- Get link
- X
- Other Apps
Kenya
imetangaza siku tatu za maombolezi baada ya kifo cha Waziri wa Usalama
wa Kenya, Profesa George Saitoti, na naibu wake, Orwa Ojode, kwenye
ajali ya helikopta ya polisi katika eneo la Ngong, nje ya Nairobi.
Rais
Mwai Kibaki alisema kifo cha Bwana Saitoti ni msiba mkubwa kwa taifa,
na serikali imetangaza kuwa baraza la mawaziri litakutana Jumatatu,
kujadili tukio hilo.
Idara
ya polisi imesema uchunguzi utafanywa kujua sababu ya ajali hiyo, na
balozi wa Marekani mjini Nairobi, amesema Marekani iko tayari kusaidia
kwenye uchunguzi huo, ikiwa itatakiwa kufanya hivo.
Msemaji wa polisi alieleza kwamba inavoelekea kuanguka kwa helikopta hiyo lilikuwa tukio la ajali.
Raia
wa Kenya walikuwa na masikitiko Jumapili, baada ya taarifa ya ajali
hiyo kujulikana, na watu wamekuwa wakizuru nyumba ya kuhifadhi maiti
mjini Nairobi kutoa heshima zao.
Makamo
wa rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka, alipofika kwenye tukio la ajali
alitoa rambi-rambi zake na alieleza wale waliokuwamo ndani ya ndege
ambao wote wameteketea:
"Ndege
hiyo ya aina ya Eurocopter ya police airwing, ambayo ilikuwa inaelekea
Yugis, ilikuwa imembeba Waziri George Saitoti, naibu waziri Orwa Ojode
na maafisa rubani wa ndege, Nancy Gitwanja na Luke Oyugi, na vilevile
askari wawili ambao wanakuwa wanaandamana na Waziri Saitoti, Inspector
Tonkei na Thomas Murimi"
Rambi-rambi
zimekuwa zikimiminika nchini Kenya, pamoja na za Kofi Annan, Katibu
Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, ambaye alipatanisha baada ya ghasia
za uchaguzi uliopita nchini kenya.
Profesa
Saitoti alikuwa akizungumza kwa ukali dhidi ya al-Shabaab na inaaminiwa
alihusika na uamuzi wa jeshi la Kenya kuingia Somalia mwaka jana.
Bwana
Saitoti aliwahi kuwa makamo wa rais na waziri wa fedha katika serikali
ya Rais Moi, na akitarajiwa kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka
ujao.
Alikuwa na umri wa mika 67.
- Get link
- X
- Other Apps