Ureno nusu fainali Euro 2012
Bao moja la Ronaldo limeiwezesha Ureno kuifunga Czech na kuingia nusu fainali Euro 2012
Mshambulizi Cristiano Ronaldo
aliwaridhisha mashabiki wa Ureno kwa kucheza vizuri sana usiku wa
Alhamisi, na juhudi zake kuiwezesha nchi yake kuishinda Jamhuri ya Czech
bao 1-0 katika mechi ya mwanzo ya robo fainali ya Euro 2012, na
kufanikiwa kuifikisha hadi nusu fainali.
Ronaldo, ambaye alifunga magoli mawili wakati
katika mechi ya awali ya mashindano hayo nchi yako ilipocheza na
Uholanzi, aliweza kugonga mwamba katika nusu ya kwanza na ya pili katika
mechi dhidi ya Jamhuri ya Czech.Hatimaye aliweza kuuelekeza mpira hadi wavuni kwa kichwa, huku zikiwa zimesalia dakika 12 kabla ya mechi kumalizika, na kipa Petr Cech akiweza kuufikia mpira, lakini hakuweza kuuzuia kutokana na nguvu nyingi zilizotumiwa na Ronaldo.
Ilikuwa dhahiri kwamba wachezaji wa Czech waliingia uwanjani wakiwa na nia ya kuimarisha ngome yao, na wala sio kushambulia, na kamwe hawakumtisha kabisa kipa wa Ureno.
Ureno sasa itakutana aidha na Uhispania au Ufaransa katika juhudi za kufuzu kwa fainali.
Bila shaka timu ambayo itakutana na Ureno itakuwa na wasiwasi ni vipi itaweza kumzuia Ronaldo, ambaye baadhi ya wadau wa soka wanasema kwa sasa ndiye mchezaji bora zaidi barani Ulaya.