KAIMU MKURUGENZI MPYA WA ATCL
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika la
Ndege la Air Tanzania (ATCL), Kapteni Milton Lusajo Lazaro.
Na mwandishi wetu
IKIWA siku mmoja tu baada ya kuteuliwa kuwa
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL), Kapteni
Milton Lusajo Lazaro amesema shirika hilo linanafasi kubwa ya kupata mafanikio
iwapo litaendelea kutekeleza mpango wake wamaendeleo wa miaka mitano.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana,
Lusajo alisema atatumia uzoefu wake alioupata katika sekta ya usafiri wa anga kuleta
mabadiriko katika shirika hilo na kuliwezesha kushindana sambamba na kampuni
nyingine za ndani na nje ya nchi.
Kpt. Lusajo rubani anaeheshimika katika
sekta ya usafiri wa anga si kwa Afrika Mashariki pekee ila Afrika kwa ujumla na
anarekodi ya kuendesha ndege kwa masaa zaidi ya elfu kumi na mbili na pia
amewahi kushika nyadhifa tofauti katika Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania
(TCAA) pamoja na ATCL kabla ya kuteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL.
“Napenda kutoa shukrani zangu kwa waziri Mwakyembe
na viongozi wengine wa Wizara kwa kuwa na imani nami. Nimekubali uteuzi wake na
nitafanya kazi alienipa kwa moyo mmoja.
Nina
ahidi kuwa nitautumia uzoefu wangu wa zaidi ya miaka 35 katika sekta ya usafiri
wa anga na kuipa ATCL uwezo kushindana kibiashara. Natoa wito kwa wafanyakazi
wenzangu kutoa ushirikiano ilituweze kusonga mbele. ,” alisema.
Lazaro alisema kampuni yake itaendelea kutoa huduma kama
kawaida na kuongeza kuwa safari zote za kampuni zitaendelea kama ilivyopangwa
na ratiba licha ya mabadiliko ya uongozi.
“Hakuna sababu ya
wananchi kuwa na wasi wasi. Kilichotokea ni mabadiliko ya uongozi tu lakini
mipango na shughuli zote za kampuni zinaendelea kama ilivyopangwa,” alisema.
Lazaro aliongeza kuwa jukumu kubwa alionalombele yake ni kuongeza
idadi ya ndege za shirika hilo aidha kwa kukodi au kuingia ubia na makampuni
mengine katika jitihada za kuimarisha nafasi ya kampuni yake ili iweze kushindana
kitaifa na kimataifa katika miaka michache ijayo.
“ATCL
haiwezi kupata mafanikio bila kuwa na ushirikiano mzuri na serikali pamoja na
wananchi kwa ujumla. Nawaomba wananchi waendelee kuonyesha ushirikiano na
uzalendo waliouonyesha katika wiki chache zilizopita baada ya kuanza kwa huduma
za kampuni yetu.
“Nawahakikishia wateja wetu na wananchi kwa
ujumla kuwa kampuni yangu itaendelea kutoa huduma na bidhaa bora zilizo katika
bei za kiushindani ukilinganisha na makampuni mengine yanayotoa huduma hii
katika soko,” alisema.