WANAWAKE WANAWEZA KUIPONYA NCHI YETU
MKE wa Waziri
Mkuu, Mama Tunu Pinda amesema wanawake wa Tanzania wanayo nafasi nzuri ya
kuungana na kumuomba Mungu ili aiponye nchi hii na majanga mbalimbali.

“Tutumie
nafasi yetu kama wanawake, kuunda jeshi kubwa la maombezi kwa ajili ya nchi
yetu. Nchi hii inahitaji maombi, na kwa hakika inamuhitaji Mungu iwe ni kwenye huduma zetu, ndoa zetu, familia zetu na
uchumi wetu binafsi na wa Taifa kwa jumla,” alisema.
Ametoa kauli
hiyo jana jioni (Jumamosi, Juni 9, 2012) wakati akifunga Kongamano la Kitaifa
la Wanawake Waombolezao lililodumu kwa siku tatu katika ukumbi wa Sinza
Christian Centre jijini Dar es Salaam.
Kongamano
hilo ambalo liliwajumuisha wanawake 70 kutoka mikoa 31 ya Tanzania Bara na
Visiwani na wageni 32 kutoka nchi za Zambia, Zimbabwe, Afrika ya Kusini, Malawi,
Uganda, Kenya, na Marekani, lilifunguliwa Juni 7, 2012 na Mke wa Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar, Bibi Asha Seif Iddi.
“Ninapenda kuwasihi
wanawake wote tusichoke kumuomba Mwenyezi Mungu naye atatupa yale tumwombayo.
Tusimame kwenye sala na maombi, naye atatusaidia,” alisisitiza.
Alitumia
fursa hiyo pia kuwaomba akinamama hao wajumuike kuwaombea Waheshimiwa Wabunge
ambao ni wawakilishi wa wananchi zaidi ya milioni 45 kwani wanatarajia kuanza
kikao cha Bunge Jumanne ijayo.
“Tumuombe Mungu awaguse Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge
ili wabaini kwamba wana jukumu la kuhakikisha wanafanya maamuzi ambayo yatawasaidia
Watanzania kujikwamua kutoka kwenye umaskini na hatimaye waweze kupata maisha
bora,” alisema.
“Sote tunaamini kwamba maombi yaliyofanyika hapa kwa
ajili ya viongozi wetu hayataenda bure bali yataleta mabadiliko ndani ya mioyo
yao ili wapate ujasiri wa kukataa maovu na kutambua kwamba uongozi walionao ni
dhamana waliyopewa na Mungu hivyo wanapaswa kutumia vyema dhamana hiyo kwa
ustawi wa Taifa letu.
Alitumia fursa hiyo kuwaomba akinamama hao wawaombee
Watanzania wote wawe na uzalendo wa kuipenda na kuithamini nchi yao wenyewe,
wawe na moyo wa kufanya kazi kwa bidiii na siku zote wawe tayari kuitakia mema
nchi hii.
Mapema, akitoa mada kuhusu ukomavu wa kiroho, Mwalimu
Nikku Kyungu kutoka Marekani alisema wanawake wa Tanzania wanayo nafasi ya
kubadilisha mambo kama tu watampa Mungu nafasi ya kutenda na kuacha kuomba kwa
mazoea.
Mwalimu Kyungu ambaye ni Mtanzania aishiye Marekani
ambaye aliokoka tangu akiwa na miaka saba, alisema ana mzigo mkubwa wa
kuliombea Bara la Afrika ili watu wake wafunguke na waweze kufaidi rasilmali
walizonazo katika nchi zao.
Naye Mchungaji Grace Kapswara kutoka Zimbabwe aliwataka
akinamama hao wawaheshimu watumishi wa Mungu na wajitoe katika kuwasaidia kama
kweli wanataka kufanikiwa maishani mwao.
Aliwasisitizia
akinamama hao haja ya kuomba kwa pamoja kama timu na kuwaeleza kwamba wakati
wao wa kuburudika na kupumzika umekwishawadia.
Kongamano
hilo la siku tatu liliandaliwa na kanisa la Tanzania Fellowship of Churches chini
ya uongozi wa Askofu Godfrey E. Malassy ambaye ni Mwenyekiti wa Mkesha Mkubwa
wa Kitaifa.