MAIGE AKUMBWA NA MKASA MWINGINE

Mapema wiki hii Mbunge wetu wa jimbo la Msalala, Mh. Ezekiel Maige alitoa shutuma dhidi ya Vikao vya juu vya chama hasa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kuwa havikumuita kumhoji juu ya  tuhuma zinazomkabili.
        Lakini pili alitoa shutuma nzito dhidi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) , Ndg. Nape Nnauye, kuwa yeye ni gamba namba moja linalotakiwa kuvuliwa, kwa kile kinachodaiwa kutokuwa na mkakati wa kuzuia wanachama wa CCM kuhamia vyama vya upinzani na kuingiza wanachama wapya.
       Mh. Maige anadai Nape kashindwa kubuni mbinu za kuingiza wanachama na zaidi kupambana na wimbi la kuhama kwa viongozi, makada na wanachama wa CCM.
       Kama katibu Mwenezi wa CCM Wilayani Kahama kwa kutambua umuhimu wa vikao, na kwa kuheshimu mamlaka ya kikatiba ndani ya Chama, nimeona si vema kukaa kimya bila Kutolea ufafanuzi tuhuma hizo ambazo kwa ujumla zinalenga kukivuruga na kukichafua Chama chetu.
         Chama chetu kinao utaratibu wa kushughulikia maswala ya malalamiko mbalimbali ya wanachama na viongozi wake. Utaratibu alioutumia Ndg. Maige si wa Chama chetu na haukubaliki kabisa. Hauna nia ya kujenga isipokuwa kubomoa.
         Haya mapungufu anayoyasema leo Maige kayaona baada ya kunyang'anywa uwaziri? Nape na vikao vya kitaifa vya Chama chetu vinahusikaje na kufukuzwa kwake uwaziri na shutuma zinazomkabili za matumizi mabaya ya dhamana ya madaraka aliyopewa na rasilimali za nchi kama Waziri aliyekuwa na dhamana ya Maliasili na Utalii?
        Busara inaonyesha kuwa kwakuwa kikao kilichomtuhumu na kusababisha kuwajibishwa kwake ni Bunge, nayeye ni mbunge angepeleka haya malalamiko yake huko na yakatafutiwa ufumbuzi. Vinginevyo kama ana malalamiko yoyote juu ya utendaji wa vikao vya juu vya chama na Katibu Mwenezi wa CCM Taifa Ndg. Nape Nnauye angewasilisha kwenye chama kwa kufuata utaratibu wa Chama chetu.
         Tunakemea na kulaani utaratibu huu wa watu kukurupuka na kushutumu viongozi wa chama chetu kwa staili aliyotumia Maige. Lengo lake sio jema na wala halina nia ya kujenga Chama chetu bali ni kubomoa. Nape anasemwa vibaya na watu wachache wasiowaadilifu kwasbabu ya uadilifu wake na kusimamia ukweli na msimamo wa vikao halali vya chama.
          Suala la wanachama kukihama Chama cha Mapinduzi si Suala geni kwani Mara baada ya kuruhusiwa kwa vyama vingi vya siasa nchini, asilimia kubwa ya wanachama walioenda kuanzisha na baadae wengine kujiunga na vyama vya upinzani walitoka CCM, na kwamba hatua ya wao kutoka haikusababishwa na uzembe we viongozi wa Chama wa wakati huo, bali demokrasia.
         Kwa kuwa Jambo Hilo si geni ndani ya vyama, hatua ya Mh. Maige kumshutumu Ndg. Nape kwa madai kuwa ameshindwa kuwa na mkakati madhubuti wa Kuongeza wanachama ndani ya CCM limelenga dhamira ya uchochezi na Chuki binafsi.
        Utaratibu huu wa baadhi ya wana CCM kuhama kwenda vyama vingine vya siasa umekuwepo kwa miaka 20 sasa na haujakiua Chama Cha Mapinduzi, iweje leo kujaribu kuwavunja moyo wana CCM kuwa chama chao kinakufa? Inanipa tabu kuamini kuwa kufa huko kwa CCM anakuona baada ya kunyang'anywa uwaziri.
         Tunamshauri Ndg. Maige ajipange upya kujijenga jimboni na kukijenga Chama badala ya huu utaratibu wa kuropoka hovyo barabarani kwa kuwashutumu baadhi ya viongozi wa Chama chetu.
        Asisahau kuwa shutuma zake kwa vikao vya juu vya Chama na kwa mteule wa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama na vikao hivyo, ni dharau kwa Chama chetu na dharau kubwa kwa Mwenyekiti wetu ambae aliwahi kumwamini katika umri mdogo na kumpa dhamana ambayo ameichezea mwenyewe! Wakujilaumu ni yeye mwenyewe, asitafute mchawi wa anguko lake!


Imetolewa na

MARCO MIPAWA NG'WANANGOLELWA
KATIBU WA SIASA NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI 
WILAYA YA KAHAMA

Popular posts from this blog

MAMBO 6 YA KUZINGATIA KATIKA MAHUSIANO

Mwanajeshi Aliyepiga Picha na Mbunge wa Arusha Mjini-Chadema Godbless Lema Kwenye Mkutano wa Hadhara Akamatwa

MATAJIRI WATANO WANAOONGOZA TANZANIA