BODI YA WATALII WAPONGEZWA
Na: Geofrey Tengeneza
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imepongezwa kwa kazi nzuri inayofanya
katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwa ni pamoja na jukumu kubwa
la kuitangaza Tanzania kama eneo bora lenye vivutio vingi vya kitalii
duniani pamoja na ushindani mkubwa kutoka nchi nyingine na hivyo kufanya
idadi ya watalii wanotembelea nchi yetu kuendelea kuongezeka mwaka hadi
mwaka sambamba na kuongezeka kwa pato la Taifa litokanalo na sekta ya
utalii.
Akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Utalii
hivi karibuni katika ukumbi wa Mikutano wa chuo cha Utalii jijini Dar
es salaam Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bibi Maimuna
Tarish amesema Bodi ya Utalii imeendelea kutekeleza vema majukumu yake
na kwamba wafanyakazi wa taasisi wana kila sababu ya kujivunia mafanikio
haya kwa kuwa kila mmoja kwa nafasi yake amechangia katika mafanikio
hayo. Amewataka wafanyakazi kuendelea kuwa wabunifu zaidi
kwa kuibua mawazo mapya yatakayosaidia kuboresha utendaji wa Bodi siku
hadi siku na kujipima kwa matokeo ya kazi na mipango wanayojiwekea.
“Nawaomba sambamba na kuwa na mipango ya kazi mfanye kazi kwa matokeo
na kuwa wabunifu kadri iwezekanavyo kwa kila mfanyakazi kujitahidi kuwa
na mawazo mapya ambayo yatasaidia shirika kuboresha utekelezji wa majukumu
majukumu yake” alisema Bibi Maimuna.
Akizungumzia mikutano ya Baraza la Wafanyakazi sehemu za kazi Katibu
Mkuu huyo amesema jambo muhimu sana katika kutatua baadhi ya matatizo
yanayoikabili taasisi husika kwa kuwa mikutano hiyo ndicho chombo cha
juu kabisa ambacho wafanyakazi kupitia wawakilishi na viongozi wao wa
vyama vya wafanyakazi na Menejimenti wanapata fursa ya kukaa pamoja
na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu taasisi na wafanyakazi kwa
ujumla. Amesema kwa kufanya hivyo ni kutekeleza kwa vitendo agizo la
serikali linalolenga katika kuendeleza na kudumisha utawala bora jambo
ambalo linadumisha umoja na mshikamano baina ya wafanyakazi.
Baraza hili jipya la wafanyakazi wa Bodi ya Utalii Tanzania pamoja
na mambo mengine kadhaa katika kikao chake hicho cha siku mbili lilipokea
na kujadili makadirio ya mapato na matumizi ya Bodi katika kipindi cha
mwaka 2012/2013, na taarifa ya utekelezaji wa mipango na kazi
mbali mbali za Bodi katika kipindi cha Julai 2011 hadi Machi 2012.
Utalii nii Sekta ya pili nchini kwa kuchangia katika pato la Taifa
ambapo inachangia kiasi cha asilimia 17.2 baada sekta ya Madini ambayo
ndiyo inaongoza. Aidha kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2011 idadi ya
watalii waliotembelea Tanzania kutoka nchi mbalimbali duniani iliongezeka
kutoka watalii 782,699 mwaka 2010 hadi watalii 867,994. Nayo mapato
yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka dola za Kimarekani 1,254.50
mwaka 2010 hadi ufikia dola za kimarekani 1,348,30