UFAFANUZI
KATIBU
wa Bunge Dk. Thomas Kashililah ametoa ufafanuzi kuwa mbunge wa Bahi,
Omar Badweli anayetuhumiwa kwa rushwa ataendele kuwa mbunge hata kama
atahukumiwa kifungo cha chini ya miezi sita jela.
Dk.
Kashililah alisema hayo jana alipozungumza kwa njia ya simu na
mwandishi wa gazeti hili kuwa mbunge huyo bado ni mtuhumiwa na pia kwa
mujibu wa katiba atakoma kuwa mbunge kama atahukumiwa kifungo cha
kuanzia miezi sita jela.
Amesema hayo baada ya mbunge huyo Badwel kufunguliwa kesi mahakamani
ya tuhuma ya kuomba rushwa ya sh. milioni nane toka halmashauri ya
wilaya ya Mkuranga, Pwani.
Dk. Kashililah alitoa mfano wa mbunge wa Mbarali, Modestus Kilufi
ambaye hivi karibuni mahakama ilimtia hatiani kwa kosa la kutishia kuua
kwa maneno kwa kukusudia na kumuhukumu kwenda jela miezi 10 au kulipa
faini ya Sh. 500,000.
Hata hivyo Kilufi alilipa faini hiyo na kuachiwa huru na mahakama ya Mbeya.
Alisema
hata kama Badwel atafungwa kifungo cha chini ya miezi sita kwa mujibu
wa katiba ataendelea kuwa mbunge atakapokuwa amemaliza kifungo chake
hicho.
"Kwa sasa Badwel ni mbunge halali kwani hayo aliyonayo ni tuhuma tu na
hatuwezi sisi kama Bunge kumuondoa mpaka ithibitishwe na vyombo
husika.
Ubunge wake utakoma tu endapo atafungwa zaidi ya miezi sita na hii ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kila mtu ana haki mbele ya sheria anaweza akajitetea na akawa huru,
sasa kama umeshamfukuza utafanyaje ni lazima tusubiri," alifafanua Dk.
Kashililah.
Alisema
kumekuwa na kesi nyingi za kupinga matokeo ya uchaguzi katika maeneo
mbalimbali lakini bunge huchukua maamuzi pale mahakama inapomaliza
hukumu yake.
‘’Ni
katiba hiyo hiyo ndiyo inamapa uhuru Badwel kuendelea kuwa mbunge
mpaka hapo atakapohukumiwa na ana haki kama wabunge wengine’’ alisema.