Ndugu Wananchi, Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza nusu ya kwanza ya mwaka 2012 salama. Kwa kutumia utaratibu wetu wa kuzungumza nanyi kila mwisho wa mwezi, leo napenda kuzungumzia mambo mawili. Jambo la kwanza ni suala la usafirishaji haramu wa binadamu nchini na la pili ni la mgomo wa madaktari. Usafirishaji Haramu wa Binadamu Nchini Ndugu Wananchi; Bila ya shaka mtakuwa mmezisikia taarifa za tukio la kushtusha na kuhuzunisha la kukutwa maiti 43 za watu wasiojulikana, zilizotupwa katika kichaka kilichopo kijiji cha Chitego, Wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma tarehe 26 Juni, 2012. Pamoja na maiti hao, walipatikana watu 84 wakiwa hai lakini wote wakiwa wamedhoofu na baadhi yao wakiwa mahututi. Hatua za haraka z...