HOTUBA YA MWENYEKITI WA TUME YA KUUNDA KATIBA
- Get link
- X
- Other Apps
Tuesday, June 19, 2012
Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba, Katibu wa Tume
Assaa Rashid (kushoto kwa Mwenyekiti) na Dkt. Salim Ahmed Salim, Mjumbe
wa Tume katika mkutano Ukumbi wa Karimjee.
|
Ndugu Wanahabari,
Nianze kwa kuwashukuru kwa kuitikia mwaliko wetu. Tume ya Mabadiliko ya
Katiba ilianza kazi mwanzoni mwa Mwezi Mei, 2012 na kipindi hiki
tumekitumia kwa maandalizi na sasa tuko tayari kuanza awamu ya kwanza ya
kazi yetu, yaani kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi. Baada ya
hapo itafuata awamu ya pili ya kuandaa taarifa, mapendekezo na Rasimu
ya Katiba Mpya. Baadaye Tume itakutana na Mabaraza ya Katiba na mwisho
Rasimu ya Katiba itafikishwa kwenye Bunge Maalum.
Kabla ya kuanza mchakato wa kushauriana na wananchi, ikiwa ni pamoja na
safari za mikoani, tumeona ni muhimu na busara kukutana na nyinyi
kwanza. Vyombo vya habari ni wadau wakubwa katika mchakato huu. Tume
inaamini kwamba vyombo vya habari vina nafasi kubwa sana katika
kufanikisha mchakato mzima hasa katika kutangaza maoni ya wananchi ili,
licha ya kukusanya maoni tu, mchakato uwasaidie wananchi kubadilishana
mawazo kuhusu aina ya Taifa wanalolitaka na aina ya Katiba
wanayoitaka.
Ndugu Wanahabari,
Pamoja nami leo Wajumbe wote wa Tume, ikiwa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti - Jaji Augustino Ramadhani, Katibu na Naibu Katibu.
Jukumu tulilokabidhiwa ni kubwa na muhimu kwa Watanzania, hivyo basi
matayarisho tuliyokuwa tunayafanya yalikuwa na lengo la kuhakikisha
mchakato mzima unakwenda kama ilivyokusudiwa.
Katika maandalizi yetu, tulitambua umuhimu wa elimu kwa umma kuhusu
mambo yatakayozingatiwa katika Katiba. Ni wazi kuwa wananchi hawawezi
kutoa maoni yao kwa ukamilifu bila ya kuwa na elimu ya kutosha. Kwa
hiyo, kwa kuzingatia umuhimu huo, Tume imetumia muda mwingi kupata na
kuandaa nyaraka muhimu kwa ajili ya kuwapatia wananchi elimu ya
kutosha.
Tume imepata nakala elfu mia tano za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya
1977, nakala elfu kumi za Katiba ya Zanzibar ya 1984 na nakala elfu mia
tano za Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83. Kwa kutambua kwamba
nyaraka hizi hazitoshi, na hata kama zikipatikana kwa wingi ni vigumu
kwa wananchi kuzisoma na kuzielewa kwa urahisi, Tume imeandaa nyaraka
ambazo ni rahisi kuzisoma na kuzielewa.
Nyaraka hizo ni Katiba ya Jamhuri ya 1977, Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, Sura ya 83, kwa lugha nyepesi, Hadidu za Rejea, Program ya
Elimu kwa Umma na Utekelezaji wa Kazi za Tume. Nyaraka hizi tumeanza
kuzisambaza na leo, tunawakabidhi nyinyi nyaraka zote ili msaidie
kuzitangaza na kuelemisha wananchi. Aidha, Tume imeandaa vipeperushi
kuhusu kazi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Maswali Yanayoulizwa
Mara kwa Mara.
Ndugu Wanahabari,
Hivi karibuni Tume itaanza safari za mikoani. Tume imejigawa katika
makundi saba na kila kundi litafanya safari nne mikoani kati ya sasa na
mwisho wa mwaka. Kila kundi litafanya kazi katika mkoa kwa wastani wa
mwezi mmoja isipokuwa kwenye mikoa iliyo midogo kwa eneo, ambapo Tume
itatumia muda mfupi. Tutaanza na mikoa minane ambayo ni Dodoma, Kagera,
Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga.
Tunaomba wananchi wajitokeze kwa wingi na kutoa maoni yao kwa uhuru,
uwazi, bila ya hofu yoyote na kwa utulivu. Tunaomba wananchi wawe
wavumilivu na watoe maoni bila jazba au kubeza. Tunaomba wananchi wawe
wavumilivu sana kusikiliza mawazo ya wengine hata kama hawakubaliani na
mawazo hayo.
Lengo letu kama Tume, ni kuhakikisha kuwa Watanzania kwa jumla wanatoa
maoni yao. Tungependa sana kama ingeliwezekana, kila Mtanzania apate
fursa ya kutoa maoni yake. Lakini, ukizingatia ukubwa wa nchi yetu na
mazingira halisi, ni wazi haitawezekana kuonana na kila mtu. Pamoja na
hivyo, ni kusudio letu kufanya kila linalowezekana kupata mawazo ambayo
yataonyesha matakwa, mategemeo na mahitaji ya Watanzania wote. Katika
upeo huo, basi tutafanya kila jitihada kwa njia mbali mbali kujaribu
kuhakikisha kwamba maoni ya Watanzania kwa ujumla yanawasilishwa na
kufanyiwa kazi vilivyo.
Pamoja na mikutano mbali mbali itakayofanyika katika mikoa yote,
tutakuwa na mfumo wa kupokea maoni ya Watanzania wa kutoka pande zote
za ndani ya nchi na nje ya nchi kupitia simu, barua pepe, mitandao ya
kijamii kama facebook, twitter na blogu na tovuti na pia kwa njia ya
posta. Tunaomba wananchi wajitahidi kutoa hoja badala ya malalamiko
peke yake. Mapendekezo ya mambo ya kuingia kwenye Katiba yatasaidia
sana badala ya malalamiko tu.
Tume, kwa kiwango fulani imeanza kuratibu maoni ya wananchi
yanayotolewa kwa njia mbali mbali. Mwelekeo wa kubaini maeneo ya
kufanyia kazi unaanza kuonekana, hasa kuhusu taasisi za dola kama vile
Serikali na vyombo vyake vyote na madaraka ya viongozi na taasisi mbali
mbali. Tume inaomba maeneo mengine muhimu nayo yapewe uzito, hasa
maeneo yaliyo katika Sura ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977. Sehemu hiyo ndiyo moyo wa Katiba. Yapo maeneo
manne muhimu ambayo Tume ingependa kupata maoni ya wananchi.
Eneo la Kwanza, linahusu misingi ya Taifa. Misingi ndiyo nguzo ya
utamaduni wa nchi na wananchi wake; misingi ndiyo nguzo ya nidhamu ya
nchi na wananchi wake; misingi ndiyo nguzo ya maadili ya nchi na
wananchi wake. Katiba yetu imetaja misingi mikuu kuwa ni uhuru, haki,
udugu, amani, demokrasia na Serikali kutofungamana na dini yoyote
ingawa wananchi wana uhuru wa kuabudu. Misingi hii ndiyo nguzo ya
mshikamano na utulivu wa wananchi. Baadhi ya watu wanasema ama misingi
hii haitoshi au imetelekezwa. Wengine wanasema inatosha. Tume ingependa
kupata maoni ya wananchi kuhusu eneo hili.
Eneo la Pili, ni kuhusu mamlaka ya wananchi. Katiba ya sasa inaeleza
kwamba wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na msukumo mkubwa wa
mchakato huu wa kupata Katiba Mpya ni matakwa ya kuwawezesha wananchi
kutunga Katiba yao. Lakini kuna watu wanasema mamlaka ya wananchi
hayakufafanuliwa, wanasema mamlaka ya taasisi za dola kama vile
Serikali, Bunge, Mahakama, Tume mbali mbali za kikatiba, na hata Vyama
vya Siasa, yamefafanuliwa. Lakini mamlaka ya wananchi hayakufafanuliwa
na wala hakuna utaratibu wa kuyatumia madaraka hayo. Wanasema wananchi
wanatumiwa tu kisiasa wakati mamlaka yao yote yameporwa. Wengine
wanasema mamlaka hayo yapo isipokuwa wananchi wameyakasimu kwa taasisi
mbali mbali. Tume ingependa kupata maoni ya wananchi kuhusu eneo hili.
Eneo la Tatu, ni malengo muhimu na misingi ya mwelekeo wa shughuli za
Serikali. Malengo hayo yameelezwa vizuri sana katika Ibara ya 9 ya
Katiba. Baadhi yake ni:-
•Kwamba utu na haki nyinginezo zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa;
•Kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo
zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na
unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu
kumnyonya mtu mwingine;
•Kwamba mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi;
•Kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini.
•Kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya
wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada za kuondosha
umaskini, ujinga na maradhi;
•Kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha
ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu
wachache binafsi.
Malengo haya ndiyo ndoto (vision) ya wananchi. Malengo haya ndiyo
yanajumuisha matumaini ya Watanzania kuhusu aina ya Tanzania
wanayoitaka. Mgawanyo wa madaraka kwa mamlaka mbali mbali za dola
unakusudiwa kuhakikisha kwamba malengo haya yanafikiwa.
Baadhi ya watu wanasema kuwa malengo haya yanatosha ila hayatekelezwi
kwa ukamilifu. Wengine wanasema kuwa hayatoshi katika zama hizi. Tume
ingependa kupata maoni ya wananchi kuhusu malengo muhimu ya Taifa. Tume
itapenda kufahamu ndoto za wananchi kuhusu rasilimali za Taifa na
jinsi ya kuzilinda, kuziendeleza na kuzitumia kwa ajili ya maendeleo ya
wananchi.
Tume ingependa kusikia ndoto za wakulima, wafanyakazi, wafugaji,
wavuvi, wafanya biashara wakubwa na wadogo, wanaume, wanawake, wazee,
vijana, walemavu na kadhalika.
Eneo la Nne, ni haki za binadamu na wajibu kwa jamii. Sehemu ya Tatu ya
Sura ya Kwanza ya Katiba ina orodha ndefu ya haki na wajibu muhimu kwa
raia. Baadhi ya watu wanasema haki hizi hazitoshi. Wengine wanasema
haki za mtu binafsi zinadhulumu haki za jamii na wengine wanasema haki
za binadamu zinaminywa au hazitekelezwi kwa ukamilifu au zinavunjwa.
Tume inapenda kupata maoni ya wananchi.
Ndugu Wanahabari,
Awamu ya Pili ya uratibu na ukusanyaji wa maoni ya wananchi itafanyika
kupitia Mabaraza ya Katiba. Wakati huo, Tume itawaomba wananchi watoe
maoni yao kuhusu Rasimu ya Katiba. Kupitia kwenu, naomba wananchi
kufika kwa wingi katika mikutano ya ukusanyaji wa maoni katika awamu
zote mbili. Nawaomba wananchi kutoa mawazo yao kwa uwazi na bila ya
hofu yoyote. Tume itafanya kazi zake kwa uhuru, uwazi na
tunawahakikishia kwamba maoni yote yatakayotolewa na wananchi, taasisi,
asasi za kiraia na makundi mengine yote yataheshimiwa na kufanyiwa
kazi ipasavyo.
Ndugu Wanahabari,
Nimalizie kwa kurudia tena kwamba jukumu la vyombo vya habari ni kubwa
katika kufanikisha kupatikana kwa Katiba Mpya. Pamoja na mambo mengine,
wananchi wa sehemu moja ya nchi watafahamu maoni ya wenzao katika
sehemu nyingine ya nchi. Naomba mlikubali jukumu hili ili kusaidia nchi
ipate Katiba Mpya iliyo nzuri.
Nawashukuru.
TOA MAONI, TUPATE KATIBA MPYA.
- Get link
- X
- Other Apps