Mabingwa watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) wataanza kutetea ubingwa wao Julai 14 mwaka huu dhidi ya Atletico ya Burundi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye ametangaza ratiba ya michuano hiyo leo (Juni 29 mwaka huu) katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Timu 11 zitashiriki katika michuano hiyo itakayoanza Julai 14 hadi 28 mwaka huu ambapo kwa siku zitachezwa mechi mbili (saa 8 mchana na saa 10 jioni) huku Tanzania Bara ikiwakilishwa na Yanga, Simba na Azam. Mechi ya kwanza siku ya ufunguzi (saa 8 mchana) itakuwa kati ya APR ya Rwanda na Wau Salaam ya Sudan Kusini.
Kundi A lina timu za Simba, URA ya Uganda, Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Ports ya Djibouti. Azam, Mafunzo ya Zanzibar na Tusker ya Kenya ziko kundi B.
Yanga inaunda kundi C lenye timu za APR ya Rwanda, Wau Salaam ya Sudan Kusini na Atletico ya Burundi.
Timu nane zitaingia robo fainali itakayochezwa Julai 23 na 24 mwaka huu. Kundi A na C kila moja litatoa timu tatu kwenda robo fainali wakati B litatoa timu mbili.
El Merreikh ya Sudan, Red Sea ya Eritrea, Coffee ya Ethiopia na Elman ya Somalia hazitashiriki katika mashindano ya mwaka huu ambayo yanafanyika Tanzania Bara kwa mwaka wa tatu mfululizo kutokana na sababu mbalimbali.
Coffee haitashiriki kwa vile ligi ya Ethiopia inaanza Julai 14 mwaka huu wakati El Merreikh wikiend ya Julai 13-15 mwaka huu itakuwa na mechi ya michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Bingwa wa michuano hiyo atapata dola 30,000, makamu bingwa dola 20,000 na mshindi wa tatu dola 10,000. Michuano hiyo itaoneshwa moja kwa moja (live) na Televisheni ya