Zaidi ya watu 50 wafariki dunia kwenye ajali ya boti nchini Malawi
Habari
kutoka Malawi zinasema kuwa zaidi ya watu 50 wamefariki dunia kwenye
ajali ya boti iliyotokea katika ziwa Malawi. Maafisa wa polisi wa nchi
hiyo wamesema kuwa boti hiyo ilikuwa na wahajiri haramu kutoka Somalia
na Ethiopia ambao lengo lao lilikuwa ni kufika Malawi na kisha kuingia
kinyemela Afrika Kusini. Baadhi ya duru zinaarifu kuwa Watanzania kadhaa
pia ni miongoni mwa waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo. Imedaiwa
kwamba boti hiyo ilizama siku ya Jumanne na miili kuanza kuelea siku
iliyofuatia. Maafisa wa usalama wamesema kuwa tayari miili 47 imeopolewa
na kuzikwa kwenye kaburi la pamoja. Ripoti ya hivi majuzi ya shirika la
kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch imesema visa vya magendo
ya binadamu barani Afrika vimezidi mno katika miezi minne ya kwanza ya
mwaka huu wa 2012 ikilinganishwa na miezi minne ya kwanza ya mwaka
uliopita.