ZITTO AIBUKA NA JIPYA
MWENYEKITI
wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na Mbunge wa Jimbo la
Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe (CHADEMA), jana aligeuka mbogo na
kuwafukuza watendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Nchini
(Tawiri) baada ya kubaini kupotea kwa silaha ambazo hadi sasa
hazijulikani ziliko.
Zitto
akiungwa mkono na wajumbe wa kamati hiyo, alisema kamati hiyo imepata
hofu kubwa juu ya kutoweka kwa bunduki hizo, na zaidi baada ya
kubainika kuwa moja ya silaha zinazoaminika kumilikiwa na taasisi hiyo
kuhusishwa na tukio la mauaji mjini Mugumu, mkoani Mara.
Mbali
na kuwafukuza watendaji wa taasisi hiyo, aliwaagiza kuwasilisha haraka
ndani ya wiki mbili, ripoti kamili itakayoeleza kinagaubaga namna
silaha hizo aina ya bunduki zilivyotoweka katika mazingira ya
kutatanisha tangu mwaka 1980.
Zitto
alisema kuwa suala la upotevu wa silaha hizo, na nyingine kuhusika
katika matukio ya kihalifu ni nyeti, na hivyo kamati hiyo ya Bunge
inahitaji maelezo ya kina kutoka kwa watendaji hao, hivyo akawatimua, na
kuwaagiza wawasilishe kwake ripoti ya kina mjini Dodoma wakati wa
mkutano wa bajeti unaotazamiwa kuanza Juni 12, mwaka huu.
“Sisi
kama kamati tumeamua kutoendelea kuijadili taarifa hii kutokana na
kuwa na hofu na suala hilo kwani hivi sasa kuna taarifa ya silaha yenu
namba 00980 ambayo inashikiliwa katika kituo cha polisi Mugumu tangu
mwaka 1999 baada ya kudaiwa kutumika kwenye mauaji,” alisema Zitto.
Mwenyekiti
huyo alishangazwa na kitendo kilichoonyeshwa na taasisi hiyo cha
kushindwa kufuatilia zilipo silaha hizo jambo ambalo linatoa taswira
kuwa zinaweza kuwa zinatumika katika uhalifu unaojitokeza nchini.
Alisema
silaha hizo zinazomilikiwa na tawi la utafiti la Kingupira lililoko
mbuga za wanyama za Serous ziligundulika kutokuwepo katika kituo hicho
baada ya kufanyika kwa ukaguzi wa mwaka 2008 na 2009.
Zitto
alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida na inayotia mashaka,
watendaji wa taasisi hiyo hadi sasa hawajatoa taarifa polisi kuhusu
kutoonekana silaha hizo kwa kipindi chote hicho.
“Ninachofahamu
ni kuwa kama silaha yako haionekani kitu cha kwanza ni lazima utaarifu
vyombo vya dola …lakini ninyi wenzetu mmenyamaza kimya wala hamjawa na
hofu na suala hilo,” alisema.
Mbunge
wa Mwibara, Kangi Lugora (CCM), alitaka kujua kwa nini baada ya
mkaguzi kugundua suala hilo limechukua muda mrefu bila kushughulikiwa.
“Hivi
mnafahamu unyeti wa suala hili? Mnajua kwa sasa nchi yetu iko katika
wakati gani katika suala la uhalifu? Sio katika maeneo ya mijini tu bali
hadi katika hifadhi zetu wanyama wengi wanauliwa hovyo. Inawezekana
silaha hizo ndizo zinatumika,” alisema Lugora.