TAIFA STARS YAWASILI RASMI MSUMBIJI
Taifa Stars imewasili Maputo saa 5 asubuhi kwa saa hapa tayari kwa
mechi dhidi ya Msumbiji (The Mambas) na kupokewa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Maputo na Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Balozi
Nyandugu.
Stars yenye kikosi cha wachezaji 20 chini ya Kocha Mkuu Kim Poulsen
imefikia Hotel 2010 LDA iliyoko karibu na Uwanja wa Taifa Zimpeto
ambapo mechi hiyo itachezwa Jumapili kuanzia saa 9 kamili kwa saa za
hapa ambapo Tanzania itakuwa saa 10 kamili.
Kwa mujibu wa programu ya Kocha Kim, timu itafanya mazoezi leo na
kesho katika muda ule ule wa mechi ya Jumapili ambayo itachezeshwa na
waamuzi kutoka Madagascar. Mpaka timu inawasili hapa hakuna mchezaji
yeyote mwenye matatizo ambayo yanaweza kusababisha asicheze mechi ya
Jumapili.