Kamati
ya Uchaguzi ya TFF inawataarifu wadau na wapenzi wa soka kuwa mchakato
wa uchaguzi wa viongozi wa YANGA kujaza nafasi zilizowazi za Kamati ya
Utendaji unaendelea vizuri chini ya Kamati ya Uchaguzi ya YANGA.
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF imepokea kutoka Kamati ya Uchaguzi ya YANGA nakala
za fomu za maombi ya uongozi wa YANGA pamoja na nakala za vyeti vya
elimu vya waombaji uongozi kama sehemu ya taarifa ya awali ya mchakato
wa uchaguzi huo wa YANGA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imebaini kuwa baadhi
ya waombaji uongozi wamewasilisha nakala za vyeti vya kuhudhuria masomo
ya sekondari (Secondary School Leaving Certificate) badala ya nakala za vyeti vya kuhitimu masomo ya elimu ya sekondari (Certificate of Secondary Education).
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF imekwisha ielekeza Kamati ya Uchaguzi ya YANGA
kuwataka wagombea wote kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF
Ibara ya 10(4) na (5) inayowataka wagombea wote kujaza Fomu Na.1 ya
maombi ya uongozi na kuambatanisha nakala ya cheti cha Elimu ya
Sekondari (Certificate of Secondary Education) kama
ilivyoainishwa kwenye Fomu Na.1 kipengere Na.9. Kamati ya Uchaguzi ya
TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya YANGA iwashauri wagombea ambao vyeti
vyao vimepotea wawasiliane na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA)
kwa maandishi ili kupata ‘Statement of Examination Results’ itakayotumwa kwa Kamati ya Uchaguzi ya YANGA kupitia TFF kuthibitisha kuwa wamehitimu elimu ya kidato cha nne.
Uhakiki
wa vyeti vya elimu ya sekondari vya waombaji uongozi hufanywa na NECTA
na vyuo husika kwa elimu ya juu kwa chaguzi za wanachama wa TFF.
Wanachama wote wa TFF wanatakiwa kuzingatia kikamilifu matakwa ya Kanuni
za Uchaguzi.