RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBI RAMBI
Marehemu Willy Edward (kulia) akiwa na Rais Jakaya Kikwete enzi za uhai wake. |
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Mheshimiwa Fenella Mukangara kuomboleza kifo cha Mhariri
Mtendaji wa Gazeti la JamboLeo, Ndugu Willy Edward Ogunde kilitokea
usiku wa kuamkia jana, Jumapili, Juni 17, 2012 mjini Morogoro.
Katika salamu zake za rambirambi, Mheshimiwa Rais Kikwete amesema kuwa ameshtushwa na kusikitishwa na kifo cha ghafla cha Ndugu Willy Edward Ogunde ambaye amepoteza maisha akiwa bado kijana ingawa tayari alikuwa amekwishakutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya tasnia ya habari kutokana na umakini wake, uzingatiaji wa weledi kikamilifu na misingi mingine mikuu ya uandishi wa habari.
“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi kifo cha ghafla cha Ndugu Willy Edward Ogunde ambaye nimejulishwa kuwa kilitokea usiku wa kuamkia jana, Jumapili, huko Morogoro ambako alikuwa amekwenda kikazi. Ndugu Willy Edward Ogunde amepoteza maisha akiwa bado kijana sana hata kama ni kweli katika muda mfupi wa maisha ametokea kuwa mfano wa kuigwa katika tasnia ya habari kwa mchango wake wa kudumisha weledi na misingi mingine mikuu ya uandishi wa habari.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mheshimiwa Waziri salamu za dhati ya moyo wangu za rambirambi kuomboleza kifo cha kijana huyu wetu na mwanataaluma wako. Aidha, kupitia kwako nakuomba uniwasilishie salamu zangu kwa wanataaluma wote wa tasnia ya habari nchini kwa kuondokewa na mwenzao. Lakini zaidi, nakuomba unifikishe salamu zangu nyingi kwa wanafamilia, ndugu na jamaa wa Marehemu Willy Edward Ogunde.”
“Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa kwa sababu msiba wao ni msiba wangu pia. Naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu cha kufiwa na mpendwa wao. Nawaombea subira na uvulivu.
IMETOLEWA NA:
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
18 Juni, 2012
DAR ES SALAAM