VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUTUNZA AMANI
Viongozi
wa dini za Kikristo na Kiislam wametakiwa kutumia vema nyadhifa na fursa
walizonazo katika kuhakikisha kuwa waamini wao wanatii sheria bila ya
kushurutishwa.
Wito
huo umetolewa na Rais Mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ally Hassan Mwinyi wakati
alipokuwa akizindua kampeni ya utii wa Sheria Bila Shuruti kwa viongozi wa dini
za Kiislam na Kikristo.
Mhe.
Mwinyi amewataka viongozi hao kutumia fursa wanazozipata kupitia Ibada na Swala
katika kuwahubiria waamini wao kuhusiana na suala zima la kutii Sheria bila ya
kushurutishwa.
Amesema
kuwa kwa kuwa viongozi hao wa dini ndio watu pekee ambao wanakuwa na watu wote
katika nyakati zote za maisha yao bila kujali
itikadi wala kabila, hivyo ni rahisi kwao kuwashawishi waumini hao watii sheria
bila ya kushurutishwa kutokana na imani waliyonayo juu yao.
Aliongeza
kuwa endapo kila kiongozi atafanikiwa kuwashawishi waamini wake watii sheria
bila ya kushurutishwa, nao wakatii , basi ni wazi kuwa uhalifu utapungua nchini
na amani yetu itadumu daima.
Alhaji
Mwinyi pia amewasifu viongozi hao wa dini kwa hatua waliyoichukua ya kuweza
kukaa pamoja bila ya kujali itikadi zao na kufikia muafaka wa kuanzisha kampeni
hiyo ambayo ina lengo la kudumisha amani nchini.
Mhe.
Mwinyi alitoa rai kwa taasisi za Kiserikali, Sekta binafsi pamoja na mtu mmoja
mmoja kuzingatia utii wa sheria bila ya kushurutishwa
kwa kufanya hivyo kutaleta tija kwa taifa.
“Watumishi
wa Umma wakitii sheria bila ya kushurutishwa wananchi watapata huduma kutoka
kwa watumishi hao vizuri na kwa hivyo itaondoa fikra potofu za kwamba watumishi
wa Umma hawatekelezi wajibu wao mpaka kwa kusukumwa”
Aidha
Alhaji Mwinyi amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri anayoifanya
katika kukabiliana na uhalifu nchini ikiwa ni pamoja na busara aliyoitumia
katika kuwashawishi viongozi hao wa dini hata wakafikia kukaa pamoja na
kuanzisha kampeni hiyo.
Akiongea
kwa niaba ya viongozi wenzake, Sheik Issa Othman Issa amewataka watanzania
kupokea mafundisho mema yanayotolewa na viongozi wao wa dini ili kujenga taifa
bora na lenye kutii mamlaka zilizopo.
Sambamba
na uzinduzi huo pia kulizinduliwa vitabu vya ‘Utii wa Sheria ni Wajibu, kufuata
sheria bila shuruti ni thawabu’ kilichoandaliwa na Taasisi ya Kiislamu ya
Mwinyi Baraka na kitabu cha ‘Baraka za utii bila shuruti’ kilichotolewa na
Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania.
Uzinduzi
wa kampeni hiyo iliyokuwa na kauli mbiu ya’ Utii wa Sheria ni Thawabu’ kwa
upande wa Kiislamu na ‘Baraka za Utii wa Sheria’ kwa upande wa Kikristo ulifanyika katika
ukumbi wa Diamond Jubilee na kuhudhuriwa na viongozi wa dini zote mbili kutoka
mikoa mbalimbali nchini.