VODACOM YATOA POLE
MAREHEMU WILLY EDWARD
Yasema ni pigo kubwa kwa wadau wa habari
·
Yawataka wanahabari kumuenzi
Kampuni ya simu ya
mawasiliano ya Vodacom Tanzania imepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya
kifo cha ghafla cha mwanahabari mahiri Bw. Willy Ogunde Edward kilichotokea
usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii.
“Tunatoa mkono wa pole kwa familia ya marehemu,
waajiri wake na kipekee familia ya wanahabari nchini kwa kuondokewa na
mpiganaji na kamanda wetu aliyekuwa sehemu muhimu ya ujenzi wa tasnia ya habari
nchini.”Alisema Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania Bw. Rene Meza
Marehemu Willy Edward alikuwa ni mdau wa habari
mwenye msaada na ushauri pale anapohitajika na aliiwakilisha vyema tasnia hii
ya habari tangu alipokuwa Majira mpaka kabla umauti haujamkuta akiwa Mhariri wa
habari wa Jambo Leo.
Marehemuatakumbukwa kwa jinsi ambavyo alikua mahiri
katika kazi yake, ndani na nje ya mipaka ya Tanzania na kwamba mchango wake
utaendelea kuwa chachu hasa kwa vizazi vijavyo vya wanahabari chipukizi nchini.
“Tutamkumbuka sana Marehemu Willy ambae alikuwa ni
mpole na mcheshi na mwenye utashi wa mafanikio katika kazi zake. Hakusita kutoa
ushauri kuboresha uandishi wa habari ili kutoa ujumbe uliokamilika na sahihi
pale alipoona mapungufu kutika habari husika”. Alisema Meza.
Mkurugenzi huyo Mkuu wa Vodacom amesema kampuni yake
daima ina thamini na kuheshimu mchango wa wanahabari katika maendeleo ya taifa
na uimarishaji ustawi wa jamii na kuamini kuwa wanahabari waliobaki
wataendeleza urithi (Legacy) aliouacha marehemu Willy.
Mungu azilaze roho za Marehemu BwWilly Ogunde Edward
mahali pema peponi –Amen.