Taarifa Rasmi Kutoka IKULU Kuhusu Ziara ya Rais Jakaya Kikwete Uwanja wa Michezo wa Azam Complex ulioko Chamazi, Temeke, Dar es Salaam unaomilikiwa na Kampuni ya Saidi Bakhressa Group Alhamisi iliyopita, Machi 21, 2013.


 Rais Jakaya Kikwete
--


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete 


alitembelea na kuzindua rasmi Uwanja wa Michezo wa Azam Complex ulioko Chamazi, 

Temeke, Dar es Salaam unaomilikiwa na Kampuni ya Saidi Bakhressa Group Alhamisi 

iliyopita, Machi 21, 2013.


Rais Kikwete alizindua Uwanja huo wa Azam Complex unaotumiwa na Klabu ya Soka ya Ligi 

Kuu ya Tanzania Bara ya Azam FC ikiwa ni tukio la mwisho la ziara yake yenye mafanikio 

makubwa ya siku nne katika Mkoa wa Dar Es salaam.


Wakati wa hotuba yake ya uzinduzi wa Uwanja huo, Mheshimiwa Rais Kikwete aliipongeza 

Klabu ya Azam kwa kuwa dira na mfano nzuri wa  kuendeleza soka nchini na kuwekeza 

katika  maendeleo ya mchezo huo unaopendwa na wenye washabiki wengi nchini kwa njia za 

kisasa.


Tokea siku hiyo ya Alhamisi, Vyombo mbali mbali vya habari nchini yakiwemo magazeti 

vimetangaza na kuandika habari nyingi na wachambuzi wa michezo wameandika maoni na 

uchambuzi wao wa kila aina kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Rais Kikwete kwenye hafla hiyo.


Wengine wameandika vizuri kwa mujibu wa ujumbe wa Rais Kikwete kwa wanamichezo wa 

Tanzania na taasisi za michezo katika nchi yetu. Lakini kwa bahati mbaya, wapo wachache 

ambao wamepindisha ujumbe huo, wengi wao wakimlisha maneno ambayo hakuyatamka 

Mheshimiwa Rais.


Aidha, wengine wamejaribu kutumia kauli ya Rais Kikwete kuwashambulia wapinzani ama 

washindani wao katika soka. Katika ari ya kila mtu kuzusha jambo lake chini ya kivuli cha 

kauli ya Rais Kikwete, wengine hata wametumia michoro ya katuni kwenye magazeti ili 

“kufafanua” kile alichokisema Mheshimiwa Rais.


Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda kutoa ufafanuzi wa baadhi ya kauli hizo 

za vyombo vya habari kama ifuatavyo:



(a)Kwamba nia ya Mheshimiwa Rais Kikwete kwenye hotuba yake ilikuwa kupongeza 

jitihada za Klabu ya Azam na Kampuni mama ya klabu hiyo Bakhressa Group kwa kuchukua 

njia sahihi na za kisayansi kuendeleza mchezo wa soka nchini.



(b)  Kwamba haikuwa nia ya Mheshimiwa Rais kuzikemea ama kuzisema taasisi nyingine za 

soka katika Tanzania ambazo nazo kwa namna yake zinachangia maendeleo ya soka katika 

nchi yetu.



(c)                Kwamba, Mheshimiwa Kikwete,  kama mpenzi wa soka na michezo maisha yake 

yote anatambua na kuheshimu mchango wa Klabu za Soka za Simba na Yanga na

 changamoto ambazo zinazikabili klabu hizo katika kuinua kiwango cha michezo nchini. 

Hivyo, ni jambo lisilowezekana kuwa yeye anaweza kuzikejeli kwa namna yoyote hizo klabu 

hizo kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari vimejaribu kuelezea tokea alipozindua 

Azam Complex.



Hakuna shaka kuwa Rais Kikwete anajua fika na anaamini kuwa waandishi wa michezo 

nchini wanafanya kazi kubwa na nzuri na wakati mwingine katika mazingira magumu ya 

kuwahabarisha, kuwaelimisha na kuwaburudisha wananchi kuhusu michezo na maendeleo 

yake nchini. Ushauri wake ni kwamba waendelee kufanya jitihada zaidi za kuongozwa na 

misingi ya taaluma, weledi na ukweli zaidi katika kuifanya kazi yao.

Popular posts from this blog

MAMBO 6 YA KUZINGATIA KATIKA MAHUSIANO

Mwanajeshi Aliyepiga Picha na Mbunge wa Arusha Mjini-Chadema Godbless Lema Kwenye Mkutano wa Hadhara Akamatwa

MATAJIRI WATANO WANAOONGOZA TANZANIA