LEO NI SIKU YA IBADA

   Leo ni Alkhamisi tarehe Mosi Shaaban mwaka 1433 Hijria sawa na tarehe 21 Juni 2012 Miladia.
Mwezi wa shaabani unaoanza leo ni mwezi wa ibada, kujipinda na kuomba maghufira. Mtume Muhammad (saw) aliutukuza mno mwezi huu na kuuita kuwa ni Mwezi wa Mwenyezi Mungu SW. Mtume na maimamu watoharifu katika kizazi chake waliusia mno kufanya ibada hususan kufunga swaumu katika mwezi huu wa Shaabani kwa sababu ndio unaotayarisha uwanja mzuri wa kuingia kwenye mwezi wa ugeni wa Mwenyezi Mungu na wenye baraka tele wa Ramadhan.
Katika mwezi huu wa Shaabani kumetukia mambo mengi muhimu kama kuzaliwa Imam Hussein bin Ali (as) mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw) na pia tukio la kuzaliwa Imam wa Zama Mahdi (as) Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake.
Tarehe Mosi Shaabani miaka 167 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Sheikh Muhammad Hassan Najafi maarufu kwa lakabu ya Sahib al Jawahir. Sahib al Jawahir alifanya uhakiki mkubwa wa masuala ya fiqhi na kusajili fikra zake katika taaluma hiyo kwa njia ya kuvutia na nyepesi. Kitabu kikubwa zaidi cha mwanazuoni huyo ni "Jawahirul Kalam" ambacho kina thamani na umuhimu mkubwa sana kati ya wataalamu wa taaluma hiyo. Katika kitabu hicho Sheikh Muhammad Hassan Najafi ameandika masuala ya kifiqhi na sheria za Kiislamu kwa kutumia hoja madhubuti na uangaklifu mkubwa.
Na siku kama ya leo miaka 31 iliyopita Imam Ruhullah Khomeini alipasisha mtazamo wa Bunge la Iran wa kumuuzulu Bani Sadr aliyekuwa Rais wa wakati huo wa Iran. Bani Sadr alikuwa miongoni mwa watu waliojidhihirisha kama watetezi wa Mapinduzi ya Kiislamu baada ya Imam Khomeini kubaidishiwa mjini Paris Ufaransa na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alitumia ujanja na propaganda kubwa zilizowahadaa watu kumpa kura za urais. Baada ya kuchukua madaraka Bani Sadr ambaye alikuwa mtu mwenye kiburi, mpenda jaha na mtenda jinai alianza kushirikiana na makundi yaliyokuwa yakipinga Mapinduzi ya Kiislamu kwa lengo la kuangusha serikali ya Kiislamu nchini Iran. Baadaye Imam Khomeini alimuuzulu cheo cha kamanda wa majeshi ya Iran na kufuatiwa na kura ya Bunge ya kumuuzulu urais wa Jamhuri. Baada ya kuuzuliwa Bani Sadr alikimbilia nchini Ufaransa.

Popular posts from this blog

MAMBO 6 YA KUZINGATIA KATIKA MAHUSIANO

Mwanajeshi Aliyepiga Picha na Mbunge wa Arusha Mjini-Chadema Godbless Lema Kwenye Mkutano wa Hadhara Akamatwa

MATAJIRI WATANO WANAOONGOZA TANZANIA