Mabingwa watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) wataanza kutetea ubingwa wao Julai 14 mwaka huu dhidi ya Atletico ya Burundi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye ametangaza ratiba ya michuano hiyo leo (Juni 29 mwaka huu) katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Timu 11 zitashiriki katika michuano hiyo itakayoanza Julai 14 hadi 28 mwaka huu ambapo kwa siku zitachezwa mechi mbili (saa 8 mchana na saa 10 jioni) huku Tanzania Bara ikiwakilishwa na Yanga, Simba na Azam. Mechi ya kwanza siku ya ufunguzi (saa 8 mchana) itakuwa kati ya APR ya Rwanda na Wau Salaam ya Sudan Kusini. Kundi A lina timu za Simba, URA ya Uganda, Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Ports ya Djibouti. Azam, Mafunzo ya Zanzibar na Tusker ya Kenya ziko kundi B. ...