MKATABA
Serikali ya Tanzania na serikali ya Jamhuri ya watu wa China kesho
(18/06/2012) zinatarajia kutiliana saini mkataba wa ujenzi wa Bomba la
kusafirisha Ges asilia kutoka Mnazi Bay Mtwara hadi Ubungo jijini Dar es
Salaam.
Mkataba huo wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 2 (mbili)
utasainiwa mjini Beijing, China kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli
nchini kwa upande wa Tanzania (TPDC) na Benki ya Exim kwa upande wa
China.
Balozi wa Tanzania nchini China Mhe Phillipo Marmo amesema hayo leo
mjini Wuhan, China wakati akizungumza na Umoja wa Wanafunzi wa Tanzania
(Wuhan Tanzania Students Association-UTASA) wanaoishi mjini hapo.
"Kesho Tanzania inatarajia kutiliana saini mkataba wa ujenzi wa
bomba la gesi asilia kutoka Mnazi Bay Mtwara hadi Ubungo jijini Dar es
Salaam utakaokamilika ndani ya mezi 12 baada ya kutiwa saini," amesema.
Kwa mujibu wa Balozi Marmo, "serikali ya Tanzania imeiwekea dhamana PTDC ili kupata mkopo kutoka benki ya Exim ya China."
ujenzi wa bomba hilo la gesi ni miongoni mwa jitihada za serikali
kutatua kero ya umeme iliyodumu kwa muda mrefu kutokana na kupungua mara
kwa mara kwa kina cha maji katika mabwawa yanyozalisha umeme yakiwemo
Mtera na Kidatu ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo yanayo zalisha umeme
unaotumika katika gridi ya Taifa.
"Mradi huu ukikamilika utasaidia kutatua kero ya umeme katika miji
ya Dar es salaam. Arusha na kiasi kingine kitauzwa Nairobi nchini
Kenya," amesema.
Pamoja na kutiliana saini mkataba huo, serikali hizo mbili hivi
karibuni zimetiliana saini mkataba wa ujenzi wa nyumba 10,000 (elfu
kumi) za askari jeshi nchini ili kupunguza tatizo la ukosefu wa makazi.
Balozi Marmo amesema, "Ujenzi wa nyumba hizi 10,000 ni mkopo wa
riba nafuu kati ya asilimia 2 hadi moja utakaolipwa katika kipindi
cha miaka 20."
Hata hivyo hakufafanua zaidi juu ya gharama za mradi huo. Mradi huo utajengwa na kamuni kutoka China.
China imekuwa mdau mkubwa wa miradi ya maendeleo nchini Tanzania
tangu miaka ya 1960 na imejenga miradi mbalimbali ikiwemo TAZARA,
Urafiki, Uwanja wa Taifa n barabara kadha.