MANAHODHA STARS WANG'ARA VODACOM
Nahodha wa Taifa Stars, Juma Kaseja na msaidizi wake Aggrey Morris wameng’ara katika hafla ya kampuni ya Vodacom kukabidhi zawadi kwa wachezaji, klabu, waamuzi na makocha waliofanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2011/2012.
Katika hafla hiyo iliyofanyika jana usiku (Juni 30 mwaka huu) hoteli ya Double Tree Hilton, Dar es Salaam, Morris anayechezea Azam aliibuka mchezaji bora wa ligi hiyo wakati Kaseja anayedakia Simba alikuwa kipa bora.
Kila mmoja alizawadiwa sh. 3,312,500 katika hafla hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye. Kaseja aliwashinda makipa Mwadili Ally (Azam) na Deogratias Munishi (Mtibwa Sugar) wakati Morris aliwashinda Haruna Niyonzima (Yanga) na Haruna Moshi (Simba).
John Bocco wa Azam aliyefunga mabao 19 ndiye mfungaji bora, refa bora ni Martin Saanya kutoka Morogoro ambaye aliwashinda Oden Mbaga (Dar es Salaam) na Amon Paul (Mara) wakati kocha bora ni Stewart Hall wa Azam aliyewashinda Charles Kilinda (JKT Ruvu) na Charles Mkwasa (Ruvu Shooting). Kila mshindi mepata sh. 3,875,000.
Timu yenye nidhamu bora ni Azam iliyopata sh. 7,750,000, mshindi wa tatu Yanga sh. 15,500,000, makamu bingwa Azam sh. 22,000,000 na bingwa Simba sh. 50,000,000.
Pia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewazawadia sh. 1,000,000 kila mmoja kwa wachezaji watatu vijana wenye umri chini ya miaka 20 waliofanya vizuri kwenye ligi hiyo.
Wachezaji hao ambao walikuwa kwenye vikosi vya kwanza vya timu zao ni Frank Domayo (JKT Ruvu), Rashid Mandawa (Coastal Union) na Hassan Dilunga (Ruvu Shooting).