Mh. Vuai Ali Vuai


ZANZIBAR, 29-5-2012.

Chama cha Mapinduzi kimetoa shindikizo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kumtaka  Waziri wa Sheria na Katiba wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Abubakar Khamis Bakar ajiuzulu kwa madai ya kushindwa kuishauri vizuri serikali katika suala la kudhibiti asasi za kiraia ikiwemo uamsho.
     Aidha chama cha mapinduzi kimetaka kufutwa mara moja kwa jumuiya ya uamsho kwa sababu imekwenda kinyume na malengo yake ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ambayo kazi yake kutoa elimu kuhusu mihadhara ya dini ya kiislamu tu.
     Akizungumza na waandishi wa habari hapo makao makuu ya CCM Kisiwandui mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Vuai Ali Vuai amesema leo, kuwa  kikundi cha kutoa mihadhara ya dini ya kiislamu cha Uamsho kimesajiliwa kwa ajili ya kutoa mihadhara ya mambo ya dini tu na sio kujishungulisha na siasa za majukwaa ikiwemo kuwahoji wananchi kuhusu uhalali wa muungano na kuwakashifu viozngozi wa serikali ikiwemo waasisi wa taifa hili.
     Alisema kitendo cha Waziri wa katiba na sheria kushindwa kuishauri vizuri serikali kuhusu mwenendo wa kikundi hicho ndiyo kimesababisha maafa makubwa na kuiingiza nchi katika wasiwasi mkubwa kiasi kuvurugika kwa sekta ya biashara na utalii.
     'Chama Cha Mapinduzi, kinamtaka waziri wa sheria na katiba wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujiuzulu mara moja kwa sababu ameshindwa kumshauri vizuri rais pamoja na serikali kuhusu mwenendo wa kikundi cha uamsho ambacho kinafahamika kwamba kazi yake kutoa mihadhara ya kidini tu na siao siasa'alisema Vuai.
     Akifafanua zaidi Vuai alisema kwa mfano vyama vya hiari vyote vilivyopata usajili wa kudumu wa kufanya shunguli zao vinasajiliwa katika ofisi ya katiba na sheria ambayo ipo katika wizara yake.
    Aidha alisema mawaziri wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar walikutana pamoja na viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa uamsho tarehe 25 Aprili na kutaka kikundi hicho kuacha kufanya mihadhara inayohusiana na mambo ya siasa au kitachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
      Kwa mfano alisema hivi karibuni jeshi la polisi lilizuwia utoaji wa vibali kwa viongozi wa chama hicho lakini vibali vilitolewa katika ofisi za mufti ambazo zipo chini ya wizara ya katiba na sheria.
     'Tulimtaka waziri wa katiba kulifanyia kazi suala hilo kuona kwamba kikundi hicho hakifanyi mihadhara inayohusiana na mambo ya siasa ikiwemo kuwakashifu viongozi na kuhoji uhalali wa muungano lakini hakufanya kazi hiyo'alisema Vuai.
    Vuai alisema hivi sasa chama cha mapinduzi kimetambuwa na kufahamu kwamba jumuiya ya uamsho ipo katika kivuli cha chama kimoja cha siasa na ndiyo maana kimekuwa kikifanya kiburi na jeuri kiasi ya kutamka kwamba hakuna mtu wa kukifuta.
     Aidha Vuai alisisitiza na kuitaka serikali kuifuta taasisi ya uamsho mara moja kwa sababu imekwenda kinyume na dhamira yake ya kuanzishwa.
      'Tunaitaka serikali kuifuta mara moja taasisi ya uamsho kwa sababu imekwenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo 'alisema Vuai.
     Aidha Vuai aliwataka wafuasi wa chama cha mapinduzi kuwa watulivu katika kipindi chote na kuacha kujishungulisha na vurugu hizo ambazo zinahatarisha amani na utulivu.
     Kwa mujibu wa katiba ya jumuiya ya uamsho,taasisi hiyo itakuwa na kazi ya kutoa mihadhara ya kidini kwa waumini na wafuasi wake na kulinda haki za binaadamu kwa makundi ya waislamu mbali mbali.
     Aidha jumuiya hiyo kazi yake kusaidia matatizo ya kijamii ikiwemo migogoto na majanga mbali mbali ikiwemo waathirika wa ugonjwa wa ukimwi.
     Katiba ya chama hicho inapiga marufuku taasisi hiyo kujishungulisha na mambo ya kisiasa ikiwemo viongozi wake.

Popular posts from this blog

MAMBO 6 YA KUZINGATIA KATIKA MAHUSIANO

Mwanajeshi Aliyepiga Picha na Mbunge wa Arusha Mjini-Chadema Godbless Lema Kwenye Mkutano wa Hadhara Akamatwa

MATAJIRI WATANO WANAOONGOZA TANZANIA