WASANII WA FILAMU KUNUFAIKA NA KAZI ZAO
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Dkt. Fenella Mukangara akiongea na baadhi ya Viongozi wa mashirikisho
ya wasanii wa filamu na Muziki kuhusu urasimishaji wa kazi za wasanii
wa Filamu na Mziki jijini Dar es Salaam (jana). (Picha na Benjamin Sawe
wa WHVUM)
Na
Concilia Niyibitanga- WHVUM
Serikali imeamua kuweka
mfumo rasmi utakaowawezesha Wasanii wa Filamu na Muziki nchini kunufaika na kazi wanazozibuni na
kuzitengeneza.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara wakati akiongea na Viongozi
wa Mashirikisho ya Wasanii wa Filamu na Muziki.
Dkt. Mukangara amesema
kuwa Serikali imesikia kilio cha Wasanii kwa kuirasimisha Sekta ya Filamu na Muziki
ili kuondokana na kilio cha muda mrefu cha Wasanii kutonufaika na jasho lao.
Amesema kuwa Serikali
itatumia mfumo wa kuziwekea kazi hizo stampu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
ambazo zitakuwa na usalama kwa nia ya kuondokana na uzalisha na udurufishaji
ovyo wa kazi hizo na kazi hizo zitawekewa ‘bar code’ kwa wepesi wa ufuatiliaji.
Urasimisaji huu unaotarajia
kuanza rasmi Januari, 2013 utawezesha wasanii kukopesheka ili kupata mitaji
itakayowawezesha kutengeneza kazi bora na zenye viwango na zitakazoweza kuingia katika soko la ushindani. Ameeleza
Dkt. Mukangara.
Amesema kuwa kwa sasa
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo; Wizara ya Fedha; na Wizara ya
Viwanda na Biashara zinaweka katika mfumo wa kielektroniki taratibu
zinazowezesha utekelezaji wa mfumo huu kuwa rahisi.
Aidha, Dkt. Mukangara
ametoa wito kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake katika kuhakikisha kero ya Wasanii kuibiwa na kutofaidika na
kazi zao inaondoka na kuwataka vijana kujipanga vizuri ili kuitumia fursa hii
na hata katika siku za usoni waweze kuwa na
Saccos za vijana katika tasnia ya filamu na muziki na waweze kukopesheka
kupitia Mfuko wa Vijana.
Kwa upande wake Rais wa
Shirikisho la Sanaa za Ufundi, Bw. Adrian Nyangamalle ameipongeza Serikali kwa
hatua ya kuirasimisha Sekta ya Filamu na Muziki na kuiomba Serikali kuangalia
uwezekano pia wa kurasimisha Sanaa za Ufundi ambazo zinaonekana
kusahaulika katika mfumo huo.
Bw. Nyangamalle amesema
kuwa katika Wasanii milioni 9 nchini, takribani Wasanii milioni 4 ni Wasanii wa
Ufundi, hivyo ni changamoto kwa Serikali hususan Wizara yenye dhamana na Sekta
hiyo kuona umuhimu wa kurasimisha kazi za Sanaa za Ufundi.