SASA NI ROBO FAINALI
Wachezaji, maafisa na mashabiki wamepata mapumziko mafupi
katika fainali za ubingwa wa Ulaya,Jumatano ,(20.06.2012), lakini
manung'uniko ya Ukraine ambayo ni mwenyeji mwenza wa mashindano haya
yanaendelea.
Ukraine wamejiunga na wenyeji wenza Poland kuwa ni pumba
katika mashindano haya baada ya kushindwa kwa bao 1-0 dhidi ya
Uingereza na gumzo lilituwama katika goli ambalo halikuwa,
ambalo refa aliamua kuwa halikuvuka mstari lililofungwa na
wenyeji hao dhidi ya Uingereza.Haki haikutendeka
Hisia za kutotendewa haki nchini Ukraine hazikuweza kupozwa na Pierluigi Collina, mkuu wa waamuzi katika shirikisho la kandanda barani Ulaya Uefa, kwa kukiri kuwa goli lile lilipaswa kukubaliwa.
Mkuu wa marefa wa Uefa Pierluigi Collina
Ukraine pia bado inaendelea kupambana na maandamano kuhusiana
na kufungwa kwa waziri mkuu wa zamani Yulia Tymoshenko , wakati
serikali ya Uingereza ikisema itasusia pambano la robo fainali
kati ya Uingereza na Italia mjini Kiev siku ya Jumapili kwa
kutomtuma waziri wake huko.Kansela uwanjani
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye ni shabiki mkubwa wa timu ya taifa , hakuhudhuria michezo yote mitatu ya makundi nchini Ukraine lakini atahudhuria mchezo wa robo fainali dhidi ya Ugiriki katika mji wa Gdanski nchini Poland Ijumaa.
Kansela Merkel
Wachezaji na makocha kutoka Ujerumani na Ugiriki wameamua
kutotoa umuhimu wa pekee katika mchezo huo ambao umegeuza hisia
katika mashindano hayo kuelekea katika mzozo wa kiuchumi
unaoathiri mataifa kadha yanayohusika.Vyombo vya habari vya Ugiriki hata hivyo vinashauku ya nafasi hii ya kuirejesha timu ya Ujerumani nyumbani mbele ya kiongozi wa taifa hilo, ambaye hapendwi nchini Ugiriki kutokana na hatua kali za kubana matumizi ambazo ameilazimisha nchi hiyo kuchukua , ili kuweza kupata mkopo wa kimataifa wa kuiokoa kiuchumi.
Refa kutoka Hungary Viktor Kassai na msaidizi wake katika mstari wa goli hawapendwi kabisa na mashabiki wa Ukraine baada ya kutokubali goli lililowekwa wavuni na Marco Devic, ambalo halingeweza kuwaweka wenyeji hao wenza katika robo fainali lakini lingefanya hali kuwa mbaya kwa Uingereza.
Wakati mashindano haya yamebakisha timu nane na taji linaonekana ghafla mbele ya timu hizi baada ya michuano ya kufurahisha ya makundi, mtanange unaanza tena upya leo Alhamis (21.06.2012) wakati robo fainali zitakapoanza mjini Warsaw kati ya Jamhuri ya Czech itakapokwaana na Ureno.
Nani atapeta
Nahodha wa Czech Tomas Rosicky ana matumaini kuwa fiti kwa mchezo huo baada ya kupata maumivu ya misuli.
Ujerumani inamiadi na Ugiriki mjini Gdanski Ijumaa, (22.06.2012), wakati mabingwa watetezi Uhispania inakipiga na Ufaransa mjini Donetsk siku ya Jumamosi na Uingereza itakamilisha ratiba hii ya michuano ya robo fainali siku ya Jumapili kwa kutiana kifuani na Italia mjini Kiev.
Kikosi cha Ugiriki, wazee wa kulinda lango
Wakati huo huo Croatia imekabiliwa na madai ya pili ya
ubaguzi siku ya Jumatano kuhusiana na mabango yaliyowekwa wakati
waliposhindwa kwa bao 1-0 dhidi ya Uhispania na kuyaaga
mashindano haya.Croatia tayari imekwisha pigwa faini ya euro 80,000 baada ya mashabiki kuelekeza matusi ya kibaguzi dhidi ya mshambuliaji wa Italia Mario Balotelli na kufyatua fashifashi katika mpambano wa Croatia katika kundi la pili mjini Poznan. Pia wamepigwa faini ya euro 25,000 kwa matukio kati ya mashabiki katika mchezo wao wa ufunguzi.