Wazalishaji Wa Chumvi Bagamoyo Walalamikia Kupanda Kwa Ushuru
by David Mathias
WAZALISHAJI
wa Chumvi katika Wilaya ya Bagamoyo wamelalamikia ongezeko la ushuru wa
chumvi unaodaiwa kupanda kwa asilimia 50 zaidi ya kiwango kilichokuwa
kikitozwa hali inayowasababishia kuongezeka kwa gharama za uzalishaji kuliko bei halisi ya masoko.
Malalamiko hayo yametolewa
mwishoni mwa wiki na Katibu wa Chama cha Wazalishaji Chumvi Tanzania
(TASPA), Julius Mosha wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari mjini hapa kuhusiana na malalamiko yanayotolewa mara kwa mara na
wadau wa sekta ya chumvi.
Mosha alisema kuwa mwaka 2008
Halmashauri hiyo ilipitisha sheria ndogo ya ongezeko la ushuru wa chumvi
toka kutoka Sh.50 kwa mfuko wa kilo 50 sawa na Sh,1000 kwa tani,
ikafikia Sh.200 kwa mfuko wa kilo 50 sawa na Sh.4000 kwa tani, hata
hivyo ongezeko hilo lililalamikiwa sana na kudai kuwa inashangaza licha
ya kuwa na malalamiko hayo kuna taarifa nyingine ya ongezeko la asilimia
50 zaidi.
Alisema licha ya kuwa na
malalamiko hayo, Halmashauri hiyo imekuwa na tabia ya kufanya maamuzi ya
kuongeza ushuru wa aina mbalimbali bila ya kushirikisha wadau kwa
mujibu wa sheria hali inayosababisha kuongezeka kwa gharama ya
uzalishaji kulinganisha na bei ya chumvi katika masoko.
Mmoja wa wadau ambaye pia ni
mshindi wa Tuzo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA ) kwa mwaka 2012
anayeongoza kwa kulipa Kodi ya Mapato katika Wilaya ya Bagamoyo Kampuni
ya H.J.Stanley and Sons Ltd imelalamikia Wilaya hiyo kutoza ushuru
mwingi katika sekta ya chumvi ikiwa ni pamoja na kuwa na urasimu katika
baadhi ya mambo yanayohusu uwekezaji.
Imeelezwa kuwa licha ya wao kuwa
na uzalendo wa kupenda kulipa kodi ya mapato kama sheria inavyowataka
kufanya hivyo , lakini wamejikuta wakipambana na ushuru wa Wilaya ambao
kimsingi ni mkubwa hali inayowatia wasiwasi katika kuendesha shughuli
zao za chumvi.
Kauli hiyo ilitolewa na Msemaji
wa Kampuni hiyo Richard Stanley wakati alipokuwa akizungumzia kuongeza
kwa ushuru wa chumvi pamoja na changamoto anazokabiliana nazo katika
sekta hiyo.
Aliongeza kuwa ushuru unaotozwa
na Halmashauri ya Bagamoyo unapingana na sheria inayowataka wao walipie
asilimia 0.3 tu ya faida wanayopata kutokana na uzalishaji wao, lakini
wanatozwa karibu asilimia 6 ambapo kwa kila mfuko wa chumvi unaozalishwa
katika Wilaya ya Bagamoyo anapaswa kulipia Sh.200.
Sambamba na hayo mwekezaji huyo
amelalamikia baadhi ya tabia inayoashiria urasimu kwa baadhi ya
watendaji pindi wanapofuatilia nyaraka mbalimbali za ardhi, kwani
wamekuwa wakipigwa danadana mara kwa mara huku wakidai nyaraka
hazionekani katika Idara ya ardhi licha ya wao kuzipeleka mara nyingi
tangu mwaka 2010.
Aidha aliiomba Serikali
kuingilia swala hili na kuangalia ni jinsi gani wanaweza kusaidia
kupunguza ushuru unaotozwa na Halmashauri ya Bagamoyo kwa wazalishaji wa
chumvi, ikiwa ni pamoja na kupunguza urasimu usio wa lazima pindi watu
wanapofuatilia haki zao.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Samuel Saliyanga alisema Hamashauri
yake inatekeleza sheria ndogo za Halamshauri na zilizopitishwa na Waziri
Mkuu na si vinginevyo na kwamba tayari imeshapitishwa sheria nyingine
ya kuongeza ushuru huo kwa watu wa chumvi.
Saliyanga alisema tayari Waziri
Mkuu ameshapitisha sheria ndogo katika Halmashauri yake kuanzia Novemba 8
mwaka 2012 na itatumika kuwatoza ushuru wa chumvi kwa kila mfuko wa
kilo 50 sh.300 badala ya Sh.200 iliyokuwa ikitozwa awali kwa kila mfuko
wa chumvi wa kilo 50 na kwamba ushuru huo si wa uzalishaji.