- Get link
- X
- Other Apps
Leo
ni siku ya wakimbizi duniani. Tanzania inaungana na Mataifa mengine
duniani katika kuadhimisha siku hii. Tangu kupata Uhuru Tanzania imekuwa
Taifa lililo mstari wa mbele katika kusaidia wakimbizi kutoka katika
Nchi mbalimbali hasa zile ilizopakana nazo.
Tanzania ni nchi ambayo
imezungukwa na kupakana na Nchi zenye machafuko, aidha ya vita vya
wenyewe kwa wenyewe kama ilivyokuwa kwa Burundi na Rwanda, pia imepakana
na nchi zenye makundi ya waasi wanaopinga serikali zao na kusababisha
machafuko kama vile Uganda, Somalia, Sudan na Kongo, lakini pia
imepakana na nchi zenye machafuko ya kisiasa kama vile Kenya na
Zimbabwe.
Siku za hapo nyuma kidogo, kutokana na Athari mbalimbali
zilizotokana na Idadi kubwa ya wakimbizi hapa nchini ambao ilikadiriwa
kufikia 1,000,000 Serikali ililazimika kubadili sera ya wakimbizi ambayo
ilitoa fursa ya kila familia kupatiwa hekta mbili na nusu za ardhi na
kuanzisha makazi na badala yake kuwatengea maeneo maalum ya makambi,
pamoja na hilo Serikali iliendelea kutafuta namna ya kuondokana na
Athari hizo na hivyo kufikiria njia mbadala katika kutafuta namna nzuri
ya kuondokana na Athari zilizoletwa na wakimbizi kama uharibifu wa
mazingira, ujambazi, wizi lakini pia wakimbizi walikuwa ni mzigo mkubwa
kwa serikali kwani walitakiwa kupata stahili zote za maisha ikiwemo,
chakula, malazi, mavazi pamoja na Ulinzi. Gharama za huduma hizi zote
zilikuwa chini ya Serikali ingawa baadhi ya Serikali za Mataifa makubwa
zilisaidia pamoja na Mashirika kama UNICEF, OAU na UNHCR.
Katika
kufikiri juu ya kuondokana na tatizo hili, Serikali ya Awamu yaTatu na
Nne chini ya Rais Jakaya M. Kikwete waliamua kuwa ni vema kwenda katika
nchi husika na kushauri njia sahihi za mazungumzo na kumaliza tofauti
zao ili kuweza kupata Amani ambayo itawezesha wakimbizi kurudi katika
Nchi zao. Juhudu hizi zilizaa matunda kwa Baadhi ya Nchi ikiwemo
Burundi, Rwanda na Kenya hivi karibuni.
Aidha, katika kuazimisha
siku hii ya wakimbizi, lipo jambo la msingi ambalo kama Taifa lazima
tujifunze na tulielewe kutoka katika mafunzo hayo. Jambo lenyewe ni
Umuhimu wa kutunza Amani yetu. Sehemu zote ambazo zimezalisha wakimbizi
hazikuwa na sababu nyingine kama njaa ama majanga ya asili bali ni
kutokana na sababu kuu moja ya kuvunjika kwa Amani. Lakini tukienda
mbele zaidi na kujiuliza ni nini chanzo cha uvunjifu huo wa Amani,
tunapata jibu kuwa ni kutokana na Uroho wa Madaraka na Ukabila.
Katika mambo ya msingi ambayo kama Taifa tulifundwa na kuaminishwa ni
pamoja na kupinga namna yoyote ya kubaguana kikabila, kidini ama
kikanda. Lakini pia tukafundwa katika misingi ya Uzalendo na Utaifa
pamoja na Kuheshimu Utawala wa Sheria na Mamlaka ya Nchi. Lakini hivi
sasa hali imekuwa Tofauti, tayari wapo watu ambao wameanza kutia doa na
kuchokonoa yale yanayotujenga kama Taifa lenye Amani, tayari wapo
wanaonadi Ubaguzi na Utengano, wapo wanaodharau na hata kubeza mamlaka
husika na hawaheshimu tena Utawala wa Sheria. Mambo haya yanafanywa kwa
jina la siasa, tumekuwa tukishuhudia kauli pamoja na matendo
yanayodhihirisha muelekeo huu mbaya.
Hali hii haitoi picha nzuri
katika mustakabali wa kujenga , kuendeleza na kuimarisha Taifa letu.
Tanzania tunao utamaduni wa kuheshimu Mamlaka na Utii wa Sheria. Lazima
wote tangu sasa tuamue kuchukua hatua thabiti kulinda umoja na amani
yetu, kwani hata sisi twaweza kuwa wakimbizi pia. Hatuna kinga ya kuzuia
hilo isipokuwa kurudi katika misingi yetu iliyowekwa na waasisi wa
Taifa hili. Jukumu la kustawisha na kulinda umoja na amani yetu ni letu
wote. Tuilinde Tanzania yetu, tujivunie Utaifa wetu.
- Get link
- X
- Other Apps