AZAM FC WAANZA KUSAKA UPEPO
Wachezaji wa Azam
WASHINDI wa Medali ya Fedha ya Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, Azam FC leo wanaanza rasmi mazoezi kwenye Uwanja
wao, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kujiandaa na michuano ya
Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Kagame.
Kulingana na
programu ya maandalizi, Azam FC wataanza mazoezi leo asubuhi, Uwanja wa
Azam Complex, Chamazi maalum kwa mashindano hayo yatakayofanyika mwezi
ujao mjini Dar es Salaam.
tayari wachezaji wa Azam kutoka nje ya Tanzania wamewasili mapema wiki hii na wamepatiwa makazi.
Usajili kwa
wachezaji Azam ulikwishamalizika kabla ya wachezaji kwenda likizo, hivyo
wachezaji wote waliosajiliwa wataanza mazoezi isipokuwa wale walioko
kwenye timu zao za taifa, Tanzania, Uganda na Zanzibar, ambazo zipo
kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa wikiendi hii.
Programu ya
maandalizi ya Kombe la Kagame, itamalizika siku moja kabla ya kuanza
mashindano hayo na yatakapomalizika, wachezaji watapewa mapumziko ya
siku chache kabla ya kuanza maandalizi kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi
Kuu.
Maandalizi kwa
ajili ya VPL yatahusisha pia ziara ya nje ya nchi ya kujiandaa na msimu
mpya, ingawa amesema nchi hiyo itatajwa baadaye.
Wachezaji wapya
kiikosini Azam msimu huu ni kiungo Mkenya George ‘Blackberry’ Odhiambo
na kipa Deogratius Munishi kutoka Mtibwa Sugar, wakati Aishi Salum,
Jackson Wandwi, Dizana, Ibrahim Rajab Jeba na Joseph Kimwaga,
wamepandishwa kutoka akademi ya Azam.
Kikosi kamili
cha Azam FC kinaundwa; na makipa, Mwadini Ally, Deo Munishi ‘Dida’ Aishi
Salum na Jackson Wandwi, mabeki wa Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni,
Waziri Salum, Samir Haji Nuhu, Luckson Kakolaki, Said Mourad, Joseph
Owino na Aggrey Morris.
Viongo ni Kipre
Bolou, Abdulhalim Humud, Himid Mao, Salum Abubakar, Abdi Kassim
Sadalla, Ramadhani Suleiman Chombo, Abdulghani Ghullam, Ibrahim Rajab
Jeba, Jabir Aziz Stima, Ibrahim Joel Mwaipopo, Kipre Tchetche, Mrisho
Ngassa, Zahoro Pazi, Khamis Mcha na George Odhiambo ‘Blackberry’ wakati
washambuliaji ni Gaudence Mwaikimba, John Bocco ‘Adebayor’.
Hii ni mara ya
kwanza kwa Azam FC kucheza Kombe la Kagame, baada ya kushika nafasi ya
pili katika msimu uliopita wa Ligi Kuu. Katika Kombe la Kagame mwaka
huu, wenyeji Bara wataingiza timu tatu, Yanga ambao ni mabingwa
watetezi, wakati Simba na Azam wanaingia kwa nafasi za uwakilishi.