WAZIRI WA FEDHA WILLIAM MGIMWA

BAJETI ya Serikali ya mwaka 2012/2013 inatarajiwa kutumia Sh15 trilioni katika vipaumbele saba ikilinganishwa na Sh13.5 trilioni zilizotengwa mwaka 2011/12.Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa aliileza Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi kuwa matumizi ya kawaida ya Serikali yanatarajiwa kuwa Sh10 trilioni na fedha za maendeleo ni Sh5 trilioni.Dk Mgimwa alimweleza mwandishi wetu kuwa kipaumbele cha kwanza katika Bajeti yake ya kwanza tangu kuteuliwa hiyo ni miundombinu.
Kwa mujibu wa waziri huyo, miundombinu imegawanyika katika makundi manne ya reli, umeme, maji salama, usafirishaji na uchukuzi ambavyo vimetengewa jumla ya Sh4.5 trilioni.
Vipaumbele vingine vya Serikali ni kilimo, viwanda, rasilimali watu, huduma za jamii, utalii, biashara ya ndani na nje na huduma za fedha.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kuwa katika bajeti hiyo, fedha zilizopelekwa Wizara ya Uchukuzi kwa ajili miradi ya maendeleo ni Sh252 bilioni huku sekta ya usafiri wa reli ikitarajiwa kutumia Sh130 bilioni.
Katika Bajeti hiyo ya maendeleo, Wizara ya Ujenzi imetengewa Sh693 bilioni, wakati sekta ya nishati ikiwa nayo imepewa umuhimu na mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka mikoa ya kusini umetengewa Sh325 bilioni.
Mwelekeo huo wa bajeti unaonyesha pia kwamba, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetengewa jumla ya Sh364 bilioni.

Kuuza mashangingi
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, zilisema katika mkakati wa kubana matumizi, Serikali itapunguza matumizi ya magari ya kifahari kwa kiwango kikubwa.
Katika hatua hiyo, inatarajiwa pia kupiga mnada baadhi ya magari hayo yanayotumiwa na mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na wakurugenzi na kununua magari madogo yenye gharama nafuu.
Hata hivyo, chanzo chetu kilisema waziri huyo hakufafanua suala hilo akisema atalizungumza zaidi wakati wa kuwasilisha Bajeti hiyo Mjini Dodoma.
Takwimu za Serikali za mwaka juzi, zilionyesha kuwa Serikali Kuu hadi na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ilikuwa ikimiliki magari 40,000, kati yake 11,000 yakiwa ya kifahari.Tayari Wizara ya Ujenzi kupitia timu ya wataalamu mwaka Aprili, 2007 ilitoa ripoti ya namna bora ya kupanga matumizi ya magari ya Serikali kwa kuangalia kila daraja la kiongozi, lakini ripoti hiyo iliishia mezani kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.

Zitto aomba ushauri
Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe amesema Bajeti yake mbadala kwa mwaka fedha 2012/13 itajikita katika kuongeza mapato ya ndani, kupunguza misamaha ya kodi na matumizi ya Serikali yasiyokuwa ya lazima.
Katika kuboresha bajeti hiyo, Zitto kupitia vyombo vya habari na mitandao mbalimbali amewaomba wadau wamshauri jinsi ya kuiboresha ili ikidhi mahitaji ya Watanzania.
 “Naomba kila mtu atakayeweza, atoe mchango wake wa juu ya nini kinatakiwa kipewe kipaumbele zaidi katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, maoni yenu yatajumuishwa katika kuboresha bajeti ya upinzani ili kuishawishi Serikali kuifuata,” alisema Zitto.
Alisema baadhi ya maeneo yatakayotazamwa kwa umakini katika bajeti hiyo ni pamoja na pamoja na mfumuko wa bei na ukosefu wa ajira.
Eneo jingine ambalo Zitto atalipa kipaumbele ni jinsi ya kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje na kuangalia namna ya kuongeza mauzo ya bidhaa ya nchi.
Akitolea mfano wa takwimu zinazoishia Machi mwaka huu, alisema Tanzania iliagiza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani 12 bilioni na kuuza nje zenye thamani ya dola 6.9 bilioni.Zitto atalenga katika kupunguza deni la taifa ambalo kwa sasa limefikia Sh22 trilioni kutoka Sh7 trilioni mwaka 2009 na Sh11 trilioni mwaka 2010.
Wabunge kuwabana mawaziri

Baadhi ya wabunge wa CCM wanatarajia kuibana Serikali katika Bunge lijalo wakidai kuwa imeshindwa kutekeleza kwa ukamilifu Bajeti ya mwaka jana pamoja na kuwawajibisha baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi.
Katika mkutano uliopita, wabunge waliibana Serikali wakitaka mawaziri wanane, manaibu waziri wawili na watumishi wengine wa umma waliotajwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), wawajibishwe. Lakini wabunge hao wamesema Rais Jakaya Kikwete aliwafuta kazi mawaziri sita na kuwahamisha wizara wawili na kuwang’oa manaibu waziri wawili miongoni mwa waliotajwa na hawajaona juhudi za kuwawajibisha watuhumiwa wengine.
Mawaziri waliofutwa kazi ni William Ngeleja (Nishati na Madini), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Omari Nundu (Uchukuzi), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara) na Mustafa Mkulo (Fedha).
Waliohamishwa wizara ni Profesa Jumanne Maghembe (Kilimo) kwenda Maji na George Mkuchika (Tamisemi) kwenda Ofisi ya Rais, Utawala Bora. Manaibu Waziri waliotemwa ni Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Athumani Mfutakamba (Miundombinu).
Tayari Maige amekaririwa wiki hii akiwa katika ziara ya kutembelea jimbo la Msalala, mkoani Shinyanga, akiweka wazi kuwa atawasha moto atakapoingia bungeni akiwa mbunge wa kawaida wiki ijayo, kwani uwaziri wake ulikuwa unamzuia kuibana Serikali.
Filikunjombe anena
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Deo Filikunjombe, alisema juzi kuwa tatizo kubwa la Serikali ni kuchelewa kuchukua hatua hata inapoonekana dhahiri kuwa kuna tatizo.
Kuhusu Bajeti alisema kitendo cha Serikali kuahidi kutoa fedha kwa wizara fulani na kutofanya hivyo ni moja ya matatizo makubwa yanayosumbua kwa sasa na atalikemea kwa nguvu zote. “Hatuwatendei haki wananchi kwa kukaa bungeni miezi mitatu na matunda yasionekane. Ukisema sehemu fulani fedha zinahitajika, Serikali inasema itazitoa, lakini mwisho wa siku hazionekani, hii siyo haki,” alisema Filikunjombe.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Augustine Mrema, alisema licha ya Rais Jakaya Kikwete kujitahidi kusafisha wizara, bado kuna watendaji wabovu katika halmashauri ambao wanazidi kumwangusha.
“Baada ya kelele za wabunge katika kikao kilichopita na Rais kuwawajibisha mawaziri, isingetarajiwa halmashauri kama za Mafia na Rufiji kutuletea uchafu na hesabu ambazo hazijahakikiwa na hazieleweki,” alisema Mrema na kuongeza:
“Sisi tunazidi kumwambia Rais na Waziri Mkuu kwamba, bado kuna halmashauri sugu, hazitaki kabisa kujirekebisha, kuna wakuu wa wilaya na wakurugenzi ambao bado wanawaangusha, wanafanya madudu huko.”
Kwa upande wake, Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Lugola alisema atakufa na Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii akidai kuwa waziri aliyetangulia amewafanyia madudu Watanzania. Mbunge huyo alieleza sababu za kutounga mkono bajeti hiyo.
“Pale bungeni walionyesha Bajaji nzuri ambazo tulizikubali, lakini walinunua Bodaboda ambazo kipindi cha mvua mgonjwa haendi…” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya alisema hakuna mtu wa kumfunga mdomo kwa kuwa anatetea maslahi ya Watanzania: “Siku zote mimi nasema asiyefanya kazi asile… kwa mazuri, lazima tuiunge mkono serikali, lakini kwa uzembe hakuna kulala mpaka kieleweke,’’ alisema Bulaya.
Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli alisema: “Nataka uwajibikaji siyo mambo ya propaganda. Huu ni wakati wa kuwajibika na atakayefanya hivyo ni rafiki yangu, lakini wazembe tutabanana nao ukumbini kuanzia wiki ijayo.’’

Popular posts from this blog

MAMBO 6 YA KUZINGATIA KATIKA MAHUSIANO

Mwanajeshi Aliyepiga Picha na Mbunge wa Arusha Mjini-Chadema Godbless Lema Kwenye Mkutano wa Hadhara Akamatwa

MATAJIRI WATANO WANAOONGOZA TANZANIA