UCHAGUZI WA VIONGOZI YANGA
Kamati ya
Uchaguzi ya TFF inawataarifu wadau na wapenzi wa soka kuwa mchakato wa
uchaguzi wa viongozi wa YANGA kujaza nafasi zilizowazi za Kamati ya
Utendaji unaendelea vizuri chini ya Kamati ya Uchaguzi ya YANGA.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF imepokea kutoka Kamati ya
Uchaguzi ya YANGA nakala za fomu za maombi ya uongozi wa YANGA pamoja
na nakala za vyeti vya elimu vya waombaji uongozi kama sehemu ya taarifa
ya awali ya mchakato wa uchaguzi huo wa YANGA. Kamati ya Uchaguzi ya
TFF imebaini kuwa baadhi ya waombaji uongozi wamewasilisha nakala za
vyeti vya kuhudhuria masomo ya sekondari (Secondary School Leaving Certificate) badala ya nakala za vyeti vya kuhitimu masomo ya elimu ya sekondari (Certificate of Secondary Education).
Kamati ya Uchaguzi ya TFF imekwisha ielekeza Kamati
ya Uchaguzi ya YANGA kuwataka wagombea wote kuzingatia Kanuni za
Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 10(4) na (5) inayowataka wagombea
wote kujaza Fomu Na.1 ya maombi ya uongozi na kuambatanisha nakala ya
cheti cha Elimu ya Sekondari (Certificate of Secondary Education)
kama ilivyoainishwa kwenye Fomu Na.1 kipengere Na.9. Kamati ya Uchaguzi
ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya YANGA iwashauri wagombea ambao
vyeti vyao vimepotea wawasiliane na Baraza la Mitihani la Tanzania
(NECTA) kwa maandishi ili kupata ‘Statement of Examination Results’ itakayotumwa kwa Kamati ya Uchaguzi ya YANGA kupitia TFF kuthibitisha kuwa wamehitimu elimu ya kidato cha nne.
Uhakiki wa vyeti vya elimu ya sekondari vya
waombaji uongozi hufanywa na NECTA na vyuo husika kwa elimu ya juu kwa
chaguzi za wanachama wa TFF. Wanachama wote wa TFF wanatakiwa kuzingatia
kikamilifu matakwa ya Kanuni za Uchaguzi.