
hotuba yangu, kwanza kwa kurudia kukushukuru wewe binafsi kwa kukubali
mwaliko wetu. Aidha, niwatake wananchi wote wa Mkoa wa Iringa na
vitongoji vyake kuwa na mwamko wa kutembelea maadhimisho haya kwenye
viwanja hivi ili waweze kuelimishwa mambo mbalimbali ya usalama
barabarani ili kujikinga na ajali za barabarani.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Baada ya kusema hayo, sasa napenda kuchuka fursa hii kukukaribisha ili uweze kutoa nasaha zako .
“PAMBANA NA AJALI ZA BARABARANI KWA VITENDO, ZINGATIA SHERIA”