SCF YAZINDUA MFUMO WA UTOAJI HABARI ZA MASOKO


Mkurugenzi wa Mradi Mfuko wa Kukuza Ushindani kwa Wazalishaji wa Kati na Wadogo (SCF), Casmir Makoye akitoa maelezo kuhusu matumizi ya mfumo utaoonyesha habari muhimu kuhusu masoko (Point of Sale (POS) datacbase) ambao utaangaza masoko ya Dar es Salaam na Zanzibar uliyozinduliwa jana Jijini Dar es Salaam. Waliokaa ni wawakilishi wa makampuni madogo na ya kati yanayosindika na kuuza vyakula. Picha na mwandishi wetu.
Na Mwandishi Wetu
MFUKO wa Kukuza Ushindani kwa Wazalishaji wa Kati na Wadogo (SCF) umezindua mfumo utaoonyesha habari muhimu kuhusu masoko ambao utaangazia masoko ya Dar es Salaam na Zanzibar.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, mjini Dar es Salaam, jana, Mkurugenzi wa Mradi huo, Casmir Makoye, alisema huduma hiyo inawalenga wajasiriamali wadogo na wa kati ambao husindika na kuuza vyakula.
Makoye alisema uzinduzi huo unatokana na maombi ya wajasiriamali wengi kutaka kufanya utafiti wa masoko ambao umekuwa na gharama kubwa.
Awali, kabla ya uzinduzi wa mfumo huo wajasiriamali waliohudhuria walifundishwa mambo mbalimbali, ambapo wawezesha kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) waliwafundisha jinsi ya kuandaa bidhaa ili ziweze kukubalika kwenye masoko na kisheria.
Mwezeshaji kutoka TFDA, Barnabas Jacob, alisema  zipo sheria na kanuni sita zinazosimamiwa na Mamlaka hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake ambazo mjasiriamali anayejihusisha na uzalishaji wa bidhaa zinazoliwa anapaswa kuzizingatia, na kwamba uhalali wa shughuli yoyote ya aina hiyo unapaswa kufuata utaratibu huo.
Jacob alisema pamoja na kuzingatia vitu hivyo, mjasiriamali anatakiwa kusajili jengo kabla hajapewa leseni ya kufanyia biashara, mambo ambayo yanafanywa na Mamlaka hiyo.
Alisema usajili wa chakula, dawa au vipodozi hutolewa baada ya kukidhi masharti yanayolenga kuhakikisha kuwa vitu vinavyozalishwa ni salama kwa watumiaji na kwamba, ipo maabara inayofanya uchunguzi wa sampuli ili kutambua usalama na uboa wa bidha husika inayotumiwa kurahisisha kutoa uamuzi wa maombi ya wateja wa TFDA.
Kwa upande wake, Ofisa Viwango wa TBS, Mathias Missanga, alisema shirika hilo lipo kwa ajili ya kusimamia na kuthibitisha ubora wa bidhaa za wajasiliamari wa aina mbalimbali, lengo likiwa kutambua ubora kabla hazijamfikia mlaji.
" Maabara ya TFDA inafanya uchunguzi wa sampuli ili kutambua usalama na ubora wa bidhaa husika. Hii husaidia na kurahisisha kutoa maamuzi ya maombi mbalimbali ya wateja katika mamlaka. Sampuli zilizochukuliwa na mkaguzi hupimwa katika maabara za TBS kwa kufuata kiwango husika, " alisema.
Aliwataka wajasiriamali kuchangamkia utaratibu huo wa mfumo wa sheria ili bidhaa watakazozalisha na kupatiwa nembo ya ubora wa shirika hilo ziweze kuuzika katika vizuri katika masoko ya Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi bila kupimwa tena.
"Serikali hutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuhudumia wajasiriamali wadogo na wa kati pale wanapoomba bidhaa zao wanazozizalisha wenyewe zithibitishwe ubora wake. Kati yao wapo ambao wanasamehewa kulipa ada yote kwa sababu ya mitaji yao kuwa midogo, " alisema ofisa huyo.
Akitambulisha mfumo huo wa habari muhimu kuhusu masoko, Makoye alisema utakuwa na utunzaji wa takwimu ambao umefanyiwa utafiti kwenye masoko 13,000 ya kuuzia bidhaa katika jiji la Dar es Salaam na Zanzibar huku ukigusa makundi makubwa ya vyakula.
Makoye alisema manufaa ya huduma hiyo kwa mjasiriliamali ni kumrahisishia msindikaji kuweza kupanga afikie eneo kubwa kiasi gani kulingana na kiwango cha uzalishaji wake, hatua ambayo itamsaidia kupunguza gharama za usafirishaji.
Wakati wa uzinduzi huo, SCF ilionyesha mfumo huo unavyofanya kazi.

Popular posts from this blog

MAMBO 6 YA KUZINGATIA KATIKA MAHUSIANO

Mwanajeshi Aliyepiga Picha na Mbunge wa Arusha Mjini-Chadema Godbless Lema Kwenye Mkutano wa Hadhara Akamatwa

MATAJIRI WATANO WANAOONGOZA TANZANIA