Mkutano Mkuu wa Dharura wa Chama cha Mpira wa Miguu
wa Wanawake Tanzania (TWFA) utafanyika Juni 23 mwaka huu kwenye ukumbi
wa Msimbazi Centre, Dar es Salaam kuanzia saa 2.00 asubuhi.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa TWFA, Lina Kessy, ajenda
kuu katika mkutano huo ni marekebisho ya Katiba ya chama hicho yanayotokana
na maelekezo ya Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) juu ya marekebisho kwenye katiba za
wanachama wake ambazo zina upungufu.
Tayari mapendekezo ya marekebisho hayo kulingana
na mwongozo wa TFF yalishapitiwa na Kamati ya Utendaji ya TWFA.
Mbali ya Kamati ya Utendaji, wajumbe wengine wa mkutano
huo ni Mwenyekiti, Katibu na mjumbe wa Mkutano Mkuu kutokana vyama vya
mpira wa miguu wa wanawake vya mikoa ya Tanzania Bara.
Wajumbe watafikia kwenye hosteli ya Msimbazi Centre
ambapo wanatakiwa kuripoti siku moja kabla ya mkutano huo.
Mgeni rasmi atakayefungua mkutano huo anatarajiwa
kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Michezo katika Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Juliana Yasoda.