HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA MIZENGO PETER PINDA (MB), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2012/2013
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika,
naomba kutoa Hoja kwamba kutokana na Taarifa zilizowasilishwa leo ndani
ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na
Utawala na Kamati ya Fedha na Uchumi zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya
Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2011/2012 na Mwelekeo wa Kazi
za Serikali kwa mwaka 2012/2013. Vilevile, naliomba Bunge lako Tukufu
likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri
Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,
Taasisi zilizo chini yake pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2012/2013.
2. Mheshimiwa Spika, tangu
tulipohaitimisha Mkutano wa Bajeti wa Bunge hili mwaka jana, Nchi
yetu imekumbwa na Majanga na Matukio mbalimbali yaliyosababisha vifo
na uharibifu wa mali. Nitumie fursa hii kutoa pole kwa wote
waliofiwa na Ndugu, Jamaa na Marafiki. Mungu azilaze Roho za
Marehemu mahali Pema Peponi. Kwa ndugu zetu walioumia na bado
wanajiuguza, tumwombe Mwenyezi Mungu awasaidie kupona haraka na kurejea
katika shughuli za ujenzi wa Taifa.
3. Mheshimiwa Spika,
nijiunge na wenzangu waliotangulia kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge
wapya, Mawaziri na Naibu Mawaziri walioteuliwa na Mheshimiwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Mei 2012. Aidha, napenda
kumpongeza Mheshimiwa Mussa Zungu Azzan, Mbunge wa Ilala, kwa
kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge. Nawapongeza pia Wenyeviti na
Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge waliochaguliwa
kuchukua nafasi zilizoachwa wazi. Vilevile, nawapongeza Waheshimiwa
Wabunge waliochaguliwa na Bunge lako Tukufu kuiwakilisha Tanzania katika
Bunge la Afrika Mashariki. Natarajia kwamba wote walioteuliwa na
kuchaguliwa watatumia nafasi hizo kwa manufaa ya Bunge na kwa maendeleo
ya Watanzania kwa ujumla.
4. Mheshimiwa Spika, kwa takriban siku Tano Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kujadili Taarifa
Kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2011, Mpango wa
Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/2013. Napenda
kutoa Pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Stephen Masatu Wasira (Mb.),
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu; na Mheshimiwa Dkt.
William Augustao Mgimwa (Mb.), Waziri wa Fedha kwa Hotuba nzuri na
ufafanuzi wa Hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge.
Vilevile, napenda kutoa shukrani zangu kwa Waheshimiwa Wabunge kwa
kujadili kwa kina Hotuba hizo na hatimaye kupitisha Bajeti ya Serikali
kwa mwaka 2012/2013.
5. Mheshimiwa Spika,
kipekee, nitumie nafasi hii, kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala inayoongozwa na Mheshimiwa Pindi
Hazara Chana, Mbunge wa Viti Maalum. Nawashukuru pia Wajumbe wa Kamati
ya Fedha na Uchumi inayoongozwa na Mheshimiwa Andrew John Chenge, Mbunge
wa Bariadi Magharibi. Kamati hizo zimetoa mchango mkubwa wakati wa
uchambuzi wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Mafungu ya
Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa na Mfuko wa Bunge. Aidha, nawashukuru Wajumbe wa Kamati zote
za Kudumu za Bunge lako Tukufu kwa ushauri waliotoa wakati wa kupitia
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za
Serikali Zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Maoni na
Ushauri wao utazingatiwa wakati wa utekelezaji wa Bajeti hii.
6. Mheshimiwa Spika,
Bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge ni mwendelezo wa utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010. Vilevile,
imezingatia Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa kutekeleza
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Malengo ya Maendeleo ya Milenia na
Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini. Katika
mwaka 2012/2013, Serikali itaimarisha usimamizi wa utekelezaji wa
Mipango na Miradi ya Maendeleo, matumizi ya fedha za Umma na
uwajibikaji. Tutatumia rasilimali chache tulizonazo kwa kazi ambazo
zitajielekeza kwenye shughuli za uzalishaji mali na kuongeza tija ili
kuchochea ukuaji wa haraka wa uchumi.
HALI YA UCHUMI
7. Mheshimiwa Spika, Pato la Taifa kwa mwaka 2011 lilikua kwa Asilimia 6.4 ikilinganishwa na Asilimia 7 mwaka 2010. Ukuaji huo wa Asilimia 6.4
ni mkubwa ikilinganishwa na kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Nchi za
Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambacho kilikuwa wastani wa Asilimia 5.1.
Kushuka kwa kiwango cha ukuaji uchumi wetu kulichangiwa kwa kiasi
kikubwa na ukame ambao uliathiri zaidi Sekta ya Kilimo na uzalishaji wa
Nishati ya Umeme Nchini. Tatizo la umeme, upungufu wa chakula katika
baadhi ya maeneo Nchini pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta katika Soko
la Dunia vilichangia pia kuongezeka kwa mfumuko wa bei. Hatua
zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kudhibiti Mfumuko wa Bei ni pamoja
na kurejesha upatikanaji wa umeme kwenye hali ya kawaida na kuimarisha
ugavi wa chakula Nchini. Hatua hizo, zimeanza kupunguza kiwango cha
Mfumuko wa Bei. Ni vyema tukumbuke kwamba, hatua za kukabili tatizo la
kiuchumi kama vile Mfumuko wa Bei zinapochukuliwa leo, matokeo yake
hayawezi kuonekana siku hiyo hiyo. Wataalam wanaeleza kwamba mara nyingi
inachukua miezi 6 hadi 18 kuona dhahiri matokeo ya hatua zilizochukuliwa. Hivyo, siku za usoni tutashuhudia Mfumuko wa Bei ukipungua zaidi.
Maboresho ya Sekta ya Fedha
8. Mheshimiwa Spika, Taasisi
za Fedha zina mchango mkubwa katika kuchochea kasi ya maendeleo na
ukuaji wa Uchumi. Kwa kutambua mchango huo, Serikali inatekeleza
Programu ya Maboresho ya Sekta ya Fedha, ambayo imekuwa na mafanikio ya
kuridhisha. Mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya Taasisi
za Fedha ambazo hadi sasa zimefikia 49 zikiwa na Matawi 519 Nchini kote. Aidha, baadhi ya Taasisi hizo zimeonesha mafanikio makubwa katika eneo la huduma za Kibenki kwa njia ya mtandao.
9. Mheshimiwa Spika, Serikali
pia imetoa msukumo wa uanzishaji wa huduma za Kifedha kupitia Vyama vya
Kuweka na Kukopa (SACCOs) ambavyo hadi sasa vimefikia 5,346. Vyama hivyo vimetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 627.2.
Pamoja na mafanikio hayo, changamoto kubwa inayoikabili Sekta ya Fedha
ni viwango vikubwa vya riba kwenye Mikopo vinavyoendelea kutozwa na
Benki za Biashara ikilinganishwa na riba ndogo inayolipwa kwa amana.
Changamoto nyingine ni kukosekana kwa Taasisi nyingi za fedha
zinazotoa Mikopo ya muda mrefu yenye masharti nafuu kwa Miradi ya
Maendeleo hasa kwenye Sekta ya Kilimo. Serikali inatambua
Changamoto hizo na tayari Mikakati inaandaliwa kukabiliana nazo hususan
kuanzisha Dirisha la Kilimo katika Benki ya Rasilimali Tanzania pamoja
na kukamilisha mchakato wa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo.
Aidha, Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji pamoja na
kuanzisha Mfumo wa kuwatambua wakopaji (Credit Reference Bureau).
SENSA YA WATU NA MAKAZI 2012
10. Mheshimiwa Spika,
katika hotuba zangu za Bajeti za miaka Miwili iliyopita, nililijulisha
Bunge lako Tukufu kuhusu maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ambayo
itafanyika tarehe 26 Agosti 2012. Nilianza kutoa Taarifa ya Sensa mapema
kwa kuwa Sensa ni mchakato unaohitaji maandalizi ya muda mrefu kabla na
baada ya zoezi lenyewe la kuhesabu Watu. Kwa kutambua umuhimu wa Sensa
katika kuandaa na kutekeleza Mipango ya Maendeleo ya Nchi, zoezi hili
limepewa kipaumbele cha pekee katika Bajeti ya Serikali ya mwaka
2012/2013. Katika Awamu ya Kwanza ya maandalizi ya Sensa, kazi
zilizofanyika ni pamoja na kutenga maeneo ya kuhesabia Watu, kutayarisha
Madodoso na Miongozo mbalimbali, kufanya Sensa ya Majaribio, kununua
vitendea kazi, kuchapisha Nyaraka za Sensa na kuunda Kamati za Sensa za
Mikoa na Wilaya.
11. Mheshimiwa Spika,
kazi za Sensa zinazoendelea ni uhamasishaji na kutoa Elimu kwa Umma ili
kila Mwananchi ashiriki kikamilifu katika zoezi hilo. Shughuli nyingine
ni utoaji wa mafunzo kwa watakaokuwa Makarani wa Kuhesabu Watu na
Wasimamizi, usambazaji wa Vifaa na Maandalizi ya kuingiza takwimu kwenye
Kompyuta. Katika utekelezaji wa zoezi hili, Serikali itawatumia
Watumishi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Walimu. Kutokana na sababu
hiyo, Serikali imelazimika kubadili mihula ya Shule ili Walimu waweze
kusaidia katika zoezi hili la Sensa.
12. Mheshimiwa Spika,
nawaomba Viongozi wote tusaidiane kuhamasisha na kusimamia utekelezaji
wa zoezi la Sensa katika maeneo yetu. Nawaomba Wananchi wote washiriki
katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwa kutoa ushirikiano na taarifa
sahihi kwa Makarani wa Sensa na Wasimamizi ambao watatembelea Kaya zetu
tarehe 26 Agosti 2012. Niwahakikishie Wananchi wote, kuwa taarifa zote
zinazokusanywa wakati wa Sensa ni Siri na zitatumika kwa shughuli za
Kitakwimu tu. Takwimu hizo hazina uhusiano na Dini, Kodi, Siasa au mambo
mengine kama hayo ambayo hayakukusudiwa.
KUIMARISHA DEMOKRASIA NA MUUNGANO
Hali ya Siasa
13. Mheshimiwa Spika,
kumekuwa na mwamko mkubwa wa Wananchi kushiriki kwenye masuala ya
Kisiasa hali inayoashiria kukua kwa Demokrasia Nchini. Vyama vipya vya
Siasa vimeendelea kusajiliwa na vilivyopo kujiimarisha zaidi. Katika
mwaka 2011/2012, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imepokea maombi ya
kusajili Vyama vipya Viwili vya Siasa. Chama cha Kijamii (CCK) kimepata
Usajili wa Kudumu na kufanya idadi ya Vyama vyenye Usajili wa Kudumu
kufikia 19. Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimepata Usajili wa muda na Chama cha Movement for Democratic and Economic Change kinaendelea kufanyiwa uhakiki.
14. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2012/2013, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaendelea
kushughulikia maombi ya Usajili wa Vyama, kuendelea kutoa elimu kwa
Wananchi kuhusu mfumo wa Vyama vingi vya Siasa na Sheria ya Gharama za
Uchaguzi ya mwaka 2010. Aidha, itafuatilia uhai wa Vyama vya Siasa kwa
mujibu wa Sheria na kuanzisha Ofisi mbili za Kanda. Kanda hizo ni ile ya
Kusini inayojumuisha Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma na Kanda ya
Magharibi inayojumuisha Mikoa ya Tabora, Kigoma, Shinyanga na Katavi.
Nitumie nafasi hii kuwasihi Watanzania kutumia fursa ya kupanuka kwa
Demokrasia kuendelea kushiriki kwenye Siasa kwa kufuata Sheria, Kanuni
na Taratibu za Nchi. Viongozi wa Vyama vya Siasa waonyeshe mfano wa
kuendesha Siasa za kistaarabu zenye lengo la kuunganisha Watanzania na siyo kuwachonganisha.
Hakuna Nchi au Kiongozi aliyewahi kupata sifa nzuri kwa kuwa chanzo cha
mifarakano. Tudumishe utulivu na amani pamoja na ustaarabu wetu wa
Kitanzania.
Mabadiliko ya Katiba
15. Mheshimiwa Spika,
Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa katika Mkutano wa Tano wa Bunge,
mwezi Novemba 2011, Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba Na. 8 ya Mwaka 2011 (Sura ya 83). Aidha, Bunge
lilifanya marekebisho ya Sheria hiyo katika Mkutano wa Sita, mwezi
Februari 2012. Hatua hiyo, ilimwezesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, kuteua Wajumbe wa Tume itakayoratibu na kukusanya
Maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba. Tume hiyo yenye Wajumbe 32 inajumuisha Wawakilishi wa Makundi mbalimbali katika jamii kutoka pande mbili za Muungano.
16. Mheshimiwa Spika, Tume
imeanza kazi rasmi tarehe 1 Mei 2012, kama ilivyopangwa. Serikali
imefanya maandalizi muhimu kuiwezesha Tume kufanya kazi yake ipasavyo
ikiwa ni pamoja na kuipatia Vifaa vya Kisasa vya kukusanya na Kutunza
Kumbukumbu na kufungua Tovuti rasmi. Aidha, Idara ya Mpigachapa Mkuu wa
Serikali imepewa jukumu la kuchapisha kwa wingi Katiba na Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ili Wananchi waweze kuelewa na kutoa michango yao
kwa uhakika zaidi kwenye mchakato wa kutoa maoni.
17. Mheshimiwa Spika,
napenda nichukue fursa hii tena kumpongeza Mheshimiwa Jaji Joseph
Sinde Warioba, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu kwa
kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Mheshimiwa
Augustino Ramadhani, Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania kwa kuteuliwa kuwa
Makamu Mwenyekiti. Vilevile, napenda kuwapongeza Wajumbe wote, wakiwemo
Katibu na Naibu Katibu kwa kuteuliwa kuunda Tume hiyo. Napenda kuwasihi
Wananchi wajitokeze kwa wingi na kutoa maoni yao kwa utulivu katika
Mikutano itakayoitishwa na Tume na kuwapa Wajumbe ushirikiano wa kutosha
ili hatimaye tupate Katiba iliyoandikwa na Watanzania wenyewe.
Muungano
18. Mheshimiwa Spika, tarehe 26 Aprili 2012, Muungano wetu ulitimiza Miaka 48 ya Watanzania kuishi pamoja, kwa amani na utulivu. Katika mwaka 2011/2012, Vikao 14 vya
Kisekta vya Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Serikali ya Muungano wa
Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) vilifanyika
kutafuta ufumbuzi wa changamoto za Muungano. Kikao cha Kamati ya Pamoja
cha SMT na SMZ, chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt.
Mohamed Gharib Bilal, kilifanyika ambapo Hoja 13 zilijadiliwa
na Hoja Mbili zilipatiwa ufumbuzi. Hoja zilizopatiwa ufumbuzi ni kuhusu
ongezeko kubwa la Ankara za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO na Mfuko wa
Maendeleo ya Jimbo. Aidha, imekubalika kuwa marekebisho ya Sheria
yafanyike mapema ili kupata ufumbuzi katika hoja zinazohusu Usajili wa
Vyombo vya Moto, Kodi ya Mapato na Kodi ya Zuio (Withholding Tax).
19. Mheshimiwa Spika,
Hoja nyingine ambazo zipo katika hatua mbalimbali za kutafutiwa
ufumbuzi zitaendelea kujadiliwa katika Vikao vya Kamati ya pamoja
vya Kisekta na Kamati ya Pamoja. Serikali pia itaendelea kuratibu
masuala yasiyo ya Muungano kwa kuhakikisha kwamba Sekta, Wizara na Asasi
Zisizo za Muungano zinakutana na kujadili changamoto zilizopo. Ni
ukweli usiopingika kwamba, Muungano wowote Duniani unakutana na
changamoto mbalimbali. Jambo muhimu ni pande zote zinazounda Muungano
kuzitatua changamoto hizo. Hivyo, ni vyema tukaendelea kukaa pamoja na
kujadiliana ili Muungano wetu huu ambao msingi wake ni mahusiano ya
kihistoria ya pande zote mbili uendelee kudumu kwa faida ya watu wetu.
BUNGE
20. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2011/2012, Bunge limetekeleza kwa ufanisi majukumu yake ya
msingi ya kutunga Sheria na kuisimamia Serikali. Kamati za Kudumu za
Bunge pia zimetekeleza majukumu yake ipasavyo na Bunge zima limefanya
Mikutano Minne kwa mujibu wa Sheria. Katika Mikutano mitatu
iliyofanyika, Miswada ya Sheria Nane (8) ilipitishwa na Maswali ya kawaida 373 na ya Nyongeza 894 ya Waheshimiwa Wabunge yalijibiwa na Serikali. Aidha, Maswali ya Msingi 78
ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa na kujibiwa. Hoja
mbalimbali za Kamati za Kudumu za Bunge ziliwasilishwa na kujadiliwa.
21. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2012/2013, Ofisi ya Bunge itakarabati Ukumbi wa Bunge na
kuboresha miundombinu mingine ya Ofisi zake ikiwa ni pamoja na kuweka
Vifaa vya Mawasiliano na kuendelea na ujenzi wa Ofisi za Wabunge katika
Majimbo. Aidha, huduma za Utafiti na Sheria zitaimarishwa sambamba na
shughuli za Kamati za Kudumu za Bunge.
MAENDELEO YA SEKTA BINAFSI, UWEKEZAJI NA UWEZESHAJI
Maendeleo ya Sekta Binafsi
22. Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Sekta Binafsi ili
iweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na kufanya
biashara na hatimaye kuwa Injini ya Ukuaji wa Uchumi. Katika kufanikisha lengo hilo, Serikali
inasimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya
Biashara na Uwekezaji Nchini wenye lengo la kurekebisha mifumo iliyopo
ili kupunguza gharama za kufanya biashara na kuwekeza Nchini. Hatua
zilizochukuliwa ni pamoja na uanzishaji wa Kituo Kimoja cha Utoaji wa
Huduma kwenye Bandari ya Dar es Salaam, ambapo muda wa mizigo kukaa
Bandarini umepungua kutoka wastani wa Siku 25 mwaka 2009 hadi kufikia wastani wa Siku 9 mwezi Mei 2012.
23. Mheshimiwa Spika, hatua nyingine ni kupunguza Vizuizi vya Kudumu katika Barabara Kuu, kuunda Kamati za pamoja kwenye Vituo vya Mipakani mwa Nchi (Joint Border Post Committees), kuendelea na taratibu za kuanzishwa kwa Vituo vya Utoaji Huduma kwa Pamoja Mipakani (One Stop Border Posts)
na kuweka mkazo kwenye matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki kwenye maeneo
ya ulipaji Kodi, Mabenki, Usajili wa Makampuni na utunzaji wa
kumbukumbu kwenye Masjala mbalimbali. Sambamba na hatua hizo,
majadiliano na Sekta Binafsi yamefanyika kwa lengo la kupata ufumbuzi wa
changamoto za Kisera, Kisheria na Mifumo ya Kitaasisi zinazoikabili
Sekta hiyo. Katika mwaka 2012/2013, Serikali
itafanya tafiti zinazohusiana na maendeleo ya Sekta Binafsi, pamoja na
kuendeleza mashauriano na Sekta Binafsi, Washirika wa Maendeleo na
Taasisi Zisizo za Serikali kwa lengo la kuiwezesha Sekta Binafsi
kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Uwekezaji
24. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2011/2012, Serikali imefanya juhudi kubwa za kuhamasisha
na kuvutia Wawekezaji wa Ndani na Nje. Kutokana na juhudi hizo, Kituo
cha Uwekezaji Nchini kilisajili jumla ya Miradi 681 yenye thamani ya Shilingi Trilioni 11.6 na fursa za Ajira 89,803. Kati ya Miradi iliyosajiliwa, Miradi 356 sawa na Asilimia 52.3 ni ya Wawekezaji wa Ndani, Miradi 166, sawa na Asilimia 24.4 ni ya Ubia kati ya Wawekezaji wa Ndani na Nje na Miradi 159, sawa na Asilimia 23.3 ni ya Wawekezaji wa Nje. Mitaji ya moja kwa moja ya Wawekezaji wa Nje (FDI), iliyoingizwa Nchini imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 681.2 mwaka 2010 hadi Trilioni 1.3 mwaka 2011.
25. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuongeza kasi ya Uwekezaji Nchini kupitia Sera ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Serikali
imefanya maandalizi ya msingi ya kuanzisha Kitengo cha Uratibu wa
masuala ya Ubia kwenye Kituo cha Uwekezaji na Kitengo cha Fedha (PPP –
Finance Unit) kwenye Wizara ya Fedha. Jumla ya Miradi 125
iliyoainishwa na Wizara mbalimbali itafanyiwa uchambuzi zaidi na Vitengo
hivi ili kubaini kama inakidhi vigezo vya kutekelezwa chini ya
utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Miradi hiyo ni
pamoja na ile ya kuzalisha umeme, ujenzi wa barabara, reli, bandari, na
ujenzi wa majengo kwa ajili ya Ofisi na biashara.
26. Mheshimiwa Spika,
Serikali imeweka umuhimu wa kipekee kuhamasisha ushiriki wa Wawekezaji
wa Kitanzania kuanzisha Miradi ya Uwekezaji katika Mikoa na Wilaya kwa
kuandaa Makongamano na Mikutano ya Kuhamasisha Uwekezaji na kutoa
elimu ya ujasiriamali kwa Wawekezaji Wadogo. Hadi sasa, Mikutano ya
kuhamasisha Uwekezaji imefanyika katika Mikoa ya Ukanda wa Ziwa
Tanganyika ya Rukwa, Katavi na Kigoma pamoja na Mikoa ya Mara, Singida,
Arusha na Mbeya. Aidha, Wilaya za Mbinga, Njombe, Mufindi, Mbozi na
Kahama nazo zimefanya Mikutano hiyo. Mikutano ya Kikanda ya Uwekezaji
itaendelea kufanyika katika mwaka 2012/2013. Nahimiza, Viongozi wa Mikoa
na Wilaya kuandaa Mikutano hiyo na kuondoa Vikwazo vinavyokwamisha
uwekezaji katika maeneo yao. Ofisi ya Waziri Mkuu itasambaza Mwongozo
kwa Mikoa ili ishirikiane ipasavyo na Mamlaka za Serikali za Mitaa
kuandaa Mikutano ya Uwekezaji.
27. Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kushiriki katika Mikutano mbalimbali inayohusu
masuala ya uchumi, biashara na uwekezaji. Mwezi Mei 2012, Tanzania
ilishiriki katika Mkutano wa World Economic Forum – Addis Ababa na
baadaye katika Mkutano wa Nchi Nane Zilizoendelea katika Viwanda (G8)
huko Washington, Marekani. Katika mikutano hiyo, Serikali ilielezea
Mipango yetu ya kuleta Mapinduzi ya Kilimo Nchini, hususan Mpango wa
Kukuza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (Southern
Agricultural Growth Corridor of Tanzania – SAGCOT). Mipango hiyo
ilipokelewa na kukubalika ambapo Tanzania imeingizwa katika Mpango wa G8 wa Kuendeleza Kilimo Barani Afrika. Nchi nyingine Barani Afrika zilizokubalika kushiriki katika Mpango huo ujulikanao kama G8 The New Alliance for Food Security and Nutrition ni Ethiopia na Ghana. Chini Mpango huu, Tanzania itanufaika na misaada ya Shilingi Trilioni 1.41 kwa ajili ya kuwekeza katika Sekta ya Kilimo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
28. Mheshimiwa Spika,
napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uongozi wake
Mahiri na juhudi zake za kuhakikisha kwamba Nchi yetu inakuwa moja
ya Nchi Tatu Barani Afrika zitakazonufaika na Mpango huo. Hii
inathibitisha kuwa ziara za Mheshimiwa Rais Nje ya Nchi mara nyingi zina
manufaa makubwa kwa uchumi na maendeleo ya Nchi yetu.
29. Mheshimiwa Spika,
maandalizi ya kuainisha Miradi itakayotekelezwa na Wawekezaji wa Ndani
na Nje katika Ukanda wa SAGCOT yameanza. Kutokana na ukubwa wa ukanda
huo wa Kilimo, Miradi itakayoainishwa itatekelezwa kwa Mfumo wa Kongano (Clusters) ambapo Wakulima Wadogo watashirikiana na Wawekezaji Wakubwa kuendeleza Kilimo.
30. Mheshimiwa Spika,
tumeanza kuona matunda mazuri yaliyotokana na ushirikiano kati ya
Wawekezaji Wakubwa na Wakulima Wadogo katika kuongeza uzalishaji na
tija. Hali hii imejionesha dhahiri kwenye Kilimo cha Mpunga huko
Kilombero ambapo Kampuni ya Kilombero Plantations Limited
iliyowekeza kwenye Shamba la Mngeta Wilayani Kilombero imewasaidia
Wakulima Wadogo kupata Teknolojia rahisi ya kupanda na kupalilia mpunga.
Wakulima hao wamewezeshwa kuanzisha vikundi vya uzalishaji na
kukopeshwa mbegu bora. Kutokana na ushirikiano huo, uzalishaji wa mpunga
kwa Wakulima Wadogo umeongezeka kutoka wastani wa Tani Mbili hadi Tani
Saba kwa Hekta moja. Utaratibu wa namna hiyo pia unatumiwa na Mwekezaji
wa Kampuni ya Sukari Kilombero na umewanufaisha Wakulima Wadogo wa Miwa
Wilayani Kilombero kupitia vikundi vyao vya uzalishaji.
Ushirikiano wa aina hiyo unatoa fursa za Masoko na Usindikaji wa Mazao
yanayozalishwa na Wakulima Wadogo wanaozunguka mashamba ya Wawekezaji
Wakubwa. Hii ni dalili njema kabisa na mfano wa kuigwa na Wawekezaji
Wakubwa na Wakulima Wadogo Nchini.
31. Mheshimiwa Spika,
natoa wito kwa Watanzania wenzangu kuona uwekezaji mkubwa katika
Kilimo kama fursa muhimu ya kuongeza uzalishaji na tija. Jambo la msingi
ni kuhakikisha kwamba maslahi ya Wakulima Wadogo yanalindwa kwa
kuwekeana mikataba mizuri na kufuatilia utekelezaji wake. Ni imani yangu
kwamba, tukiitumia vizuri ardhi yenye rutuba tuliyonayo tutaweza
kuongeza ukuaji kwenye Sekta ya Kilimo ambayo ni tegemeo kwa Watanzania
wengi na hatimaye kupunguza Umaskini wa Kipato.
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
32. Mheshimiwa Spika,
Serikali kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 kupitia Programu na Mifuko
mbalimbali. Hadi kufikia mwezi Aprili 2012, Mfuko wa Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi (Mwananchi Empowerment Fund), umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.3 kwa Wajasiriamali 7,187
katika Mikoa ya Dodoma, Lindi, Manyara, Mtwara, Pwani, Rukwa, Ruvuma,
Singida na Tanga. Sehemu kubwa ya Mikopo iliyotolewa ilitumika
kugharamia shughuli za Kilimo ikijumuisha ununuzi wa Pembejeo na Zana za
Kisasa za Kilimo na Umwagiliaji.
33. Mheshimiwa Spika, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), katika mwaka 2011/2012, Miradi 878 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 18.6
iliyoibuliwa na Wananchi kwenye Halmashauri zote Tanzania Bara na
Zanzibar ilitekelezwa. Vilevile, hadi kufikia Desemba 2011, Mfuko huo
umetoa Shilingi Bilioni 1.14 kwa Walengwa 14,000 kupitia Utaratibu wa Uhawilishaji Fedha katika Kaya Maskini. Aidha, Mafunzo ya Ujasiriamali yametolewa kwa Vikundi 500 Nchini katika Wilaya za Tanzania Bara na Zanzibar. Vilevile, Wajumbe 8,780 wa Kamati za Usimamizi wa Mradi na 13,500 wa Kamati za Serikali za Vijiji na Mitaa walipata mafunzo.
34. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha 2012/2013, Serikali itaanza utekelezaji wa Awamu ya Tatu
ya TASAF. Benki ya Dunia imepitisha Shilingi Bilioni 345.4 kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango huo utakaotekelezwa kwa kipindi cha Miaka Mitatu. Serikali pia itasimamia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili Wajasiriamali wengi zaidi wanufaike.
Aidha, Serikali itawahamasisha Wananchi kuweka akiba, kuwekeza na
kutambua na kutumia fursa za kiuchumi zilizopo ili kuongeza kipato na
ajira.
SEKTA ZA UZALISHAJI
Kilimo
35. Mheshimiwa Spika,
Serikali inatambua kuwa mkakati wa kuhimiza Kilimo cha Kisasa
kinachotumia Kanuni Bora za Kilimo, Zana za Kisasa na msukumo kwenye
Kilimo cha Umwagiliaji ndiyo njia ya uhakika ya kuongeza uzalishaji na
tija katika kilimo. Aidha, ushirikiano baina ya Serikali na Sekta
Binafsi ni nguzo muhimu ya kuleta Mapinduzi ya Kilimo. Jitihada za
Serikali katika mwaka 2011/2012 zilielekezwa katika vipaumbele hivyo
pamoja na kuongeza upatikanaji na matumizi ya Pembejeo na Zana Bora za
Kilimo.
Pembejeo na Zana za Kilimo
36. Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha mwaka 2011/2012, Serikali iliimarisha upatikanaji wa
Pembejeo za Kilimo hasa Mbolea, Mbegu Bora na Madawa ya Mimea. Jumla ya
Vocha Milioni 5.3 za Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo zilisambazwa kwa Kaya Milioni 2 Nchini. Lengo la Serikali ni kuongeza upatikanaji wa Pembejeo ili kuwanufaisha Wakulima wengi waweze kuongeza tija, uzalishaji na kipato. Kama
nilivyoahidi kwenye Hotuba yangu ya mwaka 2011/2012, tayari Serikali
imefanya ukaguzi maalum kuhusu utoaji wa Ruzuku za Pembejeo kwenye
Kilimo kwa utaratibu wa Vocha. Kutokana na matokeo ya awali ya ukaguzi
huo, TAKUKURU imefungua Kesi 19 kwa wale waliobainika kufanya
Ubadhirifu na Udanganyifu katika utoaji wa Vocha za Pembejeo za Kilimo.
Pamoja na hatua hiyo, Serikali itaboresha mfumo wa sasa wa utoaji wa
Vocha za Pembejeo kwa kubuni Mfumo mwingine ambao utaondoa upungufu
uliojitokeza katika mfumo unaotumika hivi sasa. Lengo ni kuhakikisha
kwamba Vocha zinawafikia walengwa kwa wakati na zinatumika kwa madhumuni
yaliyopangwa.
37. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba, Serikali kupitia SUMA JKT iliingiza Nchini Matrekta Makubwa 1,860 na Zana zake; Matrekta Madogo ya Mkono 400 na Pampu za Umwagiliaji 1,100
kupitia Mkopo wenye Masharti Nafuu kutoka Serikali ya India. Ili
kuwawezesha Wakulima wengi zaidi kumudu bei ya Matrekta hayo, Serikali
imeamua kupunguza bei ya Matrekta hayo kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, bei
ya Trekta Moja la Horse Power 50 imepunguzwa kutoka Shilingi Milioni 25.6 hadi Milioni 16.5 na Trekta la Horse Power 70 imepunguzwa kutoka Shilingi Milioni 45.8 hadi Milioni 38.8. Natoa wito kwa Halmashauri, Vyama vya Ushirika, Vikundi vya Wakulima na Wananchi kutumia fursa hii kununua Matrekta hayo. Aidha,
jana baada ya kushauriana na Halmashauri husika tuliafikiana kuwa
Halmashauri ziangalie uwezekano wa kuwapunguzia zaidi Wakulima kiwango
cha Asilimia 30 wanachotakiwa kuchangia katika ununuzi wa Matrekta ya
SUMA JKT ili waweze kupata Matrekta hayo kwa bei nafuu zaidi. Lengo ni
kuhakikisha kuwa Matrekta hayo yanawafikia Wakulima wengi.
Umwagiliaji
38. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imekarabati Miundombinu ya Skimu 32 za umwagiliaji zenye ukubwa wa Hekta 17,824. Aidha, kazi ya ujenzi wa Mabwawa 8 ya Maji inaendelea na Upembuzi Yakinifu wa Miradi 25 ya Umwagiliaji yenye eneo la Hekta 17,113 umefanyika. Kutokana na juhudi hizo, eneo la umwagiliaji Nchini limeongezeka kutoka Hekta 331,490 mwaka 2010/2011, hadi Hekta 345,690 mwaka 2011/2012. Katika mwaka 2012/2013, Serikali itashirikiana na Wadau wa Maendeleo kuwawezesha Wakulima 33,108 katika Skimu 20 za Umwagiliaji zenye Hekta 15,431 kulima zao la Mpunga kibiashara kwa kutumia Teknolojia za Kisasa.
Mifugo
39. Mheshimiwa Spika, Ilani
ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010 ilielekeza Serikali
iandae Programu Kabambe ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo ambayo itajumuisha
uendelezaji wa Malisho, kuchimba na kujenga Malambo, Mabwawa na Majosho
na huduma za Ugani ili hatimaye Wafugaji waondokane na ufugaji wa
kuhamahama. Katika kutekeleza maelekezo hayo, Serikali kwa kushirikiana
na Wadau wa Sekta ya Mifugo imeandaa Programu ya Kuendeleza Sekta ya
Mifugo.
Kukamilika kwa Programu hii kutaiwezesha Sekta ya Mifugo kutoa mchango
zaidi kwenye Pato la Taifa na kuwanufaisha Wafugaji. Mafanikio ya
Programu hii yatategemea sana Wadau wa Sekta ya Mifugo kuzingatia Sheria
Na. 13 ya Mwaka 2011 iliyopitishwa na Bunge lako inayohusu
Maeneo ya Malisho na Rasilimali ya Vyakula vya Mifugo. Nawahakikishia
Wananchi kwamba Serikali itasimamia kikamilifu utekelezaji wa Sheria hii
pamoja na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo, ili kuleta mabadiliko
kutoka kwenye Uchungaji kwenda kwenye Ufugaji wa Kisasa.
40. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imetoa Ruzuku ya Shilingi Bilioni 1.6 zilizotumika kununua na kusambaza lita 62,500 za Dawa za Kuogesha Mifugo na Dozi Milioni 3.5 za Chanjo ya Ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya Ng’ombe katika Halmashauri zote Nchini. Serikali pia imeendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali kujenga na kukarabati Majosho 108 na Malambo 98.
Aidha, Kituo cha Taifa cha Uhamilishaji kilichopo Usa River, Arusha
pamoja na Vituo Vitano vya Kanda vya Afya ya Mifugo vimeimarishwa. Serikali itaendelea kutoa Ruzuku ya Dawa za Mifugo na kuhamasisha Wafugaji na Wafanyabiashara kuwekeza zaidi kwenye Ufugaji wa Kisasa na unenepeshaji Mifugo.
Uvuvi
41. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2011/2012, Serikali ilianza kutekeleza Mkakati wa
Uendelezaji Ukuzaji Viumbe kwenye Maji kwa kuimarisha Ufugaji Samaki na
ukuzaji wa Viumbe vingine. Utekelezaji wa Mkakati huo, umeongeza idadi
ya Mabwawa ya Kufugia Samaki kutoka 19,039 mwaka 2010/2011 hadi 19,443 mwaka 2011/2012, na Vituo vya Kuzalisha Vifaranga vimeongezeka kutoka 8 hadi 10 ambapo jumla ya Vifaranga Milioni 1.9
vya Samaki vimezalishwa na kusambazwa kwa Wadau. Aidha, elimu ya
usimamizi na matumizi endelevu ya Rasilimali za Uvuvi imetolewa katika
maeneo ya Wavuvi. Vikundi 188 vilihamasishwa kufanya shughuli mbadala kwa kupatiwa elimu ya ujasiriamali ambapo Miradi Midogo 459 ya kiuchumi imeanzishwa. Katika mwaka 2012/2013, Serikali itafanya Mapitio ya Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka 1997 na kuandaa Mkakati wa utekelezaji.
Ufugaji Nyuki
42. Mheshimiwa Spika,
Sekta ya Ufugaji Nyuki ina mchango mkubwa katika kuondoa Umaskini na
kuhifadhi mazingira. Kwa kuzingatia fursa kubwa tuliyonayo ya Rasilimali
za Ufugaji Nyuki, Serikali imeziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa zote
Nchini kuanzisha Mashamba Darasa ya kutoa Elimu ya Ufugaji Nyuki.
Katika mwaka 2011/2012, jumla ya Wafugaji Nyuki 4,573 kutoka Wilaya 33
walipewa mafunzo ya Ufugaji Bora wa Nyuki. Aidha, Wakuu wa Mikoa na
Wakuu wa Wilaya wamepewa mafunzo kuhusu Ufugaji Bora wa Nyuki ili waweze
kuwa chachu ya uhamasishaji katika Mikoa na Wilaya kuhusu manufaa ya
Ufugaji Nyuki. Kutokana na jitihada hizo, katika mwaka 2011/2012,
uzalishaji wa Asali ulifikia Tani 9,000 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 27 na Nta iliyozalishwa ilikuwa Tani 600 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 3.
Aidha, tarehe 9 Juni, 2012 nilipata fursa ya kufungua Kiwanda kipya na
cha Kisasa cha Kuchakata Asali kilichojengwa na Kampuni ya Honey King Limited katika Kijiji cha Visiga Mkoani Pwani na hivyo kufanya jumla ya Viwanda vya kuchakata na kufungasha Asali Nchini kufikia Vinane. Napenda kuwapongeza Wawekezaji hao kwa kujenga Kiwanda chenye uwezo wa Kuchakata Tani 10,000
za Asali kwa mwaka. Nawaomba Wafugaji Nyuki kuitumia vizuri fursa hii
kwa kuzalisha Mazao ya Nyuki kwa wingi na yenye ubora ili kunufaika na
Soko la kuaminika la Kiwanda hicho na vingine vilivyopo hapa Nchini.
43. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2012/2013, Serikali itaendelea kutoa elimu ya Ufugaji
Nyuki kwa Wadau mbalimbali. Aidha, ili kutangaza Ubora wa Asali na Nta
ya Nchi yetu, yatafanyika Maonyesho Maalum ya Mazao ya Ufugaji
Nyuki mwezi Oktoba 2012. Maonyesho hayo yataandaliwa kwa ushirikiano
baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Viwanda na Biashara,
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania na Wadau wengine.
Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani Mazao na Huduma za Kifedha Vijijini
44. Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza utekelezaji wa Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani Mazao na Huduma za Kifedha Vijijini (Marketing Infrastructure Value Addition and Rural Finance Program - MIVARF)
mwezi Julai, 2011. Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kuandaa mfumo wa
utekelezaji ikiwemo uundaji wa Kamati za Usimamizi, ununuzi wa Vitendea
Kazi, kuajiri wafanyakazi na kuitambulisha Programu katika Mikoa yote.
Aidha, uchambuzi wa Maandiko ya Miradi iliyopokelewa kutoka Halmashauri
mbalimbali umefanyika na Halmashauri zitakazoanza kushiriki katika
utekekezaji wa Programu zimechaguliwa.
45. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Kilometa 250
za barabara za vjijini zitakarabatiwa, maghala mawili yatajengwa na
manne yatakarabatiwa. Vilevile, vituo vinne vya mafunzo ya uongezaji
thamani mazao vitakarabatiwa; Wakulima watapatiwa mafunzo kuhusu hifadhi
ya mazao, mbinu za kuyafikia masoko na Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao
Ghalani. Kazi nyingine zitakazofanyika ni kuviendeleza Vikundi 864 vya Kifedha vikiwemo VICOBA, kuzijengea uwezo SACCOS 108 pamoja na Asasi nyingine ndogo za Kifedha ili ziweze kutoa Huduma za Kifedha Vijijini kwa ufanisi zaidi.
Viwanda
46. Mheshimiwa Spika,
Serikali inatambua mchango na umuhimu wa Sekta ya Viwanda katika kuleta
maendeleo endelevu, kuongeza ajira, kuongeza thamani ya Mazao, Kukuza
Masoko, kuongeza Mapato ya Serikali na fedha za kigeni. Kwa kuzingatia
umuhimu huo, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na uhamasishaji wa
Uwekezaji wa Viwanda Vipya katika Maeneo Maalum ya Uzalishaji (EPZ) na
Maeneo Maalum ya Uchumi (SEZ). Idadi ya Makampuni yaliyosajiliwa katika
maeneo hayo imeongezeka kutoka 44 mwaka 2010/2011 hadi 54 mwaka 2011/2012. Uwekezaji wa Mitaji umeongezeka kutoka Shilingi Trilioni 1.02 hadi Trilioni 1.1. Pia, mauzo ya Nje yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 560.5 hadi Bilioni 706.5 na Ajira zimeongezeka kutoka 13,500 hadi 15,100.
47. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali itaimarisha Sekta ya Viwanda kwa kuhimiza uwekezaji katika Viwanda
vya kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za kilimo na kuwaunganisha
Wakulima na wenye Viwanda ili kuwawezesha kupata Soko la uhakika.
Aidha, itaendelea kuweka umuhimu katika utekelezaji wa miradi ya Makaa
ya Mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga.
Madini
48. Mheshimiwa Spika, Serikali
imechukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha Sekta ya Madini ili
Taifa linufaike zaidi na Rasilimali hiyo. Hatua hizo ni pamoja na
kuimarisha Shirika la Madini la Taifa - STAMICO ili liweze kuchukua Hisa
kwa niaba ya Serikali katika Migodi Mipya inayotarajiwa kuanzishwa.
Kupitia utaratibu huo, STAMICO inamiliki Asilimia 45 ya hisa katika Mgodi wa Backreef na Asilimia 55 zinamilikiwa na Mwekezaji. Hatua nyingine ni kuwawezesha Wachimbaji Wadogo kuanzisha Vituo
vya kuwasaidia kukopeshwa na kununua Vifaa vya Kisasa vya kuchimbia
Madini katika maeneo ya Rwamgasa - Geita, Londoni – Manyoni na Pongwe –
Bagamoyo. Aidha, kupitia
Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini, shughuli za Ukaguzi katika Migodi
mikubwa zimeimarishwa na sasa Migodi mingi imeanza kulipa Kodi ya
Mapato.
49. Mheshimiwa Spika, Serikali pia imechukua hatua madhubuti kuhakikisha kwamba Makampuni yote Makubwa ya Madini yanalipa mrabaha wa Asilimia Nne (4) kwa kuzingatia matakwa ya Sheria Mpya ya Madini Na. 14 ya mwaka 2010. Makampuni
ya madini ambayo hayajazingatia matakwa haya ya Kisheria yametakiwa
kulipa malimbikizo yote tangu Sheria hiyo ilipopitishwa mwaka 2010. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, hakuna Kampuni ya Madini ambayo itakwepa kulipa Mrabaha kwa Kiwango kipya na Kodi zote kama
inavyotakiwa. Tutakuwa makini kuhakikisha kwamba Sheria na Taratibu za
Biashara ya Madini na Hifadhi ya Mazingira zinafuatwa na kila Mmiliki wa
Mgodi. Napenda
kutoa wito kwa Wachimbaji Wadogo, jamii inayozunguka Migodi Mikubwa
pamoja na wamiliki wa Migodi mikubwa kushirikiana kwa karibu na kila
mmoja atimize wajibu wake ili kuleta mahusiano mazuri na kuepusha
migogoro isiyokuwa ya lazima.
Utalii
50. Mheshimiwa Spika, kutokana na juhudi zinazoendelea za kutangaza Vivutio mbalimbali vya Utalii, idadi ya Watalii imeongezeka kutoka 782,699 mwaka 2010 hadi 867,994 mwaka 2011, sawa na ongezeko la Asilimia 11. Mapato yatokanayo na Utalii yameliingizia Taifa Shilingi Trilioni 2.14 mwaka 2011 ikilinganishwa na Shilingi Trilioni 1.96 mwaka 2010. Serikali pia, imeandaa Programu ya Kutunza na Kuweka Kumbukumbu za Urithi wa Malikale ili kupanua wigo wa Vivutio vya Utalii. Hatua hii itaiwezesha Tanzania kutangaza zaidi maeneo ya urithi wa Utamaduni wetu pamoja na Maeneo 22 ya Wapigania Uhuru kwa ajili ya Ukombozi wa Bara la Afrika. Katika
mwaka 2012/2013, Serikali itaongeza kasi zaidi ya kutangaza Vivutio vya
Utalii wetu nje ya Nchi, kwa kutumia Balozi zetu pamoja na Tovuti;
kuwavutia Wawekezaji wa Nje na Ndani katika Sekta ya Utalii na
kuhamasisha Utalii wa Ndani.
AJIRA
51. Mheshimiwa Spika, Vijana ndiyo sehemu kubwa ya nguvu kazi katika Nchi yetu. Inakadiriwa kuwa Asilimia 35 ya Watanzania wote ni Vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35. Aidha, Vijana ni Asilimia 68
ya Watanzania wote wenye nguvu na uwezo wa kufanya kazi. Jitihada kubwa
za Serikali zinaendelea kuwekwa katika kutoa msukumo kwenye uwekezaji
katika sekta zenye fursa kubwa ya kutoa ajira nyingi kama vile
kilimo, mifugo, uvuvi, ufugaji nyuki, ujenzi, mawasiliano, uchukuzi,
utalii na viwanda. Aidha, ili kuwawezesha Vijana kupata mitaji, Serikali
imeongeza mtaji kwa Benki ya Rasilimali, Benki ya Wanawake, Benki ya
Posta pamoja na Mifuko mbalimbali ya Uwezeshaji wananchi Kiuchumi.
Vilevile, Mafunzo ya Ujasiriamali na Elimu ya Ufundi Stadi kwa Vijana
waishio Mijini na Vijijini yataimarishwa kwa lengo la kuwaongezea sifa
katika Soko la Ajira, hasa Sekta Binafsi.
52. Mheshimiwa Spika, ufumbuzi
wa uhakika wa tatizo la Ajira hususan kwa Vijana utatokana na jitihada
za makusudi za kuongeza uwekezaji katika sekta zote. Napenda kutoa rai
kwa Viongozi na Watendaji wote kwenye ngazi ya Taifa, Mikoa, Wilaya na
Mamlaka za Serikali za Mitaa; kuhakikisha kwamba wanaongeza jitihada za
kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji na kuongeza kasi
ya ukuaji wa Sekta Binafsi.
HUDUMA ZA KIUCHUMI
Ardhi
53. Mheshimiwa Spika, Ardhi
ni Rasilimali muhimu katika Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini. Hata
hivyo, ili kunufaika na Rasilimali hiyo, ni muhimu Ardhi ipimwe na kuwa
na Mpango endelevu wa matumizi bora ya Ardhi. Kwa kuzingatia umuhimu
huo, hadi kufikia Aprili 2012, mipaka ya Vijiji 11,261 ilipimwa. Vyeti vya Ardhi ya Vijiji 3,283 vilitolewa, upimaji wa Viwanja 26,788 na Mashamba 706 ulifanyika na Hati za Hakimiliki za Kimila 46,063 zilitolewa na kufanya jumla ya Hati za Hakimiliki za Kimila zilizokwishatolewa Nchini kote kufikia 157,968.
54. Mheshimiwa Spika,
ili kuwawezesha Wananchi kunufaika na Rasilimali Ardhi wanayomiliki,
Serikali itakamilisha Mradi wa Kuweka Kituo cha Kupokea Picha za Satellite (Direct Satellite Imagery Receiving Station).
Kituo hicho kitawawezesha Wananchi kupimiwa ardhi yao na kupatiwa hati
kwa vile upimaji na utayarishaji wa ramani kwa ardhi yote Nchini utakuwa
umerahisishwa kwa kiasi kikubwa. Huu utakuwa ukombozi wa kiuchumi kwa
Watanzania.
55. Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha kujenga Mtandao Mpya wa Alama za Msingi za Upimaji Ardhi Nchini (National Geodetic Control Unit).
Alama hizo zinatarajiwa kuanza kutumika mwezi Julai, 2012. Mtandao wa
Alama hizo, utarahisisha Upimaji wa Ardhi kwa matumizi mbalimbali na
kupunguza gharama za upimaji Nchini.
Nishati
56. Mheshimiwa Spika,
mwezi Agosti 2011, Serikali iliwasilisha Bungeni Mpango wa Dharura wa
Kuondoa Mgao wa Umeme uliokuwepo Nchini. Mgao huo ulisababishwa kwa
kiasi kikubwa na kupungua kwa uzalishaji hasa kwenye Vyanzo vya Umeme
vya Maji. Kutokana na utekelezaji wa Mpango wa Dharura wa Umeme hadi
kufikia mwezi Aprili 2012, jumla ya Megawati 342 zimezalishwa na
kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa. Uzalishaji huo umeimarisha hali ya
upatikanaji Umeme na hivyo Makali ya Mgao kupungua. Hata hivyo,
uzalishaji wa Umeme wa Dharura ni wa gharama kubwa kutokana na Mitambo
mingi kuendeshwa kwa kutumia Mafuta ya Dizeli.
57. Mheshimiwa Spika,
hatuwezi kuendelea na hali hii ya uzalishaji umeme kwa gharama kubwa
huku tukiwa na Rasilimali zinazoweza kubadili kabisa hali hiyo. Kwa
hiyo, Serikali imeanza kutekeleza Mradi mkubwa wa ujenzi wa Bomba la
Gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza kiasi cha
Gesi itakayotumika kuendesha Mitambo ya Uzalishaji Umeme. Tayari fedha
za kutekeleza mradi huu zimepatikana na ujenzi unatarajiwa kuanza mwaka
2012/2013. Serikali pia katika mwaka 2011/2012 imetoa Shilingi Bilioni 39 ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika ujenzi wa Mradi huo. Fedha nyingine kiasi cha Shilingi Bilioni 110 zimewekwa katika Bajeti ya 2012/2013.
58. Mheshimiwa Spika,
hatua nyingine ambayo Serikali imechukua kutatua tatizo la Umeme Nchini
ni kuongeza ushiriki wa Sekta Binafsi katika uzalishaji na usafirishaji
wa umeme. Kwa kuanzia, Serikali inashirikiana na Serikali ya Marekani
kubaini vikwazo vinavyozuia Sekta Binafsi kuwekeza kwenye Miradi mikubwa
ya Umeme. Kazi hiyo itafuatiwa na utekelezaji wa Mpango Maalum wa
Pamoja wa Miaka Mitano utakaoanza kutekelezwa mwaka 2012/2013. Lengo ni
Kuzalisha Umeme wa MW 2,700 ifikapo mwaka 2016.
59. Mheshimiwa Spika, Wakala wa Umeme Vijijini unatekeleza Programu Kabambe ya Kusambaza Umeme Vijijini katika Mikoa 16.
Mikoa hiyo ni Kigoma, Kagera, Mwanza, Mara, Shinyanga, Arusha,
Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Mbeya,
Rukwa na Tabora. Chini ya Programu hiyo, Miradi Midogo 41 inatekelezwa ambapo Wateja 22,000
watalipiwa gharama za kuunganisha Umeme kupitia Mfuko wa Nishati
Vijijini. Programu hiyo itawawezesha Wananchi wengi zaidi Vijijini
kupata Nishati ya Umeme ili kuharakisha maendeleo katika maeneo hayo.
60. Mheshimiwa Spika, kutokana
na jitihada za Serikali za kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Nishati,
kasi ya utafutaji na ugunduzi wa hazina mpya ya Gesi Asili Nchini
imeongezeka. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, hivi karibuni
Makampuni yanayofanya utafiti wa Gesi Asili Nchini yamegundua kiasi
kikubwa cha Gesi Asili yenye futi za ujazo Trilioni 3. Gesi hiyo imegundulika kwenye kina cha maji marefu baharini takriban Kilometa 80
kutoka Nchi kavu Mashariki mwa Mkoa wa Lindi. Ugunduzi huo unafanya
kiasi cha Gesi kilichogundulika hadi sasa kwenye kina cha maji marefu
baharini kufikia futi za ujazo Trilioni 20.97. Kwa kuzingatia
fursa zinazotokana na kasi kubwa ya ukuaji wa Sekta ya Gesi Nchini,
Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba Taifa linanufaika kikamilifu na
ugunduzi wa rasilimali hiyo. Serikali inaandaa Sera na Sheria Mahsusi ya
Gesi Asili pamoja na Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi kwa lengo la
kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa sekta hiyo. Aidha, Serikali
itawawezesha Vijana wetu kupata Mafunzo Maalum (Specialized Training)
yanayohusiana na masuala ya Gesi Asili kwa lengo la kupata Wataalam
Wazalendo waliobobea kwenye sekta hii kama ilivyoainishwa kwenye Mpango
wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
61. Mheshimiwa Spika,
Nchi zote Duniani zimeazimia kubadili Teknolojia ya Utangazaji kutoka
Analojia kwenda Dijitali ambayo imeonekana kuwa na tija na yenye
kutumiwa na Vifaa vingi zaidi vya Mawasiliano. Kwa kuzingatia azimio hilo, Nchi za Jumuiya
ya Afrika Mashariki nazo zimekubaliana kutekeleza mabadiliko hayo na
kuanza Kurusha Matangazo katika Mfumo wa Dijitali pekee ifikapo tarehe
31 Desemba 2012. Ili Watanzania wawe tayari kuyapokea mabadiliko hayo, Serikali imeandaa mpango wa kuelimisha Umma unaojulikana kwa jina la “Digital Tanzania” ambao ulizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwezi Agosti 2011. Wananchi wote watambue kwamba mabadiliko ya Teknolojia za Utangazaji kutoka Analojia kwenda Dijitali ni matokeo ya ukuaji wa kasi wa Teknolojia ya Mawasiliano ambao hatuwezi kuuepuka.
62. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Awamu ya Pili ya Ujenzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa wenye urefu wa Kilomita 3,000
umekamilika na kuanza kutumika. Kukamilika kwa Awamu hii kunafanya Nchi
yetu kuwa na Mkongo uliojengwa wenye jumla ya Kilometa 7,300
na kumeiwezesha Mikoa yote ya Tanzania Bara kuunganishwa kwenye Mkongo
huo. Aidha, Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa umeunganishwa na Kisiwa cha
Pemba kupitia Tanga. Katika mwaka 2012/2013, Kisiwa cha Unguja
kitaunganishwa na Mkongo huo kupitia Dar es Salaam, baada ya kukamilika
kwa ujenzi wa Mkongo wa Majini.
Barabara na Madaraja
63. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2011/2012, Serikali imeendelea kujenga, kukarabati na
kuzifanyia matengenezo Barabara Kuu, za Mikoa na Wilaya ili ziweze
kupitika wakati wote. Hadi mwezi Mei 2012, Serikali imejenga jumla ya
Kilometa 305.6 za Barabara Kuu na Kilometa 29.5 za Barabara za Mikoa kwa kiwango cha Lami. Pia, imefanya ukarabati mkubwa wa Kilometa 78.4 za Barabara Kuu kwa kiwango cha Lami na Kilometa 463.2 kwa kiwango cha Changarawe katika Barabara za Mikoa. Aidha, jumla ya Kilometa 7,209
za Barabara za Mamlaka ya Serikali za Mitaa zimefanyiwa matengenezo ya
kawaida. Vilevile, ujenzi wa Daraja la Nangoo lililopo Mtwara na Daraja
la Malagarasi Mkoani Kigoma umeanza.
64. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali imepanga kujenga Kilometa 414 na kukarabati Kilometa 135 kwa kiwango cha Lami pamoja na kujenga Madaraja 11 katika Barabara Kuu. Vilevile, itajenga Kilometa 573 kwa kiwango cha Changarawe na Kilometa 32 kiwango cha Lami katika Barabara za Mikoa pamoja na Madaraja 27. Katika kipindi hicho, Mfuko wa Barabara unatarajiwa kuingiza zaidi ya Shilingi Bilioni 400
ambazo zitatumika kwa ajili ya matengenezo, ujenzi na usimamizi wa
Miradi mbalimbali ya Barabara, zinazosimamiwa na TANROADS na Mamlaka za
Serikali za Mitaa.
Bandari
65. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2011/2012, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu na kuongeza
ufanisi wa utoaji huduma katika Bandari Kuu za Dar es Salaam, Tanga na
Mtwara pamoja na kukarabati Bandari za Kigoma na Mwanza. Aidha,
imekamilisha Upembuzi Yakinifu wa ujenzi wa Bandari Mpya ya Mbegani
(Bagamoyo) na Mwambani Tanga.
Reli
66. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2011/2012, Serikali iliweka Menejimenti Mpya ya Shirika la Reli
(TRL) inayoongozwa na Wazalendo. Serikali pia ilitoa fedha za kukarabati
Miundombinu chakavu ya Reli ya Kati ikiwa ni pamoja na ukarabati wa
Injini za Treni na Mabehewa ya Abiria. Aidha, kazi ya usanifu wa kina kwa ajili ya kuijenga Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge) na kuiunganisha na Nchi za Rwanda na Burundi imeanza mwezi Februari 2012 na inatarajiwa kukamilika Mwaka 2013.
67. Mheshimiwa Spika, Serikali za Tanzania, Zambia na Jamhuri ya Watu wa China mwezi Machi 2012, zimesaini Mikataba yenye Thamani ya Shilingi Bilioni 66.67 kwa ajili ya kuboresha Miundombinu na huduma za TAZARA. Mikataba hiyo itatekelezwa kuanzia mwaka 2012/2013. Jitihada hizo zitawezesha huduma za Reli kuimarika na hivyo kutoa mchango mkubwa katika uchumi wetu.
HUDUMA ZA JAMII
Elimu
Elimu ya Msingi
68. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali
imeanza kufanya Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 1995 kwa
lengo la kuiboresha ili kuendana na Mazingira ya sasa. Kazi hiyo
inatarajiwa kukamilika Mwaka 2012/2013. Aidha, Serikali iliendelea na
Utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi
ambapo jumla ya Madarasa 485 na Nyumba za Walimu 344 zilijengwa na Madawati 61,363 yalinunuliwa. Katika kipindi hicho, jumla ya Walimu 11,243 waliajiriwa na 2,259 walipewa
mafunzo kazini ili kuongeza ubora wa ufundishaji wa Masomo ya Sayansi,
Hisabati na Kiingereza. Lengo ni kuwajengea Walimu uwezo wa kufundisha
na hatimaye kuongeza kiwango cha Ufaulu wa Wanafunzi katika masomo hayo.
Elimu ya Sekondari
69. Mheshimiwa Spika, katika
Mwaka 2011/2012, utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Elimu ya
Sekondari (MMES II) umekuwa na mafanikio ya kuridhisha. Jumla ya
Madarasa 1,316, Maabara 127 na Nyumba za Walimu 270 zilijengwa na Madawati 123,855 yalinunuliwa. Katika kipindi hicho, jumla ya Walimu wa Sekondari 13,900 wameajiriwa na Vitabu Milioni 1.5
vilinunuliwa na kusambazwa katika Shule mbalimbali za Sekondari.
Wanafunzi waliojiunga na Kidato cha Kwanza waliongezeka kutoka 456,350 Mwaka 2011 hadi 517,993 Mwaka 2012. Hili ni ongezeko la Wanafunzi 61,643.
70. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali
itaendelea kuimarisha Miundombinu ya Shule za Sekondari ili kuboresha
mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Jitihada zitaongezwa katika
kuhamasisha ujenzi wa Madarasa zaidi kwa ajili ya Wanafunzi wanaojiunga
na Kidato cha Tano na Sita kukidhi mahitaji makubwa yaliyojitokeza baada
ya kupanuliwa kwa Elimu ya Sekondari Nchini.
Mafunzo ya Ufundi Stadi
71. Mheshimiwa Spika, Mafunzo
ya Ufundi Stadi yana mchango mkubwa katika kuwapatia ujuzi na
kuwajengea uwezo Wanafunzi wanaohitimu Elimu ya Msingi na Sekondari.
Katika mwaka 2011/2012, Serikali imekamilisha ujenzi wa Vyuo vya
Mafunzo ya Ufundi Stadi katika Mikoa ya Lindi, Pwani, Manyara, Arusha
na Dar es Salaam. Kukamilika kwa Vyuo hivyo kumeongeza idadi ya
Wanafunzi wanaojiunga na Vyuo vya Ufundi kutoka 72,938 mwaka 2010 hadi 102,217 mwaka 2011. Katika Mwaka 2012/2013, Serikali itapanua zaidi Mafunzo ya Ufundi Stadi Nchini.
Elimu ya Juu
72. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2011/2012, Serikali ilitekeleza Mpango wake wa kuimarisha
Miundombinu ya Vyuo Vikuu na Vyuo vya Elimu ya Juu Nchini. Kutokana na
hatua hiyo, Udahili wa Wanachuo katika Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu
Vishiriki uliongezeka kutoka Wanachuo 40,993 mwaka 2005/2006 hadi 139,638
mwaka 2010/2011. Idadi ya Wanachuo waliopewa mikopo ya elimu ya juu
ikijumuisha Wanachuo wa Vyuo Vikuu na Vyuo vingine iliongezeka kutoka 42,729 mwaka 2005/2006 hadi 93,784
mwezi Aprili 2012. Aidha, katika kipindi hicho, fedha zilizokopeshwa
Wanachuo hao ziliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 56.1 hadi Bilioni
291. Katika Mwaka 2012/2013, Serikali itatoa kipaumbele katika
kuongeza ubora wa Elimu ya Juu ili kuendana na mahitaji ya Soko la Ajira
Nchini na katika Jumuiya ya Afrika Mshariki.
Afya
73. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2011/2012, Serikali imetekeleza Mpango wa kugawa Vyandarua vyenye
Dawa ili kupunguza Maambukizi ya Ugonjwa wa Malaria. Hadi Desemba 2011
jumla ya Vyandarua Milioni 17.6 viligawanywa bila malipo kwa
kila Kaya yenye Watoto wenye umri chini ya Miaka Mitano Nchi nzima.
Sambamba na hatua hiyo, Mpango wa Kunyunyizia Dawa ya Ukoko aina ya ICON
kwenye kuta za Nyumba ili kuua mbu ulitekelezwa katika Wilaya 18
za Mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara ambayo imeonekana kuwa na Maambukizi
makubwa ya Malaria. Aidha, jitihada za kuongeza upatikanaji wa Dawa
Mseto za kutibu Malaria kwa bei yenye punguzo zinaendelea. Jitihada za
udhibiti wa malaria zimechangia kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka vifo 99 kwa kila watoto 1,000 mwaka 1999 hadi vifo 51 kwa kila watoto 1,000 mwaka 2010. Vilevile, vifo vya watoto wa umri chini ya miaka mitano vimepungua kutoka vifo 147 kwa kila watoto 1,000 mwaka 1999 hadi vifo 81 kwa kila Watoto 1,000 mwaka 2010.
74. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2012/2013, Serikali itaendelea na utekelezaji wa Mpango wa
Kuangamiza Viluwiluwi vya Mbu kwa kutumia njia za Kibaiolojia kwa
ushirikiano na Serikali ya Cuba. Mpango huo ulianza mwaka 2011 kwa
majaribio katika Jiji la Dar es Salaam. Aidha, Serikali itaandaa Mkakati
Maalum wa kugawa Vyandarua kupitia Shuleni ili kuhakikisha kuwa
matumizi ya Vyandarua yanakuwa endelevu. Natoa wito kwa Wananchi wote
kutumia Vyandarua vinavyotolewa na Serikali kwa lengo lililokusudiwa
badala ya matumizi mengine. Vilevile, nawahimiza kutokomeza Mazalia
ya Mbu na kuweka Mazingira katika hali ya Usafi ili tufanikiwe kuondoa
Ugonjwa wa Malaria Nchini.
75. Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kupunguza
idadi kubwa ya Wagonjwa wa Moyo wanaopoteza maisha kwa kukosa Tiba
Stahiki na gharama kubwa inayotumika kupata Tiba hiyo nje ya Nchi. Ili
kutekeleza dhamira hiyo, katika mwaka 2011/2012, Serikali kwa
kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imekamilisha ujenzi
wa Kituo cha Kisasa cha Upasuaji, Tiba na Mafunzo ya Ugonjwa wa Moyo
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Pamoja na mafanikio hayo,
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili iliendelea kutoa huduma za Upasuaji
Mkubwa wa Moyo ambapo hadi mwezi Aprili, 2012 jumla ya Wagonjwa 300 walipata huduma hiyo na hivyo kuokoa zaidi ya Shilingi Bilioni Sita (6)
ambazo zingetumika kuwapeleka Wagonjwa hao Nje ya Nchi. Napenda
kuwapongeza Madaktari na Wahudumu wote wa Afya kwa huduma nzuri
wanayotoa kwa wagonjwa. Nawasihi kuendelea na moyo huo, kwani wamepewa dhamana kubwa ya kuwahudumia wananchi kutokana na ujuzi na weledi walionao.
Huduma kwa Watu wenye Ulemavu
76. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2011/2012, Serikali imekamilisha zoezi la kuandaa Kanuni za
utekelezaji wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu iliyopitishwa na Bunge mwaka
2010. Utekelezaji wa Sheria hiyo umeanza ambapo Watu wenye Ulemavu
wanapatiwa haki na huduma za msingi ikiwemo elimu, afya, ajira na
kulindwa Kisheria. Kwa Watu wenye Ulemavu wa Ngozi, Serikali kwa kiasi
kikubwa imedhibiti Vitendo vya Ukatili walivyokuwa wanafanyiwa.
Napenda kutumia fursa hii kutoa Wito kwa Wananchi wote kuwapenda na
kuwahudumia Walemavu wakiwemo Watu wenye Ulemavu wa Ngozi.
Lishe
77. Mheshimiwa Spika,
katika Hotuba yangu ya Bajeti ya mwaka 2011/2012, nililitaarifu Bunge
kuhusu hali isiyoridhisha ya Lishe hapa Nchini na hatua ambazo Serikali
imeanza kuzichukua kukabiliana na hali hiyo. Napenda kulifahamisha
Bunge lako kuwa, Mkakati wa Kitaifa wa Lishe ulizinduliwa
rasmi tarehe 20 Septemba, 2011. Mkakati huo umeainisha maeneo
ya kipaumbele ambayo yatatekelezwa katika kipindi cha Miaka Mitano ili
kupunguza idadi ya Watoto wenye Uzito Pungufu, Udumavu, pamoja na idadi
ya Wanawake Wajawazito wenye Upungufu wa Damu.
78. Mheshimiwa Spika, ili kuliongezea uzito suala la Lishe, Kamati
zitakazohakikisha kwamba Mkakati wa Lishe unatekelezeka kikamilifu
zimeanzishwa katika ngazi ya Taifa na Halmashauri. Napenda kutoa
msisitizo wa kipekee kwamba Lishe Bora ni muhimu kwa maendeleo ya Watu
na Taifa kwa ujumla. Lishe Duni ina Madhara makubwa hasa kwa
Watoto wadogo; Mtoto mdogo anapokosa Lishe Bora, maendeleo yake katika
masomo yana walakini mkubwa na hali hiyo haiwezi kurejeshwa tena.
Hivyo, Watendaji katika ngazi zote watoe umuhimu mkubwa kwenye suala la
Lishe Bora kwa kuendelea kutoa elimu ya Lishe Bora ili Wananchi
walielewe na wale chakula chenye Virutubisho muhimu ambavyo vipo kwenye
maeneo mengi Nchini.
Maji
79. Mheshimiwa Spika,
Serikali imeboresha huduma ya maji Vijijini kwa kujenga Miradi
mipya, kupanua na kukarabati iliyopo kwa kushirikisha Wananchi. Katika
mwaka 2011/2012, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya
Ujerumani (KfW) iliendelea na utekelezaji wa mradi wa maji katika Wilaya
za Moshi Vijijini na Hai. Vilevile, kwa kushirikiana na Serikali ya
Japan iliendelea kutekeleza mradi wa maji Vijijini katika Mikoa ya
Mwanza, Mara na Tabora. Aidha, Serikali imeendelea na juhudi zake za
kujenga mabwawa ya maji katika maeneo kame Nchini. Mabwawa yanayoendelea
kujengwa ni Kawa (Nkasi), Sasajila (Chamwino), Matwiga (Chunya),
Nyambori (Rorya), Wegero (Musoma), Habiya (Bariadi), Iguluba (Iringa),
Mwanjoro (Meatu) na Seke Ididi (Kishapu).
80. Mheshimwa Spika, Serikali pia, imeimarisha usimamizi na uendelezaji wa Rasilimali za Maji katika Mabonde yote Tisa (9)
ya Maji Nchini na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa Kutunza Vyanzo vya Maji
katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, Serikali imejenga Visima 946 katika Halmashauri 84.
81. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mijini, Serikali imejenga na kukarabati Mifumo ya Maji katika Miji Mikuu ya Mikoa 19. Kutokana na jitihada hizo, kiwango cha upatikanaji wa Maji kwa wakazi wa Miji hiyo kimeongezeka kutoka Asilimia 84 mwaka 2010 hadi kufikia Asilimia 86
mwaka 2011. Katika mwaka 2012/2013, Serikali itaendelea kuboresha
upatikanaji wa Maji Mijini kwa kuimarisha utendaji wa Mamlaka za Maji za
Miji Nchini. Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam, Serikali
itakamilisha upanuzi wa Mtambo wa Ruvu Chini na kuanza ujenzi wa Bomba
Jipya la Maji kutoka Ruvu Chini hadi kwenye Matenki ya Maji yaliyopo
maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, itakamilisha
Usanifu wa Mradi wa Kuchimba Visima Virefu katika maeneo ya Kimbiji na
Mpera na kuanza ujenzi wa Visima hivyo.
ULINZI NA USALAMA
82. Mheshimiwa Spika,
Majeshi yetu ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa yanafanya kazi nzuri
kuhakikisha kwamba hali ya Usalama wa Nchi na Mipaka yetu ni shwari.
Aidha, Majeshi yetu yameshiriki kikamilifu katika shughuli za kiraia
kusaidia Wananchi wakati wa Majanga hususan mafuriko, ajali na milipuko
ya magonjwa. Pamoja na kazi hizo, katika mwaka wa 2011/2012, Jeshi la Kujenga Taifa limekamilisha ukarabati wa Makambi 10 ya Jeshi la Kujenga Taifa yenye uwezo wa kuchukua Vijana 20,000 kwa wakati mmoja. Kwa mwaka 2012/2013, jumla ya Vijana 5,000 wataanza tena kujiunga na JKT kwa Mujibu wa Sheria.
83. Mheshimiwa Spika, katika kuitikia Wito wa kutekeleza Azma ya KILIMO KWANZA, mwaka 2011/2012, Jeshi la Kujenga Taifa limezalisha Tani 731.5 za mbegu bora zenye thamani ya Shilingi Milioni 544.4. Katika mwaka 2012/2013, Serikali itaendelea kuyawezesha Majeshi yetu kwa Vifaa na Zana za Kivita na upatikanaji wa mahitaji muhimu.
Serikali pia itaendelea kukarabati Makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa
kwa ajili ya kuchukua Vijana wengi zaidi na pia kujenga maghala salama
ya kuhifadhia silaha, mabomu na milipuko.
84. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa
Wabunge watakubaliana na mimi kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi
kubwa ya kudhibiti Matukio ya Uhalifu hapa Nchini. Mafanikio hayo
yamepatikana kutokana na ushirikiano mzuri kati ya Polisi na Wananchi
kupitia Mkakati wa Ulinzi Shirikishi. Moja ya Mbinu zinazotumika na
Jeshi hilo ni kuwashirikisha Wadau, hasa Viongozi wa Kijamii kama vile
Wazee wa Kimila, Madhehebu ya Dini, Vyama vya Hiari katika kuhamasisha
Wananchi kuzuia na kudhibiti Uhalifu Nchini. Mbinu nyingine ni kudhibiti
tatizo la kuzagaa kwa Silaha Ndogo Nchini kwa Kusajili na kuhamasisha
Wananchi kujitokeza kuwekewa Alama Maalum kwenye Silaha wanazomiliki.
Hadi kufikia mwezi Februari 2012, jumla ya Silaha Ndogo 1,250
zilisajiliwa. Natumia fursa hii kuvipongeza Vyombo vyetu vya Ulinzi na
Usalama kwa kazi nzuri wanayofanya kuhakikisha Nchi yetu inakuwa salama.
85. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo, tunayo changamoto ya Ajali
nyingi za Barabarani. Ajali hizo zimeendelea kupoteza maisha ya Watu
wengi na kusababisha Ulemavu wa Kudumu kwa wengine. Jeshi la Polisi kwa
kushirikiana na Wadau wengine lijipange kukabiliana na Ajali hizo kwa
umakini ili kuokoa maisha ya Watanzania yanayopotea kutokana na Ajali
ambazo zinazuilika. Hii ni pamoja na kuendelea kutoa elimu ya Usalama
Barabarani; kufanya ukaguzi wa mara kwa mara; kuwachukulia hatua za
Kisheria Madereva Wazembe na kuweka Mfumo madhubuti wa kudhibiti Mwendo
Kasi wa Magari.
USHIRIKIANO WA KIMATAIFA NA KIKANDA
86. Mheshimiwa Spika,
Serikali inatekeleza Sera ya Diplomasia ya Uchumi inayoweka umuhimu
katika ushirikiano wenye maslahi ya kiuchumi kwa Nchi yetu na Nchi
nyingine pamoja na Mashirika ya Kimataifa. Tayari tumeanza kushuhudia
mafanikio ya Sera hii kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Balozi zetu kwa kudumisha mahusiano mema na kuitangaza Tanzania katika
medani za Kimataifa. Jitihada hizo, zimewezesha kuvutia Wawekezaji
wengi, kuongeza idadi ya Watalii, fursa za kibiashara na ajira.
87. Mheshimiwa Spika,
katika kuimarisha Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki Nchi
Wanachama zinatekeleza makubaliano ya kuanzisha Vituo vya Utoaji Huduma
kwa Pamoja Mipakani (One Stop Boarder Posts). Hadi sasa ujenzi wa Vituo Vinne vya Mpakani vya Horohoro, Holili, Sirari na Mtukula uko katika hatua za kukamilika.
Pamoja
na hatua hizo, mwenendo wa biashara baina ya Tanzania na Jumuiya Afrika
ya Mashariki umezidi kuimarika ambapo mauzo nje yameongezeka kwa
Asilimia 12.8 kutoka Shilingi Bilioni 512.76 mwaka 2010 hadi Shilingi Bilioni 578.39 mwaka 2011. Serikali
inaendelea na maandalizi ya Sera ya Mtangamano ambayo itakuwa mwongozo
wa utekelezaji wa shughuli za Kitaifa za Mtangamano wa Kikanda na
Mkakati wa Utekelezaji wa Soko la Pamoja.
TAWALA ZA MIKOA NA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA
88. Mheshimiwa Spika,
mwaka 2010/2011, Serikali ilitangaza nia ya kuanzisha maeneo Mapya ya
Utawala ya Mikoa minne ya Simiyu, Katavi, Njombe na Geita pamoja na
Wilaya Mpya 19 na Tarafa 34 kwa lengo la kusogeza na
kurahisisha utoaji wa huduma kwa Wananchi. Tayari Serikali imeyaanzisha
rasmi Maeneo hayo na Uteuzi wa Viongozi wa kusimamia Mikoa na Wilaya
hizo umefanywa.
89. Mheshimiwa Spika,
ili kuwezesha Viongozi wa Mikoa na Wilaya kutekeleza majukumu yao
ipasavyo, Serikali imetoa Mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya
zote Nchini mwezi Mei, 2012. Aidha, Serikali imetekeleza ahadi yake ya
kutoa Mafunzo kwa Madiwani 4,451 Nchini. Ni imani yangu kwamba baada ya mafunzo hayo, utendaji kazi wa Viongozi hao utakuwa ni wa ufanisi zaidi.
90. Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kusogeza huduma kwa Wananchi kwa kuzipandisha hadhi
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mamlaka za Miji Midogo ya Geita,
Bariadi na Tarime zimepandishwa hadhi na kuwa Halmashauri za Miji.
Vilevile, Tangazo la kuanzishwa kwa Halmashauri za Manispaa za Lindi na
Ilemela limetolewa kwenye Gazeti la Serikali Na.182 na 256,
na Tangazo la Kupandishwa Hadhi kwa Halmashauri ya Manispaa ya Arusha
kuwa Halmashauri ya Jiji limetolewa katika Gazeti la Serikali Na. 341. Serikali inaendelea na taratibu za kuanzisha Halmashauri za Wilaya 25 Mpya zikiwemo 19 kwenye Wilaya Mpya zilizoanzishwa na sita kutokana na kugawa baadhi ya Halmashauri.
91. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa wakati nahitimisha mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Ofisi yangu mwaka jana, niliahidi kuwa Serikali itaangalia upya viwango vya Posho za Waheshimiwa Madiwani kwa lengo la kuviongeza. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba zoezi hilo limekamilika na kuanzia mwaka 2012/2013 Waheshimiwa Madiwani watalipwa Viwango Vipya vya Posho vilivyoboreshwa.
MASUALA MTAMBUKA
Jinsia
92. Mheshimiwa Spika, Ibara ya 176 ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010, inahimiza
kutambua uwezo na nguvu kubwa ya Wanawake katika kusukuma kasi ya
maendeleo na kuleta mageuzi ya Kiuchumi, Kijamii na Kisiasa. Katika
mwaka 2011/2012, Serikali
imeandaa Mkakati na Mwongozo wa Kitaifa wa Kuzuia Ukatili wa Kijinsia
Nchini. Aidha, imeunda na kuzindua Kamati ya Kitaifa ya Kutokomeza
Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto. Katika
mwaka 2012/2013, Serikali itaendelea kutoa fursa zaidi za kuwawezesha
Wanawake katika Nyanja mbalimbali pamoja na kuratibu Utekelezaji wa
Mikataba ya Kikanda na Kimataifa kuhusu Haki za Wanawake na Watoto.
Vita Dhidi ya Rushwa
93. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2011/2012, Serikali imeendelea na Mapambano Dhidi ya
Vitendo vya Rushwa Nchini. Jumla ya Tuhuma zilizopokelewa hadi Mei 2012
ni 4,498. Kati ya hizo, Tuhuma 884 uchunguzi wake umekamilika na majalada yamefunguliwa. Aidha, Kesi 612 ziliendeshwa Mahakamani; na Kati ya hizo, Kesi 478 zinaendelea na 134 zilitolewa uamuzi ambapo Kesi 46 watuhumiwa walipatikana na hatia na kuadhibiwa, Kesi 32 ziliondolewa Mahakamani kutokana na sababu mbalimbali na Kesi 56 watuhumiwa wake waliachiwa huru. Vilevile, Mafunzo kuhusu Vita Dhidi ya Rushwa yametolewa kwa Wanajamii 328,947 na Watumishi 439 wa Serikali. Katika mwaka 2012/2013, Serikali itaendelea kuchunguza Tuhuma 2,729
zilizopo na Tuhuma mpya zitakazopokelewa pamoja na kuendelea na
Uchunguzi Maalum wa Tuhuma zilizobainishwa kwenye Taarifa za Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Ubadhirifu katika Taasisi
mbalimbali za Serikali.
Mazingira
94. Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea kutekeleza Sera, Mikakati, Sheria, Kanuni na Miongozo ya
Kuhifadhi Mazingira. Miongoni mwa kazi zilizotekelezwa ni pamoja na
kuandaa Kanuni 14 za Usimamizi wa Mazingira ikiwemo Udhibiti wa
Taka, Matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa na tathmini na ukaguzi wa
athari za Mazingira. Pamoja na miongozo hiyo, Miradi 130 imefanyiwa tathmini na kupatiwa Hati za Tathmini ya Athari kwa Mazingira, Kampeni ya Upandaji Miti imeendeshwa na mafunzo kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi yametolewa. Serikali itaendelea kuzijengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza Mikakati ya Kuhifadhi Mazingira kwa kushirikiana na Wadau wengine. Serikali pia itaendelea kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi, kutoa Elimu ya Hifadhi ya Mazingira kwa Umma na kuhamasisha utekelezaji wa Kampeni ya Upandaji Miti Nchini.
Maafa
95. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2011/2012, Serikali imeshughulikia matukio ya Maafa katika
maeneo mbalimbali Nchini. Maafa hayo yalisababishwa na mafuriko,
magonjwa ya mlipuko, upepo mkali na ukame uliosababisha baadhi
ya maeneo kupata upungufu wa chakula. Ukame ulizikumba Wilaya 55 na kuathiri Watu 2,186,990 ambao walihitaji msaada wa chakula. Hadi mwezi Mei 2012, Serikali imetoa Tani 69,688 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 24.4 kwa waathirika ikiwa ni chakula cha msaada. Vilevile, imetoa Shilingi Bilioni 5.5 kwa ajili ya kusafirishia chakula hicho hadi kwa walengwa.
96. Mheshimiwa Spika,
Serikali pia iliendelea kushughulikia Waathirika wa Milipuko ya Mabomu
iliyotokea tarehe 16 Februari 2011, katika Kambi ya Jeshi ya Gongo la
Mboto, Dar-es-Salaam. Serikali inakamilisha ujenzi wa Nyumba 36 za Waathirika wa Mabomu zilizobomoka kabisa ambazo zinajengwa na SUMA JKT katika eneo la Msongola, Manispaa ya Ilala.
97. Mheshimiwa Spika, Mafuriko yaliyotokea Jijini Dar es Salaam mwezi Desemba 2011, yalikuwa na athari kubwa. Mafuriko hayo, yalisababisha Watu 41
kupoteza maisha, mali nyingi za Wananchi kupotea na miundombinu ya
barabara, madaraja, umeme na maji kuharibika. Serikali kwa kushirikiana
na Wadau mbalimbali ilichukua hatua za kuwasaidia waathirika wa mafuriko
kwa kuwapatia misaada ya kibinadamu kama vile, makazi ya muda, chakula,
mavazi, malazi na huduma za matibabu. Serikali pia imewapatia
waathirika waliokuwa wamejenga nyumba zao mabondeni viwanja katika eneo
la Ekari 360 lililopo Mabwepande, Wilayani Kinondoni ili waweze kujenga makazi mapya. Hadi mwezi Mei 2012, Kaya 1,010 zilizoainishwa kuwa katika maeneo hatarishi zaidi zimetengewa viwanja.
Vilevile, miundombinu muhimu katika eneo hilo ikiwemo maji, barabara na
umeme pamoja na huduma za afya, elimu na Kituo cha Polisi imejengwa.
98. Mheshimiwa Spika,
ili kuondoa tatizo la Wananchi kujenga katika maeneo Hatarishi,
Serikali imeziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa Nchini ziandae Mipango
endelevu ya kuwaondoa Watu wanaoishi mabondeni na kuwahamishia katika
maeneo salama. Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam tayari zimeandaa Mpango ambao utaanza kutekelezwa katika Bajeti ya mwaka 2012/2013.
99. Mheshimiwa Spika,
mwaka jana, wakati nahitimisha Hotuba ya Makadirio ya Ofisi yangu,
niliahidi kuwa Serikali itatoa Kifuta Machozi kwa Wafugaji ambao Mifugo
yao ilikufa kutokana na Ukame Mkali uliotokea mwaka 2008/2009. Athari za
Ukame huo, ni pamoja na Vifo vingi vya Mifugo, zikiwemo Ng’ombe, Mbuzi
na Kondoo katika Wilaya za Monduli, Longido na Ngorongoro. Kutokana na
hali hiyo, mfumo wa maisha wa Wafugaji wengi ulivurugika kwa kuwa Uchumi
wao unategemea zaidi Ufugaji. Baada ya tathmini kufanyika, Serikali iliamua kutoa mifugo ya kianzio (seed stock) ili kuziwezesha Kaya zilizopoteza Mifugo yote kuendeleza ufugaji. Utekelezaji
wa zoezi hilo umeanza na utaendelea katika kipindi cha mwaka
ujao wa fedha. Napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
uamuzi wake wa busara wa kuwawezesha Wafugaji hao na kushiriki yeye
binafsi katika uzinduzi wa Mpango huo uliofanyika tarehe 19 Februari
2012, Wilayani Longido.
100. Mheshimiwa Spika, Katika
mwaka 2012/2013, Serikali itajenga uwezo zaidi wa Nchi yetu wa Kuzuia,
Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa na kurejesha hali ya kawaida kwa
Waathirika. Aidha, Serikali itakamilisha maandalizi ya Sheria Mpya ya
Menejimenti ya Maafa, mapitio ya Sera ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka
2004 na Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Sera hiyo.
Udhibiti wa UKIMWI
101. Mheshimiwa Spika, Tanzania ni moja kati ya Nchi 32
Duniani ambazo zimethibitishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuweka
jitihada kubwa za kupunguza kiwango cha maambukizi mapya ya UKIMWI kwa
Asilimia 25. Mafanikio hayo yanatia moyo kwamba mkazo unaotiliwa
na Serikali na Wadau wengine umeanza kuzaa Matunda. Hata hivyo, jitihada
zaidi zitahitajika kutoka kila Sekta, Asasi Zisizo za Serikali,
Wananchi na Watu Binafsi katika Mapambano Dhidi ya VVU na UKIMWI.
102. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imeweka jitihada kubwa za kuendelea kupunguza Maambukizi Mapya, Vifo vitokanavyo na UKIMWI na Unyanyapaa. Hadi Desemba 2011, jumla ya watu 1,125,211 wamepata huduma na Ushauri Nasaha na Upimaji wa VVU kwa hiari. Aidha, Watu wanaoishi na VVU wapatao 412,108 wanapata Dawa za ARV’s chini ya Mpango wa Taifa wa Matunzo na Matibabu. Katika mwaka 2012/2013, Serikali
itaimarisha Uratibu wa shughuli za UKIMWI hasa katika Asasi za Kiraia
na kuongeza juhudi za uraghibishaji na uhamasishaji kwa Umma. Serikali
pia itaandaa Mkakati wa Tatu wa Kitaifa wa Mapambano dhidi ya UKIMWI na
kufanya mapitio ya Mkakati wa Kinga Nchini.
Dawa za Kulevya
103. Mheshimiwa Spika, Serikali
imejizatiti kukabiliana na tatizo la usafirishaji na matumizi ya Dawa
za Kulevya nchini. Katika kipindi cha Julai 2011 hadi Februari 2012,
Kilo 349 za Dawa za Kulevya za Viwandani, Kilo 48,227 za Bangi na Kilo 10,680
za Mirungi zilikamatwa. Hali hii si nzuri na ni dalili tosha
kuwa nguvu zaidi zinahitajika ili kukabiliana na janga hili kubwa kwa
Jamii yetu. Serikali itaendelea kutoa Elimu kwa Umma juu ya madhara ya
Dawa za Kulevya, kufanya misako na operesheni katika maeneo mbalimbali
na kuendelea kuteketeza mashamba ya bangi. Aidha, Serikali itaimarisha
na kuboresha Huduma za Tiba na Utengemao kwa Waathirika wa Dawa za
Kulevya. Napenda kuwatahadharisha wale wote wanaojihusisha na biashara
hiyo haramu kwamba Tanzania siyo Kituo cha Kupitisha au sehemu ya
kufanyia Biashara ya Dawa za Kulevya. Vyombo vya Usalama vimeimarishwa
ili kudhibiti Biashara hiyo. Nachukua fursa hii kukishukuru na
kukipongeza Kikosi Maalum cha Serikali cha Kupambana na Dawa za Kulevya
ambacho kimefanya kazi kubwa ya kukamata dawa nyingi zilizoingizwa
Nchini. Nawasihi waendelee kufanya kazi hiyo kwa moyo zaidi ili
kuepusha Nchi yetu na athari kubwa zitokanazo na matumizi ya Dawa za
Kulevya.
Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma
104. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2011/2012, Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma
imefanya Mapitio ya Mpango Kabambe wa Kuendeleza Mji Mkuu Dodoma ili
kuzingatia kasi ya ukuaji wa Mji huo. Aidha, mapitio ya Ikama na
Muundo wa Utumishi umefanyika kwa lengo la kuongeza ufanisi wa
kiutendaji wa Mamlaka. Kazi nyingine zilizofanyika ni ujenzi wa Barabara
zenye urefu wa Kilomita 27 katika maeneo ya Ipagala, Area E, Chang’ombe Extension, Mwangaza, Chidachi na inaendelea na ujenzi wa Barabara zenye urefu wa Kilomita 15
kwa kiwango cha Lami katika maeneo ya Kisasa na Chang’ombe. Aidha,
Mamlaka imepata Mkopo kutoka Benki ya CRDB wa jumla ya Shilingi Bilioni 16 kwa ajili ya uwekaji wa miundombinu ya maji, umeme na barabara zenye jumla ya urefu wa Kilomita 20.6 kwa kiwango cha Lami katika eneo la Uwekezaji la Njedengwa.
105. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu itafanya kazi ya kusanifu Mipango ya Makazi ya Uendelezaji wa Miji (Satellite Towns) katika maeneo ya Ihumwa na Hombolo. Mamlaka pia itaendelea kupima Viwanja 7,850 katika maeneo ya Iyumbu, Nzuguni na Miganga na kukamilisha upimaji wa viwanja vya zamani 1,938 katika maeneo ya Ipagala, Nkuhungu na Kisasa. Hali kadhalika, Mamlaka itajenga barabara zenye urefu wa Kilomita 11.3
kwa kiwango cha Lami katika maeneo ya Area ‘A’ na Kikuyu na kuendelea
na ujenzi wa miundombinu ya maji, umeme na barabara kwa kiwango cha Lami
katika eneo la Uwekezaji la Njedengwa. Serikali pia itafanyia kazi
mapendekezo ya Mshauri Mwelekezi aliyefanya mapitio ya Muundo wa CDA
hasa kutatua mwingiliano wa utendaji uliopo kati ya CDA na Manispaa ya
Dodoma.
Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi
106. Mheshimiwa Spika,
mwezi Novemba 2011, nililiarifu Bunge lako Tukufu kwamba Tanzania
imejiunga na Mpango wa Kimataifa wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali
kwa Uwazi (Open Government Partnership – OGP). Mpango huo
unahimiza uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa Uwazi, Utawala Bora,
Uadilifu, Mapambano Dhidi ya Rushwa na Ushirikishwaji mpana wa Wananchi
katika Mipango ya maendeleo na usimamizi bora wa Rasilimali za Taifa.
Chini ya makubaliano ya Mpango huo, kila Nchi inaandaa Mpango Kazi wa
Utekelezaji ambao ni shirikishi na unaotekelezeka kulingana na mazingira
yake. Napenda kuliarifu Bunge lako kuwa Serikali imeandaa Mpango Kazi
wa utekelezaji ambapo Sekta za Afya, Elimu na Maji zimepewa kipaumbele.
Mpango Kazi huo uliwasilishwa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi
wanaohusika na Mpango huo uliofanyika tarehe 17-18 Aprili 2012, Nchini
Brazil. Utekelezaji wa Mpango huo utaanza katika mwaka 2012/2013.
UDHIBITI WA MATUMIZI YA SERIKALI
107. Mheshimiwa Spika,
katika Mkutano wa Saba wa Bunge mwezi Aprili 2012, niliahidi kuwa
Serikali itayafanyia kazi maoni, ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na
Waheshimiwa Wabunge wakati wakijadili Taarifa mbalimbali za Kamati za
Kudumu za Bunge. Taarifa hizo ni pamoja na zile za Kamati
zinazoshughulikia Hesabu za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na
Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo ziliainisha Hoja mbalimbali za
Ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali kwa mwaka 2009/2010. Aidha, nilieleza kuwa Serikali
itawawajibisha wote waliotajwa kuhusika na ubadhirifu wa Mali ya Umma
ulioainishwa katika Taarifa hizo pale itakapothibitika kuwa Watumishi
hao wametenda makosa.
108. Mheshimiwa Spika,
Serikali imeziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Taarifa na
Hoja zote za Ukaguzi za mwaka 2009/2010, zilizotolewa na Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuzitafutia majibu fasaha katika
kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Aprili 2012. Baada ya zoezi hilo
kukamilika, Taarifa hizo zitawasilishwa Ngazi ya Mkoa ambapo watapitia
majibu ya Hoja hizo na kuziwasilisha katika Kamati ya Ushauri ya Mkoa
(RCC). Taarifa za Mikoa na Halmashauri zote zitawasilishwa Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kabla ya mwezi Novemba
2012 ili hatimaye kuandaa majibu ya pamoja na kuyawasilisha Bungeni.
109. Mheshimiwa Spika,
vilevile, Wizara, Wakala, Mashirika ya Umma na Idara za Serikali
Zinazojitegemea zimeagizwa kupitia Hoja zote zilizotolewa na
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuzifanyia kazi.
Wakala wa Serikali na Mashirika ya Umma yametakiwa kupitisha majibu ya
Hoja kwenye Bodi za Wakurugenzi kabla ya kuwasilishwa Wizarani.
Utaratibu huo utakuwa endelevu na utafanyika kila mwaka. Lengo la
Serikali ni kuhakikisha kuwa Usimamizi wa Fedha za Umma unaimarishwa
katika Ngazi zote. Majibu ya Hoja zote yatawasilishwa Bungeni ili kuongeza Uwazi na Uwajibikaji wa Fedha za Umma.
110. Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua hiyo, Watumishi
wa Umma watakaotuhumiwa kufanya ubadhirifu wa fedha za Umma
watachunguzwa na tuhuma zikibainika ni za kweli watavuliwa madaraka
waliyo nayo na kufikishwa katika Vyombo vya Sheria. Napenda kusisitiza kwamba, Serikali haitawahamisha Watumishi wa aina hiyo, bali hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa
wakiwa kwenye vituo vyao vya kazi. Natoa wito kwa Watendaji Wakuu wa
Serikali, Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika ya Umma na Madiwani
kuhakikisha wanashiriki ipasavyo katika kusimamia fedha za Umma kwa
mujibu wa Sheria, Taratibu, Miongozo na Kanuni zilizopo. Nawaagiza
Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kubandika
kwenye mbao za matangazo za Makao Makuu ya Halmashauri na katika vituo
vyote vya utoaji huduma kiasi cha fedha kinachopokelewa kila mwezi na
matumizi yake. Hii itawezesha Wananchi kufuatilia matumizi ya fedha zilizopelekwa kwa ajili ya utoaji huduma kwenye maeneo yao.
111. Mheshimiwa Spika,
Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kupunguza matumizi
yasiyo na tija, hususan ununuzi wa magari makubwa na ya kifahari ambayo
gharama za ununuzi na uendeshaji ni kubwa sana. Kuanzia mwaka
2012/2013, hatua zaidi zitachukuliwa kwa kuweka ukomo wa ukubwa wa
injini wa magari ambayo yanaweza kununuliwa na Serikali Kuu na Taasisi
zake pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Chini ya utaratibu huo, magari yatakayonunuliwa yatakuwa ni yale yasiyozidi ukubwa wa injini wa CC 3,000 kwa Viongozi na Watendaji Wakuu na yasiyozidi CC 2,000
kwa Watumishi wengine ambao wana stahili ya kutumia magari ya Serikali.
Vilevile, ili kupunguza matumizi ya magari kwa Viongozi na Watendaji
Wakuu kwa safari za Mikoani, Serikali itaanzisha vituo vya Kanda vya magari ya Serikali au kila Ofisi itatenga magari machache yatakayotumika Mikoani
kwa shughuli za kikazi. Mwongozo wa utekelezaji utatolewa. Inategemewa
kuwa utaratibu huu utapunguza matumizi ya fedha za Serikali kwa kiwango
kikubwa.
HITIMISHO
112. Mheshimiwa Spika, nimeelezea
kwa muhtasari baadhi ya shughuli ambazo Serikali imetekeleza kwa
kipindi kilichopita. Aidha, nimetoa Mwelekeo wa Kazi zitakazofanyika
mwaka 2012/2013. Kwa kuhitimisha, napenda kusisitiza mambo muhimu
yafuatayo:
a) Wote
tunatambua kuwa tumeanza kutekeleza Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa
Tume ya Kuratibu maoni kuanza kazi. Tuendelee kuwaelimisha Wananchi
kuhusu Mambo ya Msingi wakati wa kuchangia Maoni, na kwamba kila mmoja
anao wajibu na Uhuru wa kutoa Maoni yake kwenye Tume bila shinikizo
lolote.
b) Tumepitisha
Bajeti ya Serikali ambayo changamoto yake kubwa ni Rasilimali Fedha
kidogo tuliyonayo kukidhi mahitaji makubwa ya kutoa huduma bora kwa
Wananchi tunaowaongoza. Kutokana na hali hiyo, ni muhimu kujipanga
vizuri kudhibiti na kusimamia matumizi ya fedha za Umma kwa ufanisi
na tija zaidi. Serikali itaimarisha Mifumo yake ya usimamizi na
ufuatiliaji na kuhakikisha kwamba fedha za umma zinatumika kulingana na
Sheria na Kanuni za Matumizi ya Fedha za Serikali.
c) Katika
muda usiozidi miezi miwili ijayo, tarehe 26 Agosti 2012 itakuwa ni Siku
ya Sensa ya Watu na Makazi Nchini. Napenda kusisitiza kwamba uandikishaji hautakuwa wa siku moja tu, bali siku hiyo ndiyo itakayokuwa msingi wa kuhesabu watu waliolala katika Kaya husika. Kazi hiyo itaendelea kwa siku saba
hadi tarehe 2 Septemba 2012. Natoa wito kwa Wananchi kutoa ushirikiano
kwa Makarani wa Sensa na kujitokeza kuhesabiwa na kuhakikisha kwamba
kila mtu anahesabiwa mara moja tu. Aidha, Viongozi katika Ngazi zote
wana wajibu mkubwa wa kuwahamasisha Wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki
kwenye Sensa.
113. Mheshimiwa Spika, kabla
ya kumaliza Hotuba yangu, nimwombe Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia
(Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa atoe maelezo ya Mapitio ya Kazi zilizofanyika katika
mwaka 2011/2012 na Mwelekeo wa Kazi za Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa kwa mwaka 2012/2013. Ni matumaini yangu kwamba
maelezo hayo yatawezesha Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kufahamu kwa
upana shughuli zinazotekelezwa na Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
SHUKRANI
114. Mheshimiwa Spika, nitumie
fursa hii sasa kuwashukuru Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa ushirikiano
walionipa katika kipindi hiki. Aidha, nawashukuru Watumishi wote wa
Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Yohana Sefue kwa kukamilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka
2012/2013. Nawashukuru Watanzania wote na Washirika wetu wa Maendeleo
kwa Michango yao ambayo imewezesha Serikali kutoa huduma mbalimbali kwa
Wananchi.
115. Mheshimiwa Spika, vilevile,
napenda kuwashukuru Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, Mbunge wa
Ismani, Waziri wa Nchi (Sera, Uratibu na Bunge); Mheshimiwa Dkt. Mary
Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, Waziri wa Nchi (Uwekezaji na
Uwezeshaji); Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara
Vijijini, Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa;
Mheshimiwa Aggrey Joshua Mwanry, Mbunge wa Siha, Naibu Waziri, Ofisi
ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na Mheshimiwa
Majaliwa Kassim Majaliwa, Mbunge wa Ruangwa, Naibu Waziri, Ofisi
ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) kwa
ushirikiano walionipa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri
Mkuu. Shukrani za pekee kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa jitihada
walizoonesha katika kipindi hiki. Nawashukuru vilevile Wafanyakazi wote
wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Uongozi wa Makatibu Wakuu, Bwana
Peniel Moses Lyimo na Bwana Hussein Athuman Kattanga na Naibu Makatibu
Wakuu, Bwana Charles Amos Pallangyo, Jumanne Abdallah Sagini na Alphayo
Japan Kidata kwa ushauri wao wa Kitaalam ambao wamenipa mimi na
Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi katika kipindi hiki. Nawashukuru kwa
kukamilisha maandalizi yote ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi
ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2012/2013.
116. Mheshimiwa Spika,
kipekee napenda nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kwangu na kuendelea
kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu ipasavyo. Pia, ninamshukuru
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa ushirikiano
mkubwa wanaonipa katika kuwatumikia Watanzania. Vilevile, ninawashukuru
Waheshimiwa Wabunge, Viongozi wote wa Kitaifa na wa ngazi nyingine zote
kwa ushirikiano wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Kwa umuhimu
wa kipekee, napenda kuwashukuru Wapiga Kura wangu kwa imani na
ushirikiano wanaoendelea kunipa katika kuleta maendeleo ya Jimbo la
Katavi. Naomba pia nitumie fursa hii kumshukuru sana sana Mama Tunu
Pinda kwa uvumilivu wake na msaada mkubwa anaonipa katika kutekeleza
majukumu yangu mazito. Vilevile, nawashukuru sana Watoto wangu ambao
mara nyingi wamekuwa wakinitia moyo na wamekuwa na uvumilivu mkubwa
wanaponikosa kwa sababu ya kazi. Wote nasema, Asanteni sana kwa kunipa
nguvu ya kutekeleza majukumu yangu. Nyote nawashukuru sana!
MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU, OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA NA OFISI YA BUNGE YA MWAKA 2012/2013
117. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/2013, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Sabini na Sita, Milioni Mia Saba Tisini na Nne, Laki Nane Thelathini na Nane Elfu (176,794,838,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Sitini na Nane, Milioni Mia Tano Ishirini na Mbili, Laki Nane Sitini na Sita Elfu (68,522,866,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Mia Moja na Nane, Milioni Mia Mbili Sabini na Moja, Laki Tisa Sabini na Mbili Elfu (108,271,972,000) ni kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo.
118. Mheshimiwa Spika, vilevile, kwa mwaka 2012/2013, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Asasi zake inaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Themanini na Sita, Milioni Mia Nane Tisini na Moja, Laki Tano Tisini na Nane Elfu (186,891,598,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Moja Sitini na Nne, Milioni Mia Sita Kumi na Nne, Laki Saba Ishirini na Sita Elfu (164,614,726,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Ishirini na Mbili, Milioni Mia Mbili Sabini na Sita, Laki Nane Sabini na Mbili Elfu (22,276,872,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
119. Mheshimiwa Spika, Ofisi za Wakuu wa Mikoa zinaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Sabini na Tatu, Milioni Mia Mbili Sabini na Sita, Laki Saba Sitini na Moja Elfu (173,276,761,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Moja Arobaini na Sita, Milioni Mia Tano Hamsini na Mbili, Laki Mbili Sitini na Mbili Elfu (146,552,262,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Ishirini na Sita, Milioni Mia Saba Ishirini na Nne, Laki Nne Tisini na Tisa Elfu (26,724,499,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo. Aidha, Halmashauri zote zinaombewa jumla ya Shilingi Trilioni Tatu, Bilioni Mia Mbili Sabini na Tisa, Milioni Mia Nane; na Sabini na Tano Elfu (3,279,800,075,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi
Trilioni Mbili, Bilioni Mia Saba Thelathini na Tano, Milioni Mia Sita
Arobaini na Sita, Laki Moja Kumi na Saba Elfu (2,735,646,117,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Mia Tano Arobaini na Nne, Milioni Mia Moja Hamsini na Tatu, Laki Tisa Hamsini na Nane Elfu (544,153,958,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
120. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano inaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Kumi na Tatu, Milioni Mia Mbili Ishirini, Laki Sita Hamsini na Tatu Elfu (113,220,653,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo Shilingi Bilioni Mia Moja Kumi na Moja, Milioni Mia Tano Themanini na Tano, Laki Sita Hamsini na Tatu Elfu (111,585,653,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Moja na Milioni Mia Sita Thelathini na Tano (1,635,000,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
MUHTASARI
121. Mheshimiwa Spika, baada
ya maelezo haya kwa muhtasari, naomba sasa Bunge lako Tukufu likubali
kuidhinisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2012/2013 ya jumla
ya Shilingi Bilioni Mia Moja Kumi na Tatu, Milioni Mia Mbili Ishirini, Laki Sita Hamsini na Tatu Elfu (113,220,653,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, na jumla ya Shilingi
Trilioni Tatu, Bilioni Mia Nane Kumi na Sita, Milioni Mia Saba Sitini
na Tatu, Laki Mbili Sabini na Mbili Elfu (3,816,763,272,000) kwa
ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa ikiwa ni Matumizi ya Kawaida na Fedha za Maendeleo
za Ndani na Nje kwa ujumla wake.
122. Mheshimiwa Spika,
pamoja na Hotuba hii, yapo Majedwali ambayo yanafafanua kwa kina
Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake,
Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya
Bunge.