Mbunge Jimbo la Ubungo Chadema, John Mnyika:Hatua kuhusu matumizi ya dola milioni 164.6 za “mabomba ya mchina” na mikataba ya miradi ya sasa ya maji jijini Dar es salaam
Mbunge wa Jimbo la Ubungo-Chadema na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini,John Mnyika
---
---
Tarehe
3 Januari 2013 kwa kutumia kifungu cha 10 cha sheria ya haki, kinga na madaraka
ya Bunge nimetaka Wizara ya Maji inipatie nakala ya ripoti ya utekelezaji wa
mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar
es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and
Sanitation Project-DWSSP) uliotekelezwa kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 jijini
Dar es salaam.
Nimetaka
ripoti hiyo ili kubaini matumizi ya dola milioni 164.6 zinazoelezwa kutumika
katika mradi huo maarufu kama wa ‘mabomba ya mchina’ kwa kuwa mpaka sasa mwaka
2013 sehemu kubwa ya mabomba yaliyowekwa wakati wa mradi huo katika Jiji la Dar
es salaam hayatoi maji huku kukiwa na upungufu katika uzalishaji, upotevu
wakati wa usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma za ufisadi katika
matumizi.
Pamoja
na kutaka ripoti ya utekelezaji wa mradi huo, nimetaka pia nakala ya ripoti ya
ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys
kuhusu mradi huo.
Nimetaka
pia kupatiwa ripoti za ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) kwa Kampuni
ya Maji Dar es salaam- DAWASCO (Dar es salaam Water Supply and Sewerage
Company) na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka-DAWASA (Dar es Salaam Water
Supply and Sewerage Authority) kwa mwaka miaka mitatu ya 2009/10, 2010/2011,
2011/2012 ili kuweza kufuatilia hatua zinazostahili kuchukuliwa.
Aidha
kwa kutumia kifungu hicho hicho cha 10 cha sheria ya haki, kinga na madaraka ya
Bunge, katika barua yangu kwa katibu wa
Bunge niliyoiwasilisha leo tarehe 3 Januari 2013 nimetaka kupatiwa nakala za
mikataba yote ya miradi inayotekelezwa hivi sasa ya maji katika Jiji la Dar es
Salaam ili kuendelea kufanya kazi ya kibunge ya kuishauri na kuisimamia
serikali kueupusha kasoro zilizojitokeza katika miradi ya miaka iliyopita
kujirudia hivi sasa.
Kati
ya mikataba niliyotaka kupatiwa ni ile ya miradi ya miundombinu inayoendelea
kujengwa na mikopo iliyopatikana kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu huyo ikiwa
ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango
Maalum wa Maji Dar es salaam 2011-2013 ambao uliwasilishwa katika Baraza la
Mawaziri mwezi Machi 2011 na kuridhiwa kutekelezwa ukihitaji jumla ya shilingi
bilioni 653.85; ambao utekelezaji wake unasuasua.
Izingatiwe
kwamba Jiji la Dar es salaam lina adha ya maji ya muda mrefu ambayo kila mkazi
wa jiji hili ana wajibu wa kuhakikisha inapatiwa ufumbuzi hivyo mwaka 2013
utumike kuongeza msukumo wa uwajibikaji katika sekta ya maji ambayo ni muhimu
kwa uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.
Pamoja
na kuwa matokeo ya sensa ya mwaka 2012 kiwilaya na kimikoa bado hayajatangazwa,
Jiji la Dar es salaam linakadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya milioni nne; hivyo
ni sawa na takribani asilimia kumi ya watanzania wote milioni 44.9
waliotangazwa.
Upatikanaji
wa maji katika Jiji la Dar es salaam miaka michache baada mwaka 1961 ulikuwa
zaidi ya asilimia 68; hivi sasa miaka 51 baada ya uhuru tumerudi nyuma na
upatikanaji ni kwa wastani asilimia 55 tu tena kwa mgawo.
Pamoja na kero ya mgawo wa
maji hali hii imesababisha ongezeko kubwa la bei ya maji kwa wananchi wa kipato
cha chini wanaotegemea kupata maji kutoka sekta binafsi ambapo wanaonunua maji
kwa madumu hununua bei ambayo ni takribani mara 15 ya bei ya mteja anayepata
huduma ya maji ya bomba.
Hali
ni mbaya zaidi kuhusu uondoaji wa maji taka ambapo ni chini ya asilimia 10 tu
ya makazi ndiyo yaliyounganishwa katika mtandao wa maji taka na hivyo kuleta
uchafuzi wa mazingira hususani katika maeneo yasiyopimwa. Hata katika maeneo
yaliyopimwa Jijini Dar es salaam mitandao ya maji taka haijakarabatiwa na
kupanuliwa kwa wakati kwa kuzingatia ongezeko la watu suala ambalo
lisipochuliwa kwa uzito unaostahili madhara yatatokea katika siku za usoni.
Hatua
za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na uondoaji wa maji taka
zinapaswa kuchukuliwa kuhusu hali hii kwa kuzingatia kuwa idadi ya watu katika
Jiji la Dar es salaam inaendelea kukua kwa kasi likiwa ni jiji la tatu kwa
ongezeko kubwa la watu barani Afrika na la tisa duniani.
Kwa
nyakati mbalimbali katika kipindi cha kati ya mwaka 2000 mpaka 2010 Serikali
imekuwa ikitoa ahadi za kumaliza tatizo la majisafi na majitaka katika Jiji la
Dar es Salaam bila utekelezaji sahihi, kamili na wa haraka; hivyo uamuzi wa
kutumia sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge na kazi zingine za kibunge
nitakazozifanya mwaka huu wa 2013 zitaongeza uwajibikaji katika sekta ya maji
kwa manufaa ya wananchi na nchi kwa ujumla.
Imetolewa
mtandaoni tarehe 4 Januari 2013 na:
John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo